Pages

Thursday, September 12, 2013

My article for newspaper: Mifuko ya viatu

Jinsi ya kuhifadhi viatu vyako hasa kama una eneo dogo

Inasikitisha viatu kurundikana kwenye boksi au kapu ambapo inachukua muda na kuleta hasira ya kutafuta mwenzake aliko. Unaweza kuondoa adha hii kwa kuhifadhi viatu vyako kwenye mfuko wa viatu kwa kukipa kila kiatu kifuko chake.

Mfuko wa kuhifadhia viatu ni kifaa kinachotundikwa kwa ajili ya kuweka viatu kwenye mpangilio na hutundikwa kwenye kulabu za nyuma ya mlango au ndani ya mlango wa kabati la nguo.
Mifuko ya viatu ni njia ya gharama nafuu kuliko zote ya kuhifadhi viatu na ni suluhisho tosha kama una eneo dogo na hata kama umepanga chumba kimoja au wewe ni mwanafunzi anayeishi hosteli.. Unachotakiwa ni kununua mfuko wako, kuutundika nyuma ya mlango na kuanza kuhifadhi viatu vyako. Ikiwa inapatikana kwa rangi na vifaa vya kutengenezea mbali mbali iwe ni plastiki, kitambaa au wavu, mifuko ya viatu imetengenezwa wa ajili ya kuhifadhia viatu wakati ikichukua nafasi kidogo sana ya nafasi uliyonayo. Mifuko hii kwa kawaida sio gharama kubwa na inadumu miaka nenda rudi.

Kwa baadhi hasa wale walioishi nje ya nchi kwa kuwa maeneo ni madogo kwa mfano nyumba zijulikanazo kama apatimenti matumizi ya mifuko ya viatu nyumbani ni kitu cha kawaida na wakati mwingine huitumia mifuko hii kuhifadhia vitu vingine zaidi ya viatu. Faida zake hasa kwa wenye nafasi ndogo ni matumizi mazuri ya eneo ukilinganisha na matumizi ya vitu kama boksi au kapu. Zaidi ya hayo mifuko ya viatu itasaidia viatu viwili visisuguane hivyo kuvifanya vidumu muda mrefu na pia kuondoa adha ya kutafuta kiatu cha pili!

Mifuko mingi ya kutundika ya viatu ina vifuko kwa ajili ya kuhifadhi kiatu kimoja kimoja. Mara nyingi vifuko hivi vinaonyesha kilichomo ndani kwa hivyo ni rahisi kuona kiatu na kuamua ni kipi unataka kuvaa. Mifuko mingi ya kuwekea viatu vifuko vyake viko wazi juu.

Baadhi ya mifuko ya viatu vifuko vyake vina zipu juu kama mifuko ya nguo. Hii yenye zipu inafaa zaidi kama unasafiri mara kwa mara na pia kuwekea viatu ambavyo huvivai mara ka mara , unafunga zipu ili visijae vumbi. Watu wanaosafiri mara kwa mara mifuko ya viatu yenye zipu inafaa zaidi kwani wakati wa safari unachofanya ni kunyanyua mfuko wako, kuuweka ndani ya begi huyooo unaondoka.

Kuna baadhi ya maduka hasa maduka makubwa ya vifaa vya nyumbani ambapo mifuko hii inapatikana kwa ununuzi. Pia kwenye maduka mengi yanayouza zaidi viatu mifuko hii inapatikana ya aina mbalimbali. Kama hujapata mfuko wa viatu unaopendelea kwenye maduka hayo basi waambie wakuagizie kwani wao wanasafiri mara kwa mara kuchukua viatu kwa watengenezaji wa nje. Na hawa watengenezaji huwa lazima wanatengeneza na mifuko ya viatu.
Ukubwa wa mifuko ya viatu unabeba kati ya jozi nne hadi ishirini za viatu na mingi ni ya kila kiatu kuwa na kifuko chake.                                                                 

Inawezekana vifuko vya mfuko wa viatu kuhifadhia vitu vingine zaidi ya viatu. Kwa mfano katika chumba cha mtoto mchanga vifuko hivi vinaweza kutumika kuhifadhia visoksi na vinguo vingine vya king’aling’ali. Kichanga kinavyokuwa vifuko vya chini vinaweza kuhifadhia vidoli vyake wakati vinguo zisivyo kwenyen msimu vyaweza kuhifadhiwa kwenye vifuko vya juu.
Kwenye kupanga vitu kwenye chumba cha kulala vitupio na vipodozi vinaweza kuhifadhiwa kwenye mfuko wa viatu uliotundikwa nyumba ya mlango. Vifuko vinaweza kutumiwa pia kwa kuhifadhi soksi.

Mfuko wa viatu unaweza kutumika pia ofsini kwa matumizi mengine mbali na viatu hasa vile vitu ambavyo unatumia mara kwa mara na unataka ukinyanyua mkono tu unabeba kwa mfano mkasi, pini za stepla na kalamu za maka. Na mara nyingine kunakuwa na nyaya nyingi maneneo ya ofsini kama za kompyuta, kamera simu za masikioni na chaja za simu. Mara nyingi nyaya hizi zinajifungafunga na inakuwa ngumu kuzitenganisha. Suluhisho linaweza kupatikana kwa kuhifadhi nyaya hizi kila moja kwenye kufuko chake ndani ya mfuko wa viatu. Ni ubunifu tu unahitajika!

Mfuko wa viatu unaweza kutumika kama suluhisho la kuhifadhia bafuni. Kama mfuko ni wa plastiki vifaa vinavyotumika kila siku bafuni kama brashi, shampoo kitaulo cha uso, vyanuo  na vifaa vingine vya usafi vilivyo kwenye chupa vinaweza kuhifadhiwa kwenye vifuko vya mfuko wa viatu badala ya kurundika kila kitu juu juu.

Mifuko ya kuhifadhia viatu unaweza kuiita mifuko ya miujiza kwa kuhifadhia vitu mbalimbali. Unaweza kuitundika katika kila mlango hata ikapelekea kupungukiwa na milango ya kutundikia! Vifuko vyake kwakweli ni suluhisho kwa kuchambua na kuhifadhia vitu vidogo vidogo. Watoto wanaojifunza kazi zao za shule za sanaa kwa mfano, unaweza kutumia vifuko vya mfuko wa viatu kuhifadhia penseli, rangi na mifutio humo badala ya kila kitu kuzikwa kwenye madroo.  Mifuko ya viatu ni bei rahsi mno, rahisi pia kutundika na hii inaifanya kuwa chaguo sahihi kwa ajili ya kuhifadhia viatu vyako na vitu vingine vingi hasa kwa wale wenye eneo dogo au mwenye nyumba anayetaka unadhifu tuseme umepanga chumba kimoja ndani ya nyumba yake.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

UPDATE: Mwenyeji wangu wa kwenye interview amepata dharura mtoto wake anaumwa kwa hivyo tutafanya kesho, na kipindi kitakuwa recorded, kitawekwa hewani siku za mbeleni.

No comments:

Post a Comment