Pages

Friday, January 18, 2013

My article for newspaper: Jinsi ya kupamba kwa vioo


Jinsi ya kupamba  nyumba yako kwa kutumia vioo

Kwa uchache kila binadamu anapenda vioo. Huenda unajiuliza kama kuna sehemu nyumbani kwako ambayo hupaswi kuweka kioo. Kupata jibu la swali hili kwanza jiulize ni nini kinachooonekana  kwenye kioo hicho. Ni kitu ambacho unakipenda zaidi? Kama una kioo kinachotazamana na kabati lenye mrundikano wa vitabu basi ukiangalia kwenye kioo hicho unaona makabati mawili yenye mrundikano wa vitabu! Na vile vile kioo kinachotazamana na picha nzuri kitakuonyesha picha mbili nzuri.

Vioo vinaweza kufanya mwanga wa nje uje ndani na kuleta mng’ao ndani ya nyumba. Weka kioo kitazamane na dirisha na mara moja mahali panafunguka. Kioo pia kinaweza kusaidia kufanya sehemu nyembamba kuonekana pana. Weka kioo kwa jinsi ambayo kitanasa mwanga wa asili kutokea dirishani; kwa hiyo mwanga utadunda kurudi chumbani. Hii ni dondoo muhimu  kwa mapambo ya ndani kwa vyumba vyenye mwanga hafifu.

Sehemu mojawapo ya kuepuka vioo ni chumba cha chakula. Sijui yeyote ambaye angependa kujiangalia kwenye kioo wakati anakula. Mazingira ya nyumbani yawe yanafanikisha malengo yako. Chochote kinachokufanya usijisikie vizuri hakisaidii kufanikisha malengo hayo.

Swala la vioo kwenye chumba cha kulala ni la mtu binafsi.  Ingawa vioo ni muhimu kwenye chuma hiki ila sio vitazamane na kitanda. Ukubwa na mahali pa kuweka ni vitu muhimu vya kuzingatia. Ukuta uliotundikwa kioo kwenye chumba cha kulala mara nyingine unaweza kuondoa mazingira ya hisia kuwa chumba cha kulala ni kama mahali patakatifu. Ni nani anapenda kujiona sehemu kubwa ya mwili wake? Jaribu kufunika vioo vikubwa usiku ili kuleta usingizi mwororo.

Watoto ni wadadisi wa mazingira yao. Mara nyingi wanaogopeshwa na vivuli wanavyoona kwenye vioo usiku. Watoto wengi wanaogopa kuwa kwenye vyumba vyao hasa usiku kwa ajili ya vioo. Mara chache kufunika vioo vyote usiku inasaidia, vinginevyo ni vyema kuondoa vioo kwenye kuta za vyumba vya watoto na kuvitundika kwa ndani ya milango ya makabati ya nguo.

Vioo bafuni ni kawaida sana na vina kazi kwa hivyo watu wengi wala hawafikirii kama ni mapambo ya ndani. Hata hivyo vioo vinaweza kuongeza mapambo ya chumba chochote. Vioo vikubwa vinaweza kuwa vizito zaidi; vitundikwe kwa uangalifu.

Kuweka ama kutoweka kioo kitazamane na mlango wa mbele ni swali ambalo watu wengi wanajiuliza. Baadhi wanafikiri kuwa kioo kwenye ukuta unaotazamana na mlango wa mbele kinawachanganya wageni wanaokutembelea njia ya kuelekea; kwa hivyo watu hawa hupendelea kutundika picha kubwa na kuweka kioo upande mwingine wa ukuta ila sio kitazamane na mlango wa mbele. Kama utapenda kuweka kioo zingatia urefu wa yeyote aliyeko ndani ya nyumba yako na pia mgeni wako.

Cheki kuona kuwa vioo vyote ndani ya nyumba yako vimetundikwa katika urefu sahihi. Kioo kitundikwe kwa jinsi ambayo kichwa cha kila mtu ndani ya nyumba kitaonekana. (Watoto wadogo wanaweza kuwa na vioo kwenye vyumba vyao vya kucheza ambavyo vimetundikwa kwa urefu sahihi kuendana na wao.) Sio afya na hujisikii vizuri ukijiangalia kwenye kioo na kuona sehemu ya kichwa chako imekatika ama kichwa chote hakionekani kabisa. Watu wengi pia wanatundika vipaneli vya vioo vilivyoko kwenye fremu moja ambapo inakuwa ngumu kujiona kivuli kilichokamilika badala yake unajiona vipande vipande. Kama vile isivyo poa kujiona sehemu ya kichwa ikiwa imekatwa vile vile haipendezi kujiona vipande vipande. Kama una fremu ya vioo vya namna hii basi itundike itazamane na dirisha ambapo italeta hisia ya kuwa kama nayo ni dirisha la ukweli.

Kioo chenye ufa au kipande maeneo ya kati kinachokosekana kitakupa hisia ya wewe kuwa na ufa au chochote unachokiona kwenye kioo hicho. Unaweza kupenda kioo cha sanaa fulani lakini kama kivuli unachokiona  hakionekani vizuri basi hicho hakifai.
Tundika mfululizo wa vioo vitatu ama vitano vyenye urefu sawa, vyembamba kufanya ukuta mfupi kuonekana mrefu. Mfululizo huu unatengeneza mtindo wa kuvutia kwa kuonyesha sehemu tu ya chumba badala ya picha nzima. Kwa mtindo huu chagua ukuta ambao haupokei mwanga wa jua wa moja kwa moja ili kuepuka chumba kung’aa sana.

Yote kwa yote nia inachukua sehemu kubwa katika kupamba kwa vioo. Fikiria kabla ya kutundika kioo. Kwa nini unakitundika hapo? Ni nini kinaenda kuakisi. Kama vikiwekwa kwa mwamko na nia, vioo vinaweza kuwa mapambo mazuri sana ya nyumba yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment