Pages

Thursday, March 7, 2013

My article for newspaper: Feni ya Stovu


Umuhimu wa feni ya stovu

Jiko ni kitovu cha nyumba ya kisasa. Jinsi nyumba inavyozidi  kuwa za kisasa, ndivyo inavyokuwa na jiko lenye vifaa na muonekano wa kisasa pia. Katika makala hii jiko litamaanisha chumba chenyewe na stovu itamaanisha pale panapobandikwa sufuria. Ili kufanikisha uingizaji wa hewa jikoni nyumba za kisasa zina vifaa vya jiko vya kisasa. Mojawapo ya vifaa hivi ni feni ya stovu.

Feni ya stovu ni kifaa kinachofungwa juu ya stovu kwa ajili ya kukusanya moshi, harufu, mvuke na ghasia nyingine zizalishwazo hewani wakati wa kupika. Kwa ufanyaji kazi wa kuridhisha feni ya stovu inatakiwa kuwa na upana sawa na wa stovu yenyewe. Kuna feni ambazo zinanyonya moshi na mvuke na kutoa nje ya nyumba na kuna ambazo zimetengenezwa kwa jinsi ambayo moshi na harufu zinanyonywa ndani kwa ndani hata kama mfumo wa kutoa nje ya nyumba haupo. Kwa hiyo usijali kuwa jiko lako halina mfumo wa kukuwezesha kutoa uchafu huo wa mapishi nje ya nyumba, bado unaweza kufunga feni hii aina ya pili yaani ya kuvuta uchafu ndani kwa ndani.

Ndio, nyumba yako inaweza kuwa na harufu za mapishi ambazo hazikukoseshi faraja lakini ni ukweli kuwa harufu hizo sio nzuri kwa afya yako. Wakati unapopika, mvuke, gesi na moshi zinaachiliwa hewani kama uchafu na kwenda kutulia kwenye fenicha, makabati, nyavu za jiko na hata ukutani. Uchafu huu unaharibu samani za nyumba yako na pia hewa ya jikoni.
Inawezekana jiko la bibi yako lilikuwa kwa jinsi ambayo uingizaji wa hewa ulikuwa rahisi, lakini kwa nyumba za kisasa zenye jiko humo humo uingiaji wa hewa jikoni unaweza kuwa wa taabu. Kwa maana hiyo ni vyema kufunga feni ya stovu ili kuwezesha hewa safi ndani ya nyumba.  Kwa jinsi ambavyo nyumba zetu zinakuwa kubwa, jiko linakuwa ndio sehemu ya kuwezesha starehe ndani ya  nyumba kuanzia kuandaa chakula cha wageni jumapili na vyakula vingine vyote vya familia. Jifunze njia sahihi za kuwezesha uwepo wa hewa safi ndani ya jiko lako mara zote.

Hewa safi jikoni wakati wa kupika ni usafi, na ni afya kwa wakaaji na hufanya  mazingira na harufu safi ya nyumba kwa ujumla. Wakati wa kupika kwa gesi, hewa ukaaa inazalishwa hewani kama uchafu kutokana na kuungua kwa hiyo gesi ya kupikia. Hewa hii inaweza kusababisha matatizo kadhaa kama maumivu ya kichwa na hata kifo. Kwa hivyo leo hii kuna njia nyingi za uwekaji wa hewa safi ndani ya jiko na mojawapo ni hii ya kufunga feni ya stovu. Ukienda kwenye maduka ya vifaa vya umeme ukaulizia feni ya stovu huenda usieleweke kirahisi. Jina ambalo limezoeleka na ni maarufu kwa wauzaji wa vifaa hivyo ni “hood” na huwa zipo za ukubwa mbalimabali kuendana na ukubwa wa stovu yako. Kama nilivyosema awali feni hizi zipo ambazo uwekaji wake unatakiwa uwe ulikuwa kwenye mpango wa ujenzi wa jiko ambapo hizi ni zile zenye bomba maalumu la kutoa moshi na harufu nje ya nyumba, na zipo zile ambazo harufu mvuke na moshi hunyonywa ndani kwa ndani  na chujio maalumu zilizojengewa kwenye feni hiyo kwa hivyo hata kama mpango wa jiko haukuweka mfumo wa feni ya stovu bado utaweza kuifunga feni yako.

Feni ya stovu inafungwa kwa jinsi ambayo gesi, mvuke, moshi na mafuta vinavyotoka kwenye hiyo hewa ya moto wakati wa kupika zinadakwa na feni hiyo. Upana wa feni unavyozidi upana wa jiko ndivyo uchafu mwingi unavyodakwa. Moja ya nyanja muhimu sana kwenye kuwa na hewa safi ndani ya nyumba ni kwa kudhibiti kiasi cha unyevu. Kwa kuwa ni unyevu mwingi unaotokana na mapishi ni vyema kukumbuka kuwasha feni yako kila unapopika. Mfumo wa uingizaji hewa kwenye nyumba yako kwa jinsi ulivyowekwa  wakati wa ujenzi kwa maana ya madiridha na kadhalika unaweza kudhibiti kiasi fulani cha unyevu, lakini kama huna feni ya stovu utaanza kusikia kiwango cha hewa safi ndani ya nyumba kikishuka wakati wa kupika. Unyevu ukiruhusiwa kujijenga unazalisha vumbi, ukurutu wa mafuta, uozo na hata fangasi ambavyo huweza kusababisha maradhi ya ngozi, macho na hata matatizo kwenye mfumo wa kupumua wa binadamu.

Ingawa kufungua madirisha inaweza kusaidia kuondoa moshi na harufu kwa kiwango fulani, bado haitoshi kutoa uchafu wote uzalishwao hewani wakati wa kupika na kuleta hewa safi jikoni.
Ili kufanya kazi vyema mfumo wako wa uingizaji hewa jikoni inabidi uwe unasafishwa mara kwa mara. Chujio za feni zisafishwe kila baada ya miezi mitatu na mfumo mzima usafishwe mara moja kwa mwaka.

Karibia hood zote zina taa, kwa hivyo hii inasaidia pia kuongeza mwanga kwenye sufuria yako wakati wa kupika na kuwezesha kuona chakula kilicho chini ya feni. Fanya mazingira na hewa ya ndani ya jiko na nyumba yako kwa ujumla yawe safi kwa kuweka feni ya stovu leo!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755200023

No comments:

Post a Comment