Pages

Wednesday, October 23, 2013

My article for newspaper: Muonekano wa bustani mahali ndoa inapofungwa






Apa kiapo cha ndoa yako mahali pa kipekee na pa kumbukumbu maishani kwa sababu unastahili. Kwa kawaida ndoa zinafanyika, nyumbani kwa ndoa za kimila ama kwenye nyumba za ibada ama kwa ofisi za msajili wa ndoa wa serikali. Ila kwa siku za karibuni kutokana na utandawazi dunia imekuwa kijiji kwa hivyo kusababisha walimwengu kuigana tamaduni hasa zile ambazo jamii husika inaona zinafaa. Eneo mojawapo lililoathirika na utandawazi ni hili la mahali pa kufungia ndoa. Ndoa za kufungwa kwenye bustani au maeneo mengine kama ya makumbusho na vivutio vingine ni jambo linalokuja kwa kasi na ni tamanio la mabibi harusi wengi.

Harusi inaweza kuwa ndilo tukio maalum kuliko yote kwenye maisha ya mtu. Ni tukio la maajabu na hata hivyo linaweza kuleta msongo wa mawazo hasa kwa muoaji na muolewaji ila siendi kuongelea hilo kwa sasa. Tunaenda kuangalia muonekano wa eneo la bustani ambapo ndoa itafungwa namna ya kulifanya lionekane maridadi kuwa na mpangilio hivyo kufanya tukio la kufunga ndoa yako kuwa la kipekee kuanzia pale wanapokaa viongozi wa kufanga ndoa, bwana na bibi harusi hadi kwa wageni waalikwa.

Kila bibi harusi mtarajiwa anachagua rangi za harusi yake kutokana na matakwa yake binafsi, lakini kupamba kwenye bustani inamaanisha kuwa asili imeshakufanyia nusu ya kazi yako! Ni kama umeshapewa bonasi ya mapambo kwa ndoa inayofungiwa kwenye bustani ila hata hivyo bado unatakiwa kufanya kazi kidogo. Tembelea bustani husika wiki moja kabla ya harusi kuhakikisha kuwa majani yamekatwa, chini kumerekiwa na maua yamekatiwa. Kama kuna upungufu wa maua labda ni kipindi cha jua kali hakikisha unaongeza hata kama ni ya vyungu toka kwa wauzaji.
Kama mmeamua kuapa kiapo chenu cha ndoa kwenye bustani kuna mawazo lukuki ya jinsi ya kufanya eneo hili livutie kwa wageni na kwa picha zenu za kumbukumbu kwa siku hiyo kubwa!
Kwanza kabisa angalia hapo mahali kama kuna kitu cha asili kama vile mti. Kwenye eneo hili ndipo utakapoweza kuweka kijukwaa kwa ajili ya viongozi wanaofunga hiyo ndoa. Na unaweza kuninginiza mapambo kwenye mtio huo vile vile. Leo, zaidi ya ilivyowahi kuwa, kijani cha bustani ni pambo tosha, usichezee hela kununua maua mengi ya ziada, tumia vitu vya asili vilivyoko eneo hilo hilo la bustani. Chagua mapambo machache sana ya rangi ambazo zitaendana na zilizopo kwenye bustani asili tayari, badala ya kuchagua ambazo zitashindana nazo.

Baada ya hapo panga viti vya mashuhuda/wageni watakaofika kushuhudia mkifunga ndoa. Tumia viti vya kuvutia kwa rangi na staili zinazokubaliana na mandhari yako. Viti vingi vya bustanini ni vya chuma  na mbao ambavyo vinaweza kuwa sio burudani kwa kaa kwa muda. Ukiweza kutupia mito ya viti itakuwa bora zaidi na pia inaongeza mguso wa mapambo.

Kwenye hivi viti panga vikae mpangilio wa pande mbili kwa maana ya kuacha njia katikati ya pande hizo. Kwenye viti vya mstari wa  pembezoni mwa njia unaweza kupamba kwa kuvifunga tai na maua. Kama ni eneo lenye jua kali sana hakikisha mpambaji wako anatayarisha maua lakini ayafunge dakika chache kabla ya tukio kuanza ili yasinyaukie juani.

Kwenye njia iliyoko kati ya pande mbili za viti acha uzuri wa asili wa majani ya bustani, huna haja ya kutandika zulia kwenye njia hii. Badala yake kwa kusaidia viatu wa bibi harusi na wageni wengine waliovaa viatu vya kisigino chembamba kinachoweza kuchimba chini kutokana na udongo laini wa bustani weka mawe ya kukanyagia kama yale ya Tanga ambayo yana kawaida ya kuonekana kwenye bustani kwa hivyo nayo ni kivutio. Pia weka mahali pa kuingilia kwenye eneo hili la bustani lililotengwa kwa shughuli na papambe.

Fikiria hali ya hewa na muda. Si busara kukaanga wageni wako kwenye jua kali kwa mfano. Chagua muda ambao jua sio kali kwa kuwa hutaki kuweka kivuli kwa ajili unataka uzuri wa asili wa bustani. Pia ni vyema ukatenga eneo la mbali kidogo hapo hapo bustanini kwa kuweka paa endapo una wasiwasi wa mvua kunyesha. Na hakikisha wale wageni wanaotoka mbali na hawajui hali ya hewa ya eneo husika unawataarifu kabla. Wengine wanapenda kupaka yale mafuta ya kuzuia jua.

Weka alama za kuelekeza wageni. Bustanini panapofungwa ndoa panaweza kuwa ni mbali toka wageni wanakoshukia, labda kwa mbele kuna jengo kwa mfano na bustani ipo nyuma ya hilo jingo. Inabidi kuweka alama za kuwaonyesha wageni wako eneo bustani ilipo. Vibao vyako vya kuelekeza vinaweza kuandikwa pia lugha ya wageni wako wengine ambao hawajui lugha kuu ya hapo kama wapo. Kwa mfano inawezekana kuna wageni wasiojua Kiswahili, hakikisha  umewawekea lugha yao nao wajisikie wapo nyumbani. Vibao hivi visiwe tofauti na mandhari nzima ya rangi zako za harusi ulizochagua.

Je kila mtu anaweza kusikia? Kama ukipiga picha ya ndoto yako ya kufungia ndoa kwenye bustani karibia na bahari pata picha upepo na kelele za watoto wanaocheza ufukweni. Usisahau kipaza sauti mahali pa kufungia ndoa. Mtu wako wa mziki ataweza kukusaidia katika hili.

Yote kwa yote kumbuka kuwa ndoa ni cheti! Hakikisha taasisi zinazohusika zinakubaliana na ndoa kufungiwa eneo ulilochagua.
Kama umeamua kufungia ndoa kwenye bustani, hongera! Ndoa hizi zina mahaba na ni nzuri. Nakutakia safari njema ya hatua inayofuata ya kuelekea kwenye sherehe ya harusi.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment