Pages

Wednesday, October 16, 2013

My article for newspaper: Zingatia haya kabla ya kununua shuka



Shuka ni kitu rahisi tu ila kama unasoma makala hii, ni kuwa unajisikia kuzidiwa nguvu na aina zilizopo au umechoka kufanya manunuzi mabaya. Usingizi mzuri wa usiku una matokeo makubwa ya ni jinsi gani unafanya kazi na kujisikia wakati wa mchana, na shuka unazolalia zinachukua nafasi kubwa ya kilele cha matokeo haya. Zaidi pia ni kuwa unataka kununua shuka ambazo zinatosha godoro na zisizochakaa mapema.

Ni kitu gani cha kwanza ambacho mtu anaona wakati anapoingia kwenye chumba chako cha kulala? Bila shaka ni kitanda. Ni ajabu kama utakuwa na chumba cha kulala kisichokuwa na kitanda. Pengine kitanda ndio sababu kubwa inayofanya uite chumba hiki kuwa ni cha kulala! Unaweza ukaboresha muonekano wa chumba chako cha kulala kwa kutandika kitanda shuka laini na kufunika kwa duveti tu bila kugusa maeneo mengine ya chumba. Hii inakupa maboresho ya chap chap kwa hivyo kuokoa muda na pesa.

Kuna rangi na mitindo mingi ya shuka sokoni. Unakumbuka wakati shuka zote zilikuwa ni za pamba na ni za kijani? Kama ndio basi bila shaka utakuwa unapigwa na butwaa ni shuka za aina ngapi zilizopo sokoni leo hii. Unaweza ukaongeza rangi, staili na michoro mbalimbali kwenye chumba chako cha kulala kwa kutumia shuka na duveti za kisasa. Endelea kusoma hapa ili ujue ni nini cha kufanya kabla hujatumia hela yako ya thamani kununua shuka mpya.

Pima ukubwa wa kitanda chako. Kuna uwezekano mkubwa umeshasikia hiyo lugha ya vitanda vya ukubwa wa twin, au queen au king. Usidanganyike na majina haya ya vitanda, kiukweli ni kuwa hakuna vipimo sahihi vya kitanda kwa majina haya. Sasa kabla hujaenda kununua shuka, pima kitanda chako kwa umakini ukichukua vipimo kutoka kichwani hadi miguuni, upande kwa upande na unene wa godoro. Kuwa na uhakika unajua kwa usahihi ni nini unahitaji kabla ya kununua.

Shuka nyingi zinauzwa kwa hayo majina kama hayo yanayoweza kukuvutia hapo juu kuhusu ukubwa wa kitanda. Usidanganyike, kwa kuwa tayari una vipimo sahihi vya kitanda chako, kama ni ile aina ya shuka ya kufitisha kuvalisha godoro hakikisha inazidi inchi mbili ya vipimo ulivyo navyo ili kuwa na kitambaa cha kutosha kusaidia kuvalisha kona za godoro. Kama ni aina ile ya shuka ambayo ni flati basi hakikisha kinaongezeka kitambaa cha kutosha cha kuchomekea ili shuka isikimbie godoro unapokuwa umelala. Kuwa makini, wataalamu wanasema shuka nyingi zinapungua kwa asilimia saba ya ukubwa wake baada ya kufuliwa kwa mara ya kwanza, na shuka zenye asilimia mia ya pamba zinapungua zaidi!

Shuka nyingi zinawekwa rangi baada ya nyuzi zake kusukwa, ambapo inazifanya kuwa ngumu mpaka baada ya kufuliwa mara kadhaa. Zile shuka zinazotengenezwa na nyuzi zilizotiwa rangi kabla ya kusukwa huwa ni laini na ni za bei kubwa zaidi.
Soma maelezo ya lebo ya mtengenezaji wa shuka husika, yatasema wingi wa nyuzi zilizotumika kutengenezea kwa kila inchi moja ya mraba. Baadhi ya wanunuzi hawajui kuhusu wingi wa nyuzi na pengine shuka zinapitishwa na muuzaji (labda ni ofsini muda wa chakula la mchana) watu wananunua bila kusoma maelezo. Wingi wa nyuzi unasababisha ubora wa shuka. Kwa kiwango cha kitaalam wingi wa nyuzi uwe zaidi ya 250 na usiwe chini ya 175. Kwa shuka ambazo utalalia kila, raha jipe mwenyewe, nunua zenye ubora wa juu kwa kiasi ambacho utamudu. Zaidi ya yote ni imani kuwa utatumia saa nane kwa siku ukiwa umezilalia!
Ukiwa unanunua shuka mguso wa kitambaa ni muhimu pia. Pamba ni kitambaa cha shuka ambacho ni maarufu zaidi, ingawa baadhi ya watu wanapendelea shuka zenye mchanganyiko wa pamba na labda satini ama hariri ama polista ili kupunguza kujikunja kunja. Shuka za mchanganyiko wa pamba na polista ni imara zaidi na hazijikunji kunji ila changamoto yake  ni kupoteza ulaini na ni ngumu kuondoa madoa ukilinganisha na pamba tupu.
Angalia maelezo ya ufuaji. Labda shuka unazotaka kununua ni ambazo ni lazima zifuliwe kwa mafuta maalum tu (hazifuliwi na maji) hivyo kutakuwa na gharama ya kuzipeleka dry cleaner kila wiki. Je utamudu hiyo? Hakikisha utaweza kutunza shuka zako jinsi mtengenezaji alivyopendekeza. Zitadumu muda mrefu na hata kama ikitokea tatizo na ukiwarudishia wakijiridhisha kwamba zilikuwa zinatunzwa inavyotakiwa watakusikiliza.

Amua kama unataka kununua shuka zako kwa seti ama moja moja. Nunua nyingi kuliko unazohitaji. Kama umetumia muda mwingi kutafiti na kupata jibu la ni shuka zipi unahitaji huna haja ya kufanya zoezi hilo tena ndani ya kipindi kifupi. Fikiria kununua seti mbili ama tatu ambazo zinaendana kwa ajili ya kubadilisha ili hata kama mtu amemwaga kitu kwenye shuka la juu unalibadili hilo peke yake bila kuhusisha la chini.

Pata muonekano na weka staha kwenye chumba chako cha kulala kwa mvuto wa juu kwa rangi na mitindo mbali mbali ya shuka, mwisho wa siku ni wewe unalala humo. Na kinachojalisha zaidi wakati huo ni burudani. Hutaweza kulala kwa raha kama huna matandiko  laini na safi.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment