Pages

Thursday, February 21, 2013

My article for newspaper: Vizulia na mito


Mito na vizulia kama vitupio vya sebule ya kisasa
Pamba na pendezesha sebule yako kwa kuwa ni chumba unachoweza kupumzika zaidi ukiwa nyumbani kwako.  Hii inaweza kubadilisha mahali hapo kutoka kuwa sehemu ya kawaida ya kirafiki ya kupiga umbea hadi kwenye sehemu ya kisasa zaidi yenye muonekano wa kianasa na kutoa tamko la ladha yako. Makala hii itakujuza baadhi ya mapambo na vitupio vya kisasa vya sebule unavyoweza kupambia sebule yako:

Mito ni kitupio muhimu kwa mapambo ya sebuleni  na inaweza kuchangamsha rangi kwa sofa zenye rangi za kupooza.  Pia inaongeza faraja na huwa sofa nyingi zinakuja na mto mmoja au miwili lakini unaweza kuongezea ikawa mingi kwa kadri unavyotaka. Mito inapendezesha na unaweza kubadili ya rangi tofauti tofauti kubadili muonekano na anga ya sebule.  Unaweza kuwa na mito ya sofa kwa matukio maalum kama siku ya kuzaliwa na krismasi.

Zaidi ya kuwa mapambo mito ya sofa hutumika pia kwa ajili ya usingizi wa mchana wakati ambapo unahitaji mmoja kulala chini kwa dakika chache. Weka mto mgongoni uuegemee kama hupendi nafasi ya kiti ulichokalia. Mtoto mdogo anaweza kukalia mto wa sofa kumsaidia akae mezani. Ukiwa umemkasirikia mtu unaweza kumrushia mto wa sofa bila kusababisha uharibifu mkubwa.
Mito ya kwenye sofa inaweza kuwa laini au ya kutekenya. Unaweza kuipata kwenye vitambaa vya kung’aa au  vilivyofubaa. Mito ya pamba ni mizuri kuliko yote na unaweza kuiosha pale inapochafuka. Mito ya hariri inaweza kuwa mizuri na kuleta ufahari lakini mara nyingi ni ghali.

Vizulia vidogo vidogo vya kutupia maeneo kadhaa sebuleni vinaweza kutumika kufunika maeneo mabovu ya zulia kuu au sakafu na pia kuonyesha eneo maalum la kukaa ndani ya sebule. Vizulia hivi hupendeza sana hasa kama sebule ni kubwa na pia kuvitupia kwenye njia za kuingilia. Vizulia vya kutupia vina faida kubwa zaidi ya kufunika sakafu tu. Wakati wa kununua angalia mambo kama rangi, urahisi wa kuondoa madoa na saizi. Chagua saizi ambayo sio kubwa sana au ndogo sana kwa sebule husika. Vile vyembamba virefu ni kwa ajili ya maeneo ya ujia. Kama unanunua kizulia cha kutupia kwa ajili ya chumba kikubwa, ni wazo jema.

Vizulia hivi vipo vya pembe nne na vya duara. Kuchagua kizulia sahihi kwa eneo fulani inawezekana kuwa rahisi kabisa kwa kuzingatia maswali yafuatayo:
Kizulia husika kinatakiwa kiwe cha ukubwa gani? Ni staili ipi itafaa zaidi kutimiza malengo ya kuweka kizulia hicho hapo mahali, je ni staili ya pembe nne au duara?  Ni michoro na rangi zipi zitafaa zaidi? Ni kwa ajili gani unahitaji kizulia husika? Pima ukubwa wa mahali kabla hujafanya manunuzi.

Vizulia vya kutupia maeneo vinaweza kukugharimu hela nyingi kwa hiyo ni muhimu kuvitunza kuhakikisha maisha marefu.. Nyonya mchanga na vumbi mara kwa mara maeneo yanayokanyag wa mara kwa mara, na usisahau kunyonya mchanga na vumbi  mara chache maeneo  yanayokanyagwa mara chache. Safisha madoa mara yatokeapo badala ya kuyaacha kwa muda mrefu kwani yatakomaa. Kama una vizulia vikubwa na huenda ulinunua kwa gharama kubwa utahitajika kupeleka kwa wataalamu wa kufua mazulia mara kadha wa kadha. Kumbuka kugeuza chini ya kizulia kuona kama kuna mchwa au mende wanaoharibu.

Kupaka kuta za sebule yako rangi nyeupe kunakupa nafasi nzuri ya kuwa mbunifu wakati wa kununua fenicha na mapambo mengine. Weka  taa za aina mbalimbali sebuleni, za kusomea, za kutia msisitizo eneo la burudani,  za kila siku za kuwasha wakati wa familia kukutana  na taa za disko wakati wa pati.

Eneo la vyomba vya habari nayo inashika kasi kwa sebule za kisasa.Kwa hivyo mapambo na mtindo wa eneo hilo nao unapewa kipaumbele. Eneo hili ukuta wake huwa unapakwa rangi ya kukolea wakati maeneo mengine yanapakwa rangi hafifu. Eneo la vyombo vya habari huwa pia na shelfu za vitabu na DVD.

Samani na pazia pia vinaongeza rangi, staili na mapambo ya sebule. Kama utatumia vitupio vya sebuleni kwa njia sahihi, utafanya  muonekano wa sebule wa kuvutia. Lakini hakikisha kuwa huzidishi vitupio. Changamoto moja ya mito ya sofa  ni kuipanga kila baada ya unaponyanyuka kwenye kochi na kama utakuwa na mingi inaweka ikapoka chumba kwa hivyo kukifanya kionekane kurundikana. Faidi rangi ya vizulia vya kutupia kwa kuzioanisha vyema na mapamba yako mengine. Kama una sebule kubwa kumbuka kutupia tanki la samaki ili kuongeza uhai kwenye vitupio vyako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment