Pages

Wednesday, September 19, 2012

My Article for Newspaper: Picha na fremu za ukutani



Mapambo ya picha na fremu kwenye kuta za nyumba unayoishi

Labda una picha nyingi zinazosubiri kutundikwa ukutani na unataka kupata dondoo ya jinsi ya kuzitundika. Makala hii itakuelimisha jinsi ya kupanga sanaa ya picha na fremu ukutani na kutengeneza mandhari ya ladha yako.
Kanuni kuu ni kuwa fremu na picha zitundikwe kwa urefu wa usawa na macho yako ukiwa umesimama au kiasi cha futi tano toka sakafuni. Kama kuta ni ndefu basi tundika picha juu kidogo zaidi. Ni muhimu kuchagua fremu na picha nzuri ili kuleta uchangamfu kwenye kuta. Swali laweza kuwa ni kwa vipi na wapi sanaa hizi zaweza kutundikwa ukutani? Jibu ni kuwa jiulize ni maeneo gani ya ukutani ungependa macho yaelekee.

Kutundika sanaa na picha ukutani ni njia bora ya kuunda sehemu ya kuelekeza macho. Kazi hii inahitaji mpango wa muda na inashauriwa upange picha na sanaa zako za fremu sakafuni kwanza uone ni muonekano gani unapenda. (Kwa njia hii unaweza kusogeza kupanga unavyotaka bila kuacha matobotobo ukutani!) Siri kuu ya mafanikio ya zoezi hili ni kupanga kwa kuleta uwiano. Baada ya kuridhika na mpangilio ulivyo sakafuni basi ni wakati wa kuhamishia ukutani. Tumia futi kamba kupima msatari wa eneo unalotaka kutundika kuona kuwa kuna uwiano. Kwa mfano kwa picha nne zenye fremu ndogo kushoto mwa fremu kubwa zinaleta uwiano na fremu mbili za saizi ya kati kulia kwa hiyo picha kubwa. Daima kumbuka uwiano hata kwenye kuta za chumba au ujia, usijaze mapambo ukuta mmoja na kuta nyingine zikabaki tupu kwani uwiano kwenye chumba chote utakuwa umepotea.

Tundika picha za kumbukumbu ya tukio fulani ama za familia pamoja kutengeneza staili ya kipekee. Weka picha hizo kwenye fremu za rangi moja tuseme nyeusi au rangi ya mati. Chagua ukuta halafu weka picha au fremu tatu zinazolingana ukubwa katikati ili kutengeneza eneo la kuelekeza macho, baada ya hapo ongeza mistari mingine ya picha juu na chini ya hizo tatu kwa kila fremu kuwa umbali wa inchi moja hadi mbili. Staili hii  ni nzuri kama hapo mbeleni utaamua kuongeza picha hapa na pale. Tundika karibukaribu kufanya kundi moja la fremu na picha ukutani.

Picha za ukuta wa ngazi kama unaishi kwenye nyumba ya ghorofa mpangilio wake una chagamoto kidogo wa kuja na muonekano sahihi. Ila kanuni kuu ni kuwa muonekano wa picha na fremu zilizotundikwa uendane na umbo la zile ngazi. Yaani picha ziwe zinaongezeka kwa kwenda juu mwelekeo wa ngazi. Picha hizi zikipangiliwa vizuri huwa ni pambo la ukutani lenye kuvutia na la muonekano wa kipekee. Watu wazima wengi wanaoishi kwenye nyumba za ghorofa wanapendelea kuweka picha za harusi za watoto wao kwenye ukuta wa ngazi japo wanapozeeka wanashindwa hata kupanda huko juu!

Tundika picha fulani kwenye ukuta wa sehemu fulani kama ifuatavyo:-
Kwenye kuta kubwa:  Kuta kubwa ni kama zile za kwenye ujia, ngazi au sebule. Ili kuleta ladha kwenye kuta hizi ipe kila picha nafasi ya kupumua. Kwa mfano kama ni kwenye ngazi weka picha moja halafu ruka ngazi mbili weka ya pili. Picha na fremu kubwa zinapendeza kwenye kuta kubwa na kama hauna uhakika juu ya picha gani uweke chukua picha yako au ya familia ikuze kwenye fremu na uitundike.

Juu ya Sofa:  Tundika picha na fremu umbali wa mkono mmoja toka kwenye sofa. Hakikisha mtu aliyekalia hilo sofa kichwa chake hakigusani na picha.

Mlundikano wa picha: Tundika picha kwenye kundi moja karibu karibu ili kutengeneza sehemu ya kuelekeza macho. Amua umbo la kikundi chako hicho cha picha kiwe ni yai au boksi. Hii inawezekana kwenye kuta zenye nafasi kubwa au ndogo kama sebuleni na chumba cha kulala, kutegemea na muonekano unaoutaka.

Mlazo: Kwa kutundika picha kadhaa kwa mstari wa kulala inaleta hisia ya nafasi. Hii pia inapendeza kwenye ujia na chumba cha kulala.

Kuamua ni wapi na vipi uweke ukutani mapambo yako ya sanaa ya fremu na picha kutakupa uamuzi wa saizi na umbo la sanaa unazotaka kununua. Pale unapokuwa unajua ukuta husika unaotaka kutundika picha ni wa shughuli gani, rangi na staili basi unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya manunuzi yanakayoendana na mandhari hayo.

Kutundika picha na sanaa za fremu kwenye kundi au moja moja imekuwa ni njia sahihi ya kuhuisha kuta za nyumba.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange 0755  200023

No comments:

Post a Comment