Pages

Thursday, October 10, 2013

My article for newspaper: Feni

Zaidi ya kuleta ubaridi na matumizi nafuu ya nishati na pesa, feni pia ni pambo la ndani

Wakati wa majira ya joto, ni ngumu kukaa ndani na kujisikia burudani, starehevu na amani  bila kupandisha bili ya umeme. Wakati huo ndipo kila mmoja anahangaika ni kwa vipi aweze kumudu ndani kuwa na ubaridi. Kwa bahati nzuri suluhisho ni rahisi zaidi ya kuwekeza kwenye kiyoyozi. Ingawa kwenye maeneo mengine ya nchi kiukweli ni kuwa wakati wa joto kiyoyozi kinahitajika kwani kwa kawaida maeneo hayo joto huwa ni kali sana. Lakini pale unapotaka kuweka chumba kimoja kipoe kidogo feni inaweza kuwa ni suluhisho.

Ni muhimu kujua kuwa feni haipunguzi joto ila inatengeneza mpepea ambao unamfanya mtu asikie ubaridi kwani mpepea huo unasaidia kuvukiza jasho toka kwenye ngozi ya mtu huyo. Ni hisia hiyo hiyo unayopata pale unapofungua kioo cha gari likiwa linatembea. Kuweka feni kila chumba ambacho watu wanakaa inasaidia wanafamilia kupooza miili wakati wa joto wakati huo huo ikiwa ni matumizi nafuu kipesa kulinganisha na kiyoyozi. Teknolojia imewezesha kuwa na aina za feni za matumizi madogo sana ya nishati kulinganisha na miaka ya nyuma. Tafiti zinasema kuwa feni inaweza kuwasaidia wenye nyumba kupunguza matumizi ya nishati kwa hadi asilimia hamsini ya ambayo ingekuwa bili ya kiyoyozi kwa kutengeneza mpepea ambao unafanya joto kuwa chini kwa nyuzi 7  hadi nane za sentigredi kuliko ambavyo ingekuwa bila feni wala kiyoyozi.

Feni zipo za kwenye dari, za mezani, za sakafuni na za ukutani. Feni hizi zinatengeneza mzunguko wa upepo ambao unakuweka burudani zaidi nyumbani kwako, hata kama una vipoozeo vingine kama uingiaji ndani wa hewa ya asili au kiyoyozi.
Feni ya kuning’iniza darini inachukuliwa kuwa ndio yenye ufanisi zaidi kwa kuzungusha hewa kwenye kila eneo la chumba.  Pia feni ikiwashwa pamoja na kiyoyozi inasaidia kupunguza matumizi ya umeme kwani unasetia kiyoyozi kwenye fukuto la juu kwa kuwa feni inakuwa imeshaleta mpepea tayari (ukisetia kiyoyozi kwenye fukuto la chini ndivyo kinavyokula umeme mwingi).

Feni za darini zinatakiwa kufungwa sehemu ambayo ukuta wake una urefu wa si chini ya futi nane ili mapanga yake yaweze kufanya kazi vizuri. Feni zenye mapanga makubwa zinazungusha mpepea zaidi ya zenye mapanga madogo. Pia mapanga makubwa yanafanya kazi nzuri kwa kasi ndogo kuliko madogo. Ukubwa wa feni uendane na ukubwa wa chumba, kama chumba ni kikubwa kwa mfano sebule, weka feni zaidi ya moja. Feni izimwe wakati ukiondoka chumbani kwani inapooza ngozi za watu na sio chumba.  Kwa nyumba kubwa, kufunga feni ndogo ya darini kwenye chumba cha kufulia na chumba cha kuvalia si jambo la ajabu. Kwenye bafu za wakuu wa familia pia ni mahali sahihi pa kufunga feni ndogo kwani mvuke wa maji ya moto na vikausha nywele vinaweza kufanya bafu liwe na joto na mnato. Kifeni kidogo cha darini kitaleta burudiko mahali hapo.

Feni ya bei kubwa inafanya kazi kiufanisi, kiulaini na kimya kimya zaidi ya ile ya bei ndogo. Hakikisha kiwango cha kelele kilichoandikwa kwenye feni kabla ya kuinunua na kama itawezekana isikilize ilifanya kazi kabla ya kuinunua. Na pia nunua feni yenye lebo inayoonyesha matumizi ya nishati kwani feni ya aina hii ina ubora kuliko ile isiyoandikwa chochote. Pia hakikisha kwamba feni unayotaka kununa ni ya mazingira ya nje au ndani ya nyumba, kwa mfano feni ambayo imeandikwa ni ya ndani haitakiwi kutumika nje – hata kama eneo limezibwa sana. Unyevu na uchepechepe unaweza kuathiri ufanyaji kazi wa mota na mapanga ya feni.
Kuna aina mbalimbali tofauti za feni za nje kutegemea na mahitaji na vitu vilivyoambatana na feni hiyo. Kuna ambazo zina taa zilizoshikiliwa humo humo, kuna za rimoti na zenye virekebisho vya ukutani na mwendo wa mpepea. Watengenezaji wa feni za nje pia wanaweka bwembwe za mapanga yanayofanana kama majani. Kwahivyo ukiona feni ya hivyo unajua moja kwa moja kuwa ni ya mazingira ya nje ya nyumba. Pia feni zenye maelezo kuwa zinaweza kuwekwa maeneo ya maji maji ndio zinafaa nje kama kwenye varanda na kadhalika. Feni ya kwenye varanda ikiwa ni ya kuninginia darini na yenye taa humo humo inafaa zaidi.

Mitindo ya feni ipo mingi bila kikomo na baadhi yake imetumika kama mapambo. Kwa mfano kuna mapanga ya feni ya rangi mbalimbali tofauti za kuendana na mapambo yako ya ndani.  Staili mbalimbali za feni zinawezesha kuendana na fenicha zilizopo chumbani. Pia kwa kusisitiza mapambo yako ya ndani unaweza ukachagua nyumba ya mota kwa rangi unayoitaka. Na kama ulikuwa hujui, unaweza kupaka rangi unayoipenda kwenye mapanga na mota kabla ya kufunga feni. Ni rahisi hasa kama mradi wako ni wa kufunga feni nyumba nzima.

Utashangaa ni kwa namna gani feni inaweza kuleta mabadiliko nyumbani kwako, na kama ukiwa na moja kwa kipindi, utapigwa na butwaa ni kwa vipi uliishi bila kuwa nayo.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment