Pages

Wednesday, May 29, 2013

My article for newspaper: pamba kwa mimea ya ndani



Ongeza uasili ndani ya nyumba kwa kupamba na mimea

Kama unataka kupamba nyumba yako kwa njia ya asili na kuleta hewa safi ndani hakuna chaguo zuri zaidi ya mimea ya ndani ya nyumba. Mimea ya ndani ni zana ya mapambo ambayo huongeza uzuri wa rangi ya kijani kwa kiasi cha kutosha na kuboresha hali ya hewa ndani ya chumba. Unaweza ukaiweka kwenye kona tupu, kwenye madirisha, shelfu au kama pambo la kati. Kitu kizuri juu ya mimea ya ndani ni kuwa inaweza kukua vizuri eneo lolote, liwe dogo au kubwa pamoja na hali ya hewa ya ndani na mwanga utakaoweza kupatikana. Kuna aina mbalimbali za mimea ya ndani kwa wauzaji wa maua ya asili ambayo inakidhi kila hitaji.

Hata hivyo ni wachache wanaoweza kukabiliana na changamoto na utunzaji wa mimea ya ndani. Kazi kama kuyamwagilia kila siku,  kuweka mbolea, kuondoa majani makavu na kupruni ni mambo kadhaa yanayoweza kumkatisha mwenye nyumba tamaa. Bado kiukweli mimea ya ndani sio ngumu kivile kuitunza.

Unatakiwa kuchagua chumba ambacho umeamua kupamba kwa mimea ya ndani. Mimea hii inaonekana maridadi kwenye sehemu yoyote ya nyumba. Unaweza ukaipambia jikoni, bafuni, sehemu ya kuingilia au sebuleni. Unatakiwa kuchagua sehemu nzuri ya kuweka huo mmea katika chumba husika. Epuka kuweka mmea karibia na moto au karibia na bomba la kuchemshia maji. Hakikisha kuwa sehemu uliyochagua inapokea mwanga wa jua wa kutosha kwa ajili ya afya ya mchakato wa usanisinuru (hii ni njia ya mimea ya kujitengenezea chakula kwa kutumiamwanga wa jua).

Unatakiwa kuchagua aina ya mimea ya ndani unayotaka kuweka.  Mimea na maua yanayofaa kuwekwa ndani ya nyumba ipo ya aina nyingi kwenye bustani za wauza maua. Mimea maarufu ya ndani ni ya jamii ya aloe vera, bambuu, kaktasi na magimbi. Wakati wakununua uliza mahitaji ya mmea husika kwa mfano kiasi cha jua, joto na maji kinachohitajika ili mmea ustawi vizuri. Nunua tu ile ambayo unaona utaweza kuitunza. Kumbuka walau mara moja kwa wiki zungusha chungu cha mmea kuwezesha mmea kukua kwa uwiano.

Mimea ya ndani inatakiwa kuwekwa kwenye vyungu vya mapambo kuendana na mapambo mengine yaliyopo hapo mahali. Vinaweza kuwa vyungu vya kauri vilivyochorwa kwa mikono au vyungu vya kisasa vya rangi ya silva inayong’aa pia vyungu vya kioo vinaonekana maridadi sana kwa maeneo ya sebuleni na chumba cha kulia chakula.

Kwa ujumla utunzaji wa mimea ya ndani  unahitaji muda na nguvu kidogo ingawa kuna matatizo yanayoweza kutokea na kuleta usumbufu mkubwa. Mojawapo  na kubwa la  matatizo haya ni ukungu ambao unaweza kujijenga kwenye udongo au majani ya mimea yako ya ndani. Ukungu ni jambo linaloweza kuleta uharibifu kwako na kwa mimea yako. Ikiwa basi tatizo la ukungu limejitokeza chukua kitambaa kilicholoa ushike jani kwa chini (ili kuliongezea nguvu  lisivunjike) na lifute, hii itaondoa ukungu wote unaoonekana. Usije ukajaribu kufuta na kitambaa kikavu kwani utaharibu sehemu ya juu  ya jani. Wakati majani yote yakiwa yameshafutwa, ruhusu mmea kukauka kwa kuuweka eneo ambalo linaingiza hewa.

Kama ukungu umeota kwenye udongo wa chungu basi ondoa eneo la juu na uweke udongo mwingine. Hata hivyo kama udongo utakuwa umevamiwa kwa kiasi kikubwa basi inashauriwa kuondoa udongo wote na kujaza chungu upya. Ongezea na dawa ya kuzuia fangasi kwenye udongo wa mimea yako ya ndani.

Hakikisha maji kwenye chungu yanatembea. Njia kuu ya ukungu kujijenga ni udongo kuwa na maji maji kwa kipindi kirefu. Kila chungu cha mimea ya ndani kiwe na ukanda wa kokoto ndogo chini ili kuruhusu mchanganyiko ulioko ndani ya chungu kukauka vyema. Hii inafanya mimea yako iwe na afya na kupunguza uwezekano wa ukungu kujijenga. Pia weka mmea wako wa ndani eneo ambalo linaingiza hewa kwa vile ukungu unashamiri eneo ambalo hewa ni hafifu.

Safisha mimea yako ya ndani mara kwa mara. Vumbi linajijenga kwenye majani ya mimea ya ndani kama linavojijenga kwenye  maeneo mengine ndani ya nyumba. Hili vumbi linafanya uchafu mwingine ujijenge juu ya majani na mmea kushindwa kufanya vyema usanisinuru hivyo kudhoofu. Kufuta majani mara kwa mara na kitambaa kilicholoa inasaidia kuondoa vumbi kujijenga kwa hivyo kuondoa uwezekano wa ukungu. Ondoa majani yaliyokufa mapema iwezekanavyo.

Mimea ya ndani inaweza kuwa na faida kubwa katika nyumba zetu na maisha yetu. Inaweza kuchuja hewa ndani ya nyumba na kufanya mazingira yenye afya. Hata hivyo ni vyema kuwa makini kwakuwa kuna mimea ambayo ni sumu kwa wanyama wa ndani kama vile paka na kadhalika na pia kwa watoto wadogo. Fanya utafiti wako vizuri na uone ni wapi pa kupamba na asili ndani ya nyumba yako. Chunguza mimea mbalimbali ambayo unaweza kupamba maeneo hayo na uone kama utunzaji wake utaendana na maisha unayoishi. Kama ukikwama pata ushauri kwa wataalamu wa mambo ya bustani na mimea. Wataalamu hawa watakusaidia kupata na kukuhakikishia mimea ya ndani  itakayokufaa.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

Thursday, May 23, 2013

My article for newspaper: meza ya kahawa


Jinsi ya kupamba meza ya kahawa


Meza ya kahawa inaweka sebule pamoja na ikiwa imepambwa vyema inahuisha muonekano mzima wa chumba. Meza ya kahawa ni meza  isiyo refu ambayo imebuniwa kuwekwa mbele ya sofa, kuegemesha vinywaji ( na ndipo jina lilipotokea) majarida, vitabu na vitu vingine vidogodogo vya kutumia wakati mtu amekaa sebuleni kama vile kosta za kuwekea vinywaji na hata wakati mwingine hutumika kuwekea miguu. Meza ya kahawa ni kitovu cha sebule nyingi na zipo za maumbo mbalimbali kama vile duara, yai au pembe nne na nyingi ni za mbao na chache za kioo pia zipo chache sana  za chuma. Meza hizi pia zinaweza kuwa na sehemu ya kuhifadhia kwa chini.  Cha msingi ni kutumia hii sehemu tambarare ya meza kuonyesha mapambo ya chumba chako bila kutupia kila kiwezekanacho juu yake.
Kwa kuwa meza ya kahawa ina matumizi mengi, mara nyingi ni ngumu kujua ni kwa vipi uipambe. Je umeshajiuliza, ufanye nini na hii sehemu  tupu ya meza ya kahawa? Wakati mwingine ni vyema kuipamba isivyo rasmi sana ili kuleta hisia za burudani na starehe ili hata kuweza kunyanyua mguu wako na kuutuliza hapo na kusoma gazeti wakati ukifurahia kinywaji chako. Au labda ni wakati wa kula chakula hivyo kutakiwa kukaa meza ya chakula lakini kuna kipindi cha luninga ukipendacho kwa wakati huohuo, basi unageuza meza ya kahawa kuwa ya chakula. Ukifikiria kwa uhalisia, kwa muonekano usio rasmi mapambo ya meza ya kahawa yanawezesha wanafamilia kuitumia kwenye kukutana kupumzika, kucheza michezo, kusoma vitabu na kuangalia luninga wakati huohuo wakiburudika na vinywaji. Meza hii inakusanya pamoja faraja na furaha ya familia. Bila hii meza ya inchi 60 kwa 30, ni wapi ungeweka vivywaji vyako, karatasi, vitabu, majarida na kadhalika…je ni sakafuni?

Hata hivyo kwa sebule zilizo rasmi meza ya kahawa iliyo juu ya zulia jeupe na yenye mapambo ya thamani yanayong’aa ni ya kushangaa tu kwa jicho, haiguswi hadi pale tu anapotembelea mgeni wa heshima! Lakini ijulikane kuwa kwa sebule zisizo rasmi meza ya kahawa iliyowekwa kwa jinsi ambayo kati ya sofa na meza kuna nafasi ya kutosha kwa miguu kuwa huru shughuli zinapoisha meza husafishwa, hupangwa vizuri na kuachwa maridadi ikisubiri shughuli nyingine kwa mgeni mwingine au kwa makutano mengine ya familia.

Wakati wa kupamba meza yako ya kahawa zingatia nafasi iliyopo, jinsi watu wanavyopita kukalia sofa. Hutapenda kuvunja mapambo yako ya thamani kutokana na msongamano. Hakikisha kuna uwiano kati ya pambo na meza, kwa mfano usiweke vesi kubwa ya maua  yenye matawi kama zile za kuweka sakafuni kwenye kona ya chumba kwenye meza ya kahawa. Kwa ajili sebuleni ni sehemu ambayo mazungumzo yanaendelea hutapenda kuona mgeni wako aliyekaa sofa ya upande mmoja akivunjika shingo kujaribu kumuangalia mgeni aliyekaa sofa ya upande wa pili kutokana na kuzuiwa na ukubwa wa maua yaliyoko mezani.

Jua eneo sahihi la kuweka meza yako ya kahawa na mpangilio wa mapambo yake kutokana na matumizi ya meza yenyewe. Kama nilivyoandika kwenye makala iliyopita ya muonekano wa sebule ya kuwa kuna sebule ambazo zinatumiwa na wanafamilia na wageni kwa pamoja (sebule zisizo rasmi) na kuna zile ambazo ni chumba rasmi kinachotumika kukiwa na mgeni tu; hivyo basi kama meza ya kahawa ipo kwenye sebule isiyo rasmi wakati wa kuipamba zingatia kuwa itakuwa inavurugwa na kuwagikiwa vinywaji mara kwa mara. Ni wengi wenu mmesikia waume zenu na watoto wakilalamika  “hivi hiki kimeza kinatakiwa kuwa hapa kweli?” Usiweke mapambo ya kuvunjika kirahisi hapa, yahifadhi kwa eneo lingine.   Tumia mapambo ambayo hayawezi kuharibiwa kirahisi kwa mfano kwenye meza ya sebule isiyo rasmi usiweke vesi za maua zenye maji pamoja na vitabu pamoja.
Kwenye kupamba meza ya kahawa ni muhimu kuzingatia mapambo mengine yaliyoko hapo sebuleni. Iwapo utaamua kupamba meza yako ya kahawa kwa vimapambo vidogo vidogo vingi basi ni vyema ukaviweka kwenye sinia la mapambo au kuvitandaza kwenye kitambaa cha kati cha meza ya kahawa ili meza isionekane kama bahari ya vikorokoro. Kwa mfano kama ukiweka kwenye sinia la mapambo basi wakati kuna shughuli wahusika wanaweza kusogeza sinia pembeni na meza kutumika kwa shughuli.

Wakati wa kutafuta mapambo ya meza yako ya kahawa, hakikisha unatafuta pambo la kati ambalo ni alama yako ama kitu unachopendelea, au labda ulilinunua ulipotembelea mahali fulani kwa hivyo litakuwa linakupa ukumbusho fulani. Utahitaji pambo kubwa la kumiliki meza ambalo la
linaweza kuwa vesi ya maua, mshumaa au kinyago au kitu chochote tu ambacho kitavuta jicho.
Furahia kupamba meza yako ya kahawa kwani ni njia mojawapo nzuri ya kubadili muonekano wa sebule bila ya kutumia gharama kubwa au wataalamu. Iwe ni kwa kuweka pambo moja kubwa au mengi madogodogo mkakati wako ni kupata mlingano na uwiano ndani ya chumba.

Mwisho ila muhimu zaidi, kabla hujapamba meza yako ya kahawa, ni muhimu kuchagua staili ya meza ambayo itaendana na mahitaji na maisha unayoishi. Fikiria kuhusu kazi zake na itatumikaje. Je ni ya kwenye sebule iliyo rasmi au ni sebule ya familia nzima pamoja  ambapo watoto wanakaa na kufanya kazi zao za shule au mume wako atawekea miguu wakati akitazama ITV?  Kufahamu matumizi na mahitaji ya meza yako ya kahawa itakupa mwelekeo sahihi wa ni mapambo gani ya kununua na jinsi ya kuyapambia!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

Thursday, May 16, 2013

My article for newspaper: mpangilio kabati za jikoni


Jinsi ya kuwa na mpangilio ndani ya kabati za jikoni

Iwe ni jiko la kwenye nyumba unayohamia au la siku zote ikiwa mambo jikoni hayaendi kirahisi kama inavyotakiwa, kuweka mpangilio kwenye jiko lako kutarahisisha mambo na vilevile kulifanya lionekane safi.

Kuweka vitu katika mpangilo ndani ya kabati za jikoni kutaleta hisia mpya kwa chumba hiki ambacho kinatumika zaidi nyumbani. Kabati za jikoni zenye mpangilio zitakusaidia kupata vifaa kirahisi na pia kukuzuia usinunue vitu mara mbili mbili ambavyo tayari unavyo.

Kutokana na jikoni kuwa na vifaa vya aina mbalimbali ambavyo vinatakiwa kuwa kwenye kabati basi inamuwia ngumu mhusika kuweka mpangilio mzuri na ndio maana ni vyema kuwa na mkakati rahisi wa kupanga ambao ni kuweka vifaa vinavyoendana pamoja.

Tosa kifaa chochote ambacho hukitumii. Mpe rafiki, ndugu au gawa kwenye vituo vya kutoa misaada kwa jamii. Kuwa mkweli kwa nafsi yako! Je ni lini mara ya mwisho kutumia hicho kimashine cha kusaga nyama au hiyo chupa kubwa ya chai ya kutumika labda kwenye chumba cha mkutano wa watu 20 uliyopewa zawadi wakati fulani. Kama ni nyumba yenye familia changa labda chupa hii ulipewa zawadi kwenye harusi yako. Vifaa vya kutengenezea juisi kama vile blenda je ni kweli unahitaji kuwa na mbili? Je kuna jinsi rahisi ya kufanya kazi fulani ama kupata hitaji fulani bila ya wewe kulitengeneza mwenyewe. Kwa mfano ni jitihada kubwa utatumia kusaga nyama mwenyewe badala yake kwa nini usinunue nyama iliyosagwa tayari? Kama utapunguza vifaa kama hivi kwenye kabati zako ya jikoni basi utajipatia nafasi kubwa zaidi ya kuweka vitu vingine ambavyo unavihitaji zaidi.

Kwa hivyo kabla hujaanza kupanga upya kwenye kabati zako ya jikoni au kununua vifaa mbalimbali vya kuhifadhia, unatakiwa kuwa makini sana kwa kuondoa mrundikano wote kwanza. Unavyoweza kutupa au kugawa vitu vingi zaidi ndivyo utakavyokuwa na vitu vichache ambavyo kweli unavihitaji na ukaweza kuvipanga na kuvihifadhi.

Baada ya kuondoa mrundikano ni wakati sasa wa kupangilia vinavyotakikana kuwepo kwenye kabati za jikoni kwa jinsi ambayo italeta maana unavyopika na muonekano wa jiko lako kwa ujumla. Kimsingi kuweka mpangilio kwenye kabati za jikoni inamaanisha kupanga vyakula vyako, vifaa, sufuria na vikaangio na zana nyingine za jikoni kwa njia ambayo inakurahisishia maisha wewe na familia yako. Usidanganyike na mionekano; hakuna wewe bila wewe. Jambo la muhimu la kuzingatia ni kuwa panga kwa jinsi ambayo kila kitu unachokitumia mara kwa mara unaweza kukifikia kirahisi zaidi iwezekanavyo. Jagi la vijiko na miiko karibia na stovu linasaidia kuweka vifaa vya kupikia karibu.

Rekebisha vitu ambavyo havifanyi kazi. Kama mkono wa sufuria umevunjika; vitu vya aina hii vinaleta mrundikano kwa hivyo rekebisha au ondoa ununue nyingine. Kama huwezi kununua nyingine kwa wakati husika basi weka kwenye orodha ya mahitaji yako kwa siku za mbeleni.
Hifadhi vifaa vinavyotumika mara kwa mara maeneo ambayo yanafikika kirahisi. Angalia ni kifaa gani unatumia zaidi. Vifaa ambavyo hutumii mara kwa mara kama vile tuseme kikaangio ambacho unatumia mwishoni mwa wiki tu au wakati wa likizo vinaweza kuwekwa juu kabisa ya mashelfu au mwisho kabisa ndani ya kabati. Vinaweza hata kuhifadhiwa stoo badala ya kwenye kabati za jikoni.

Hakikisha kila kifaa kwenye kabati zako ya jikoni yana haki ya kuchukua nafasi yako hiyo ya thamani! Vifaa vyote usivyotumia mara kwa mara viwekwe mbali bila kujali thamani ya kifaa, kama unatengeneza keki mara moja ndani ya miezi sita basi bakuli la kuchanganyia na vifaa vyote vya kutengeneza keki vihifadhi stoo.

Tazama kwa umakini vifaa ambavyo ni vya kudumu juu ya kaunta. Kaunta inatakiwa kusafishwa mara kwa mara kwa vile ni eneo lako la msingi la kufanyia kazi. Weka kwenye kabati vifaa vingine ambavyo kwa kweli havina ulazima wa kukaa kaunta.

Kupangilia vifaa kwenye kabati kuendane na kusafisha. Ukishasafisha droo moja au shelfu, tandika zile karatasi za kwenye kabati la vyombo kabla hujaanza kupanga vitu. Kusafisha na kupanga kwa wakati mmoja kunarahisisha kazi. Tumia kabati za chini kwa vifaa vizito na zile za juu kwa vifaa vyepesi kama glasi za mvinyo na vitu ambavyo unatumia mara kwa mara na unataka ukinyoosha mkono tu unabeba. Mfano ni chumvi na viungo vya kusaga vya vyakula.

Chagua kontena zitakazoendana na mahitaji ya chakula kinachohifadhiwa humo. Kontena zenye mifuniko ni sahihi  kuzuia chakula kisimwagike wakati zile zinazozuia hewa isipite ni sahihi zaidi kwani zinafavya chakula kikae muda mrefu bila kuharibika. Chagua kontena za ukubwa wa kutosha za kuweka vyakula ndani ya kabati. Vyakula hivi ni kama sukari, unga, mchele na kadhalika. Kontena ndogo ndogo zinafaa kwa ajili ya viungo vya kusaga vya vyakula. Kontena za kuhifadhia vyakula kwenye kabati ya jikoni zikiwekwa majina ni bora zaidi kwani mpishi ataweza kutofautisha kirahisi kati ya kontena la unga wa ngano na la unga wa mahindi.

Mara kwa mara kagua uwezekano wa kuwepo kwa mende na wadudu wengine kwenye kabati za jikoni kwani wadudu hawa wanaweza kuharibu vyakula vyako. Unaweza kuweka vidonge vya kuua mende kabatini au unga wa kuua wadudu au hata ukaamua kupuliza dawa mara moja kila baada ya miezi sita.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

Thursday, May 9, 2013

My article for newspaper: Mawe ya kukanyagia



Kutengeneza njia kwenye bustani kwa kuweka mawe ya kukanyagia

Kwa mandhari ya kuvutia na kukidhi mahitaji ya nje ya nyumba wenye nyumba wengi wanasahau kuweka njia  kwenye bustani. Wengi wanaelekeza nguvu zao kwenye kuweka mandhari ya varanda ivutie ,  kuchagua maua ya bustani, kuweka vitofali vya chini vya kuzuia tope na wachache wenye uwezo wa kuweka mabwawa ya kuogelea hufanya hivyo na kusahau njia ya kwenye bustani  ambayo huunganisha maeneo mengine ya nje ya nyumba na bustani.

Sio tu kuwa njia ya kwenye bustani inamwongoza mtu kujionea uzuri wa bustani bali pia njia hii huleta mhemko. Jinsi ya haraka, rahisi na gharama nafuu ya kutengeneza njia kwenye bustani ni kwa kuweka mawe ya kukanyagia. Mawe haya chimbuko lake ni sherehe za chai za kwenye bustani ambapo mawe ya kukanyagia yaliwekwa ili kuzuia viatu vya wageni visinase kwenye udongo laini wa bustani. Kwa jinsi hii mawe ya kukanyagia yalisaidia kuhifadhi majani na kumwelekeza mgeni eneo mahsusi.

Mawe ya kukanyagia ya kwenye bustani leo hii yanaweza kuwa na lengo lile lile la kutengeneza njia  lakini pia yanaweza kuwa kama mapambo hasa pale yanapokuwa na maumbo na rangi mbalimbali na pia muundo wa njia yenyewe ama kuwekewa taa za kumwongoza mpitaji nyakati za usiku.

Imeonekana mawe ya kikanyagia ni njia rahisi na ya haraka kutengeneza njia kwenye bustani kwa kuwa mawe haya yanawekwa kwa kuchimba kidogo sana na huwa kuna nafasi kati ya jiwa na jiwe kwa hivyo haihitajiki kutafuta tambarare. Na pia yanafunga eneo kubwa kwa mawe machache.  Hauwi na wasiwasi na msingi wake kama vile ambavyo unajali msingi kwenye kujenga ukuta ama sakafu ya nyumba. Mawe ya kukanyagia hayahusiki katika kanuni ya msingi imara. Mara nyingi mawe haya hayawekwi kutengeneza njia ulioonyooka kwani kwa historia ya njia ya bustani nia ni kumwezesha mpitaji kuitazama na kuifurahia bustani kwa ukaribu zaidi maeneo mbalimbali.  Njia za kutembea kwenye bustani zina jinsi ya kupunguza mwendo na kufurahia uasili ya bustani.

Mawe ya kukanyagia kwenye bustani yafaa yatengenzwe kwa zege au kama ni mawe ya asili kama yale ya tanga pia yanafaa.  Yawe flati na kwa ukubwa wa mtu kutembea kwa uhuru na unene wake uwe wa inchi mbili. Umbali kati ya jiwe na jiwe uzingatie pia hatua za watoto wadogo kwa hivyo yasiwekwe mbalimbali sana.
Mawe ya kukanyagia ya kwenye bustani yanakuwa kwenye maumbo mbalimbali kwa mfano pembe nne, pembe sita, duara au hata bila ya umbo maalum ni kwa kadri ya ubunifu wako tu wakati wa kuyatengeneza. Weka mawe haya yatokeze juu ya ardhi kiasi cha inchi moja. Hii itasaidia kuwa na sehemu kavu ya kukanyaga na bado ukaweza kupitisha mashine wakati wa kukata majani.

Kwa usalama, eneo la kuwekea mguu lisiwe laini kwa jinsi ambayo mtembeaji anaweza kuteleza kwa mfano nyakati za mvua mawe yakiwa yameloa. Wewe na mtu wako wa bustani mnayaweka mawe kwa uangalifu kwa kuzingatia, umbo la mawe na saizi na mnaweza kutengeneza njia ya kuvutia mno kutokana na maumbo na rangi za mawe yenyewe.

Leo hii mawe ya kukanyagia kwenye bustani ni kwa matumizi na mapambo na sio kama mawe yanayowekwa kwenye madimbwi kukuwezesha kuruka tope ili kufanya miguu yako isilowe na kuchafuka. Mawe ya kwenye bustani yanakuruhusu kutembea kwenye bustani bila kuloa umande au kukanyaga  matope. Yanaweza kuongeza rangi na maumbo mapya kwenye bustani kwa nia ya mapambo. Mawe haya ni rahisi kutengeneza na kuweka, unaweza kufanya mradi wa kuyatengeneza na kuyaweka kwenye bustani mwenyewe ukiwa na msaidizi mmoja tu. Njia za kwenye bustani zinasaidia kupunguza kasi ya mwendo kwa hivyo kufurahia uasili wa mandhari ya bustani.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023