Pages

Wednesday, November 14, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya msimu wa sikukuu




Njia chapchap za kupamba ndani na nje ya nyumba yako msimu huu wa sikukuu

Chochea furaha na msisimko wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kupamba ndani na nje ya nyumba yako. Vitu rahisi hata  kama ni vijipambo vya meza tu huleta tofauti kubwa ya muonekano wa mazingira ya nyumbani.

Baadhi ya njia tofauti unazoweza kuhuisha muonekano wa kizamani wa nyumba yako ni kama ifuatavyo:
Ongeza picha: Kuongeza picha nyumbani kwako kunaongeza muonekano mpya mara moja kutoka ule wa zamani. Ni njia rahisi kabisa kuhuisha sebule yako. Au unaweza kuongeza picha za familia yako ama nunua picha za fremu kuleta muonekano wa kipekee.
Mimea na maua: Pamba mazingira ya ndani na nje ya nyumba kwa maua na mimea. Vesi ya maua au mmea uliooteshwa kwenye chungu kwenye kona ya mahali ndani mwako vinaleta mvuto.
Badili pazia: Hizo pazia za kila siku zinafanya nyumba isionekane tofauti au na mvuto kwa ajili ndio hizo hizo kila siku. Hakuna kitu kinacholeta tofauti kubwa kwenye muonekano wa nyumba kama pazia. Weka mapazia ya aina, mitindo na vitambaa na mishono mbalimbali.
Rangi:  Kupaka rangi ni njia iliyozoeleka zaidi wakati wa kusheherekea. Zimua kuta za mazingira ya nyumbani kwako japo kwa kuongeza koti moja tu ya rangi. Kama labda kupaka rangi chumba kizima ni gharama na kazi kubwa basi paka hata mlango tu.
Weka mito mipya: Badilisha mito ya sebuleni kwako na uweke ya rangi mbalimbali. Mito yenye rangi kali zilizokolea kwenye sofa zako au hata ile mikubwa ya kukalia sakafuni inabadilisha muonekano wa ndani ya nyumba bila ya kutumia gharama au kazi kubwa.
Panga vitu upya: Sio cha zaidi bali tu ni kuhamisha tuseme fenicha moja toka eneo moja hadi lingine. Kufanya hivyo utashangaa jinsi itakavyohuisha muonekano wa mahali.
Pamba eneo la lango kuu:  Kinachoonekana kwanza kinamkaa mtu moyoni daima kwa hiyo unaweza ukahuisha muonekano wa kuingialia nyumbani kwa kupamba eneo la kuingilia. Kwa mfano vyungu vya maua vya chini au vya kuning’inia lango kuu vitaleta mvuto wa kipekee.
Boresha fenicha: Paka rangi fenicha ya zamani au hata ibadili kuongeza matumizi yake. Hii haitaleta tu muonekano mpya bali pia itaongeza thamani na matumizi ya fenicha hiyo.
Weka virembo vidogodogo:  Katika nyumba nyingi utakuta kuna sehemu ambazo unaweza kuweka virembo vidogodogo kama vile juu ya kabati au shelfu na kadhalika. Kutumia nafasi hizi kuweka marembo kutaleta mvuto ndani ya nyumba na kuongeza uzuri wa kutazama na kushangaa.
Mapambo ya msimu:  Vitu vya wakati husika vyenye mvuto vinaweza kuwekwa kama mapambo nyumbani bila hata kutoa jasho. Kwa mfano unaweza weka matunda au maua ya msimu kwenye bakuli la kuvutia, au vesi na kuweka mezani na ikavutia sana.                                                                                      
Pia unaweza kuzungushia taa zisizo na gharama za msimu wa sikukuu kwenye miti ya bustanini au eneo la lango kuu au hata eneo la ngazi wakati wa sikukuu na kuleta muonekano wa maajabu.
Kama tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zinazokuja ni krismasi na mwaka mpya hivyo usisahau kupamba kwa mti wa krismasi! Mti huu umekuwa ni pambo la kipekee kwenye nyumba nyingi duniani na hata maeneo ya jumuiya na ofisi nyingi kila mwaka kwenye sikukuu ya krismasi.

Kama unataka kuongeza viungo vya mapambo kwenye nyumba yako yenye muonekano wa siku zote wala huhitaji kutumia gharama kubwa. Mabadiliko kidogo lakini yeye mashiko yatafanya nyumba yako kuonekana upya. Kutembea kwenye nyumba inayoonekana tofauti wakati wa sikukuu kiukweli kutahuisha na kuongeza msisimko wa sikukuu. Hutakiwi kuwa mtaalamu wa mapambo ya nyumbani ili kuleta mabadiliko haya. Kinachotakiwa tu ni kuwa mbunifu wa kufikiri. Jinsi ya kushehereke sikukuu ni kupamba nje na ndani ya nyumba kwa vitupio murua. Kutegemeana na ladha yako unaweza kupamba kwa rangi zilizozoeleka kwa sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo ni Top of ForBnyekundu, nyeupe na kijani. Mawazo ya upambaji ni lukuki, kutegemea na bajeti, ladha binafsi na mazingira ya makazi yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni tuwasiliane viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.

No comments:

Post a Comment