Pages

Thursday, August 29, 2013

my article for newspaper: tai za pazia



Ongeza unadhifu  wa chumba kwa kutumia tai za pazia   
                                                                                
Tai za pazia ni kwa ajili ya matumizi na mapambo. Kutokana na mitindo lukuki iliyopo ya tai hizi, unaweza kupata seti ya tai ambayo itaendana na mapambo yako mengine ya ndani. Nia kuu ni kushikilia pazia mbali na dirisha hivyo kudhibiti kiasi cha mwanga unaotaka kuruhusu uingie ndani kwa kuwa na uwezo wa kufungua pazia zikashikiliwa kwa tai na wakati huo huo ukaongeza umaridadi wa muonekano.

Tai za pazia ni njia rahisi ya kufanya pazia za kitambaa kuonekana nadhifu na maridadi, au kwa kudumu ama wakati wa mchana. Baadhi ya watu wanapendelea kuacha pazia wazi wakati wa mchana na kuzifunga usiku. Hii inasaidia kuongeza mwanga wa asili chumbani na kuleta hisia za usalama zaidi usiku. Kwa kufungua pazia zionekane maridadi, tai za pazia ni suluhisho. Kwa kawaida tai hizi zinashikiliwa na vishikizo ama kulabu zinazochimbiwa ukutani karibia na dirisha. Vishikizo  hivi vyaweza kuwa vya mbao au chuma na vinawekwa kutegemea na staili na uzito wa pazia zikihudumia kuendana na mapambo ya chumba.

Tai za pazia zinatengenezwa kwa unene tofauti kutokana na uzito na staili ya pazia. Tai nzito zinafaa kwa kushikilia pazia nzito lakini pia zinatumika kwa pazia nyepesi. Tai za pazia zenye kifundo ni maarufu na za kimapambo zaidi na zinatumika kwa pazia za vitambaa vinene na vizito. Kwa sababu tai hizi huwa ni kubwa na nzito hivyo zinaendana moja kwa moja na aina hii ya pazia. Vifundo kwenye tai hizi huwa vinakuwa ni vya kusukwa kwa nyuzi na wakati mwingine huwa vifundo hivi vimeongezewa shanga. Kwa hivyo kwa umaridadi unaweza kuchagua rangi mojawapo kwenye tai itakayooana na pazia na mandhari nyingine za chumba.
Tai za pazia zisizokuwa na maridadi  zimetengenezwa kwa kitambaa chepesi na zinatumika kufungia pazia nyepesi. Rangi zake zinaweza kuendana na zile za pazia. Tai za pazia sio lazima ziwe ni kitu cha kipekee, zinaweza hata kutengenezwa kutokana na kitambaa hichohicho cha pazia. Hii ni njia rahisi ya kutumia kitambaa sahihi cha pazia na tai zake kuendana na mandhari ya chumba.
Tai za pazia zinatofautiana sana kwa umbo na ukubwa. Fikiria ni tai gani zinakazokidhi mahitaji yako na muonekano wa chumba unaotaka kutengeneza. Kwa hivyo wakati wa kunua tai za pazia hakikisha unajua kuwa unataka za ukubwa gani na ziendane kwa uzito na pazia utakazotumia; hii itamalizia muonekano wa chumba. Uwe na uhakika pia wa idadi ya tai unazohitaji, je utataka ziwe kwa seti au moja moja. Ni mara ngapi tai husika zitatumika. Kwa mfano zitakuwa zimeshikilia pazia muda wote kama mapambo au ni wakati wa mchana tu. Kama ni za kufungua na kufunga mara kwa mara basi tumia zile tai ambazo hazina madoido mengi.

Kulabu za kushikilia tai za pazia zinawekwa kwa urefu ambao hautakuwa shida kufungua pazia. Hakuna urefu maalum wa wapi pa kufunga tai za pazia.  Pia fimbo pazia zilikotundikwa zinahusika kwani nyingine ni ngumu kuvuta pazia wakati wa kufungua, kwa hivyo ziwe fimbo ambazo hazina usumbufu ukitaka kufungua na kufunga pazia. Weka fimbo ambazo pazia litateleza kilaini wakati wa kufunga na kufungua.

Kwa kweli pazia zitakuwa hazijakamilika bila tai maridadi za pazia. Kitupio hiki kidogo tu kinabadilisha muonekano mzima na mandhari ya chumba chako.
Iwe nia ni kufungua pazia ili kuruhusu mwanga kiasi kuingia ndani au kuzipa pazia umbo la umaridadi zaidi basi tai za pazia ni muhimu kutimiza malengo haya mawili. Ni muhimu kuisikiliza sauti yako mwenyewe na kutengeneza makazi ambayo yanafaa staili ya maisha unayoishi wewe na ya familia yako. Mitindo inakuja na kuondoka lakini kama utajenga kujiamini na kuwa staili ambayo ni ya kipekee nyumbani kwako hutaangukia kwenye utumwa wa kurukia kila pambo la ndani utakaloona. Kulinganisha na kushindanisha kila pambo madukani kutanyonya nguvu yako ya ndani badala ya kuielekeza kwenye mambo mengine, ukiwa mkweli wa nafsi yako mwisho utapata ladha yako ya kudumu.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023

No comments:

Post a Comment