Pages

Wednesday, January 9, 2013

My article for newspaper: Nyumba yenye mpangilio


Jinsi ya kuwa na mpangilio na kuondoa mlundikano wa vitu katika nyumba yako

Unapohitaji kitu na ukakifuata mahali kinapotakiwa kiwe usipokikuta hapo unaweza kujisikia hasira, kuchanganyikiwa na hata kama ni katika uzalishaji ukapungua.  Hutakiwi kuwa mtaalamu wa mpangilio wa vitu ili kuweza kuwa na mipangilio mizuri zaidi mwaka huu. Haijalishi ni mpangilio kwenye kabati lako la nguo, chumba cha kulala, meza yako ya ofsini au hata kwenye akaunti yako ya barua pepe. Utajisikia vizuri utakapoweza kuchambua na kuweka vitu kwenye mpangilio.

Wengi wetu tunashawishiwa na vitu, matukio na watu ambao tuko karibu nao kwa hiyo inaleta mantiki kabisa kuanza kuweka mpangilio na kuondoa mlundikano kwenye chumba chako cha kulala. Ondoa vitu vyote ambavyo kwakweli havihusiki kwenye chumba hiki kwa mfano vifaa vya mazoezi, vitu vya ofisini na kadhalika. Usisahau kuondoa mlundikano mvunguni.

Weka mpangilio kwenye kabati lako la nguo.  Hatua ya kwanza ni kuondoa kila kitu. Hapo ndio utakapoweza kuona una nini. Vitu kwenye kabati lako hili vitakuwa kwenye makundi manne: vya kubaki, vya kugawa, vya kutupa (takataka) na vya kuhamishia eneo lingine yaani vile ambavyo havitakiwi kuwa kwenye kabati la nguo. Andaa maboksi na raki za viatu, na usisahau mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuwekea vitu vya kugawa. Kuwa mkweli, je ni kweli kuwa unahitaji na kupenda kila kitu? Kama nguo, kiatu ama kitupio hujakiona, hujakihitaji au hujakivaa ndani ya  mwaka mmoja basi kitupilie mbali.

Kila nguo iliyoko kwenye kabati lako la nguo jiulize maswali matatu: Je inakutosha? Ulishaivaa miezi 12 iliyopita? Ina thamani ya kuifanya iwe kwenye kabati lako la nguo? Kama majibu ni hapana basi iweke kwenye fungu la kugawa.

Endelea na mchakato huo huo kwenye nguo na viatu vya mwenzi na watoto wako. Utakapomaliza zoezi hili utajikuta una mzigo mkubwa wa vitu vya kugawa na hata taka nyingi.

Vile vile kwenye ofisi yako iwe ni ofisi ya nyumbani au ya mahali pa kazi basi kama msemo wa safari inaanza kwa hatua moja tenga saa moja ya saa yako ya kazi kwa kupitia nyaraka moja moja. Amua ni ipi ya kutupa,  ni ipi ya kumwagiza mfanyakazi wa chini yako aifanyie kazi, ni ipi ya masjala na mwisho ni ipi ya wewe kuifanyia kazi mara moja. Jiwekee utaratibu wa kumeneji nyaraka zako. Kama unadhani hailipi kutumia muda wako fulani kuweka vitu kwenye mpangilio basi wacha uone ni vipi vitu vilivyolundikana vinaweza kukuvuruga katika maisha yako ya kila siku.

Kwenye droo za kabati lako la sebuleni. Je kumejaa daftari za zamani na vitabu vya jinsi ya kuendesha biashara vya nyakati ukisoma elimu ya juu na risiti za bili zilizolipwa miaka mingi iliyopita? Au pengine droo hizo zimejaa midoli na vigari vya watoto wako ambao sasa wako kidato cha pili? Ikiwa ni hivyo basi akili ni lazima ivurugike. Vitu visivyo kwenye mpangilio na uhitaji wa wakati husika vinakunyonya nguvu taratibu. Na hata kutafuta kitu kwenye mlundikano ni mbaya zaidi.

Ingia jikoni, hali ya jiko lako ndio hali ya afya yako. Kwahiyo ihurumie afya yako kwa kusafisha na kuweka mpangilio kwenye jiko lako! Safisha kwenye jokofu, punguza viporo vilivyoshamiri huko. Safisha jiko lenyewe, masufuria na vikaangio. Safisha kwenye madroo yote na ondoa chupa zote zisizohitajika.

Kama kawaida mlango wa mbele ni kivutio cha nyumba na ni eneo unaloanzia kupata nguvu unapoingia nyumbani. Zipe fahamu zako unafuu kwa kuweka mazingira ya mlango wa mbele kwenye mpangilio ili kuondoa msongo wa mawazo. Ondoa vitu kwenye mlango huo ambavyo kwakweli havitakiwi pale kwa mfano doo la uchafu, vyungu vya maua vyenye nyufa na kadhalika. Lete muonekano wa umaridadi kwenye eneo hili la mbele ya nyumba.

Tafuta njia ya kushughulika na barua na bili zinazokuja nyumbani ili zisisambae kila mahali. Droo dogo kwenye kabati lako la nguo linaweza kuwa suluhisho la kuhifadhi barua zako kama hamna nafasi eneo lingine.

Sababu ya watu wengi kutopenda kuweka vitu katika mpangilio na kuondoa vile visivyotumika sio ni kwa vile inahitaji nguvu na muda. Sababu ya ukweli ni kuwa mchakato mzima una hisia kama vile ni tiba, na ni zoezi linalohitaji stamina. Ila habari njema ni kuwa mara ufanyapo zoezi hili na kuweka mkakati na miundombinu ya kuwezesha vitu kutolundikana tena basi maisha yanakuwa rahisi kwako kwani utazungukwa na mazingira freshi na safi.

Zingatia kuweka mpangilio, kuondoa mlundikano ili kufanya maeneo mbalimbali ya nyumbani kama yalivyoainishwa hapo juu kuwa nadhifu kwa kuwa yameunganika na ustawi wako hapo nyumbani. Watafiti wa kisayansi  walishagundua kitambo kuwa mlundikano wa vitu humsababishia binadamu kutozingatia mambo na pia kuwa na uwezo mdogo wa kuchanganua mambo.

Makala hii imeandikwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

No comments:

Post a Comment