Pages

Thursday, May 9, 2013

My article for newspaper: Mawe ya kukanyagia



Kutengeneza njia kwenye bustani kwa kuweka mawe ya kukanyagia

Kwa mandhari ya kuvutia na kukidhi mahitaji ya nje ya nyumba wenye nyumba wengi wanasahau kuweka njia  kwenye bustani. Wengi wanaelekeza nguvu zao kwenye kuweka mandhari ya varanda ivutie ,  kuchagua maua ya bustani, kuweka vitofali vya chini vya kuzuia tope na wachache wenye uwezo wa kuweka mabwawa ya kuogelea hufanya hivyo na kusahau njia ya kwenye bustani  ambayo huunganisha maeneo mengine ya nje ya nyumba na bustani.

Sio tu kuwa njia ya kwenye bustani inamwongoza mtu kujionea uzuri wa bustani bali pia njia hii huleta mhemko. Jinsi ya haraka, rahisi na gharama nafuu ya kutengeneza njia kwenye bustani ni kwa kuweka mawe ya kukanyagia. Mawe haya chimbuko lake ni sherehe za chai za kwenye bustani ambapo mawe ya kukanyagia yaliwekwa ili kuzuia viatu vya wageni visinase kwenye udongo laini wa bustani. Kwa jinsi hii mawe ya kukanyagia yalisaidia kuhifadhi majani na kumwelekeza mgeni eneo mahsusi.

Mawe ya kukanyagia ya kwenye bustani leo hii yanaweza kuwa na lengo lile lile la kutengeneza njia  lakini pia yanaweza kuwa kama mapambo hasa pale yanapokuwa na maumbo na rangi mbalimbali na pia muundo wa njia yenyewe ama kuwekewa taa za kumwongoza mpitaji nyakati za usiku.

Imeonekana mawe ya kikanyagia ni njia rahisi na ya haraka kutengeneza njia kwenye bustani kwa kuwa mawe haya yanawekwa kwa kuchimba kidogo sana na huwa kuna nafasi kati ya jiwa na jiwe kwa hivyo haihitajiki kutafuta tambarare. Na pia yanafunga eneo kubwa kwa mawe machache.  Hauwi na wasiwasi na msingi wake kama vile ambavyo unajali msingi kwenye kujenga ukuta ama sakafu ya nyumba. Mawe ya kukanyagia hayahusiki katika kanuni ya msingi imara. Mara nyingi mawe haya hayawekwi kutengeneza njia ulioonyooka kwani kwa historia ya njia ya bustani nia ni kumwezesha mpitaji kuitazama na kuifurahia bustani kwa ukaribu zaidi maeneo mbalimbali.  Njia za kutembea kwenye bustani zina jinsi ya kupunguza mwendo na kufurahia uasili ya bustani.

Mawe ya kukanyagia kwenye bustani yafaa yatengenzwe kwa zege au kama ni mawe ya asili kama yale ya tanga pia yanafaa.  Yawe flati na kwa ukubwa wa mtu kutembea kwa uhuru na unene wake uwe wa inchi mbili. Umbali kati ya jiwe na jiwe uzingatie pia hatua za watoto wadogo kwa hivyo yasiwekwe mbalimbali sana.
Mawe ya kukanyagia ya kwenye bustani yanakuwa kwenye maumbo mbalimbali kwa mfano pembe nne, pembe sita, duara au hata bila ya umbo maalum ni kwa kadri ya ubunifu wako tu wakati wa kuyatengeneza. Weka mawe haya yatokeze juu ya ardhi kiasi cha inchi moja. Hii itasaidia kuwa na sehemu kavu ya kukanyaga na bado ukaweza kupitisha mashine wakati wa kukata majani.

Kwa usalama, eneo la kuwekea mguu lisiwe laini kwa jinsi ambayo mtembeaji anaweza kuteleza kwa mfano nyakati za mvua mawe yakiwa yameloa. Wewe na mtu wako wa bustani mnayaweka mawe kwa uangalifu kwa kuzingatia, umbo la mawe na saizi na mnaweza kutengeneza njia ya kuvutia mno kutokana na maumbo na rangi za mawe yenyewe.

Leo hii mawe ya kukanyagia kwenye bustani ni kwa matumizi na mapambo na sio kama mawe yanayowekwa kwenye madimbwi kukuwezesha kuruka tope ili kufanya miguu yako isilowe na kuchafuka. Mawe ya kwenye bustani yanakuruhusu kutembea kwenye bustani bila kuloa umande au kukanyaga  matope. Yanaweza kuongeza rangi na maumbo mapya kwenye bustani kwa nia ya mapambo. Mawe haya ni rahisi kutengeneza na kuweka, unaweza kufanya mradi wa kuyatengeneza na kuyaweka kwenye bustani mwenyewe ukiwa na msaidizi mmoja tu. Njia za kwenye bustani zinasaidia kupunguza kasi ya mwendo kwa hivyo kufurahia uasili wa mandhari ya bustani.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda viviobed@yahoo.co.uk au 0755 200023

No comments:

Post a Comment