Pages

Friday, January 24, 2014

my article for newspaper: rangi za mazulia


Kupamba nyumba yako ni zaidi ya kuchagua rangi za kuta na aina ya fenicha — unatakiwa pia uchague rangi sahihi ya zulia.
Kuchagua rangi sahihi za mazulia kwa ajili ya nyumba yako sio uamuzi mdogo, mazulia ambayo utakaa nayo kwa miaka. Kwa ajili kuweka mazulia ni moja ya mapambo ya ndani yanayogharimu zaidi kimuda na kipesa. Kwa mfano si busara kutandika zulia la ukuta kwa ukuta ambalo unategemea kuondoa chini ya miaka mitatu. Kwanza si kazi ya kitoto kuanza kutoa vitu ndani kwa ajili ya kutanzika zulia la aina hii, na pili huwa zulia hili ni kubwa kwa hivyo pia ni gharama. Nimefanya mahojiana na Bi Aisha Idd ambaye anauza mazulia ya nyumbani kutaka kujua mambo ya kuzingatia kwa upande wa rangi wakati wa kununua mazulia ya nyumbani.
Bi Aisha anasema michoro na rangi za mazulia zinabadilika kila wakati kwa hivyo kwa ajili mazulia ni gharama, unatakiwa kuchagua yale ya rangi ambazo zitaoana na muonekano wa sasa ama mipango ya baadaye kama ipo juu ya nyumba yako. “Kwa kawaida rangi za mapambo ya sakafu huwa zinakuwa nyuma mwaka 1-2 kulinganisha na zile rangi za mitindo ya nguo, anasema Bi Aisha” Hii ina maana kwamba rangi maarufu zaidi kwenye maduka ya nguo za wanawake, zitaanza kuonekana kwenye sakafu za nyumba miaka kadhaa mbele. Upo hapo!
Kwa mazulia ya nyumbani ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa sasa ni rangi za dhahabu, kijani, silva, damu ya mzee na rangi ya udongo. Rangi zisizokolea au kwa maneno mengine rangi za mwanga kama vile bluu, khaki, kijivu na rangi ya maziwa zinaonekana kuwa maarufu zaidi kwa sasa. Hata hivyo hakuna rangi ambayo inashika kasi kwa sasa kama kijivu na khaki na wala haijalishi mabadiliko ya mara kwa mara ya rangi hizi. Aisha anasema labda ni kutokana na kuwa kuna jinsi nyingi ya kuoanisha rangi hizi mbili na vizulia vya kutupia.  
Sasa basi wakati wa kuchagua mazulia kwa ajili ya sakafu za nyumba yako zingatia mambo kadha wa kadha. Bahati nzuri ni kuwa vizulia vile vya kutupia baadhi ya maeneo vinakuja kwa bei, michoro na rangi lukuki ambapo ushindwe wewe tu. Kwa kweli sio ngumu kupata ukubwa na rangi unazotaka kwa uwezo ulio nao. Siku zote kumbuka kuwa uchaguzi wako wa mazulia ya nyubani kwa kila chumba ni msingi wa ladha yako.
Baadhi ya dondoo zifuatatzo zitakusaidia kuchagua rangi sahihi ya mazulia ya kwenye vyumba vya nyumba yako. Kwa kuwa zulia huwa ni la kudumu na kuweka la rangi fulani ni  uamuzi wa gharama kufanya, hapa ni dondoo chache za kukusaidia katika uamuzi huo mgumu.
Kwanza kabisa fahamu kuwa zulia ni moyo wa nyumba yako. Linatoa utambulisho wako hasa lile la sebuleni. Kwa vile mnachukua muda mwingi sebuleni kama familia, fikiria rangi ambayo inaenda kukubaliana na mfumo wa maisha yenu. Je sebule yako ni rasmi au ni ya kujimwaya mwaya?
Kuamua ni mazulia ya rangi ipi ununue, fahamu ni kwa kiasi gani yatakanyagwa. Zulia linavyozidi kukanyagwa ndivyo kuna uwezekano wa kuchafuka kwa maana ya kumwagikiwa vimiminika vilivyobebwa na wapitaji, madoa na majasho ya miguu. Mazulia ya rangi za mwanga kwa mfano khaki na kijivu huonyesha uchafu kirahisi lakini yanaweza kusafishika kwa dawa za kuondoa madoa kwenye mazulia ila kama mazulia yenyewe sio imara basi yataanza kuonyesha alama za uchakavu kwenye maeneo hayo ukiliinganisha na mazulia ya rangi za giza. Kama una wanyama wa ndani au sakafu ya nje ya nyumba isiyo ngumu ni rahisi mazulia yako kuchafuka kuliko yule anayeishi kwenye nyumba yenye mazingira ya nje yaliyowekwa sakafu ngumu. Familia nyingi haziweki zulia jikoni.
Fikiria matumizi ya eneo ambapo zulia litawekwa kabla ya kuamua rangi. Je unataka zulia lilete mwanga ama lipunguze mwanga chumba ambacho kina mwanga mkali zaidi? Nyekundu ni sahihi kwa vyumbani, sebuleni na kwenye ujia kwani haionyeshi madoa kwa hasira kama rangi za mwanga. Ila kwa vyumba ambavyo vina kiasi kikubwa cha mwanga wa jua fikiria juu ya zulia kuchuja, tatizo ambalo linaonyesha sana kwenye zulia za rangi za giza.
Kuchagua rangi kunahusika sana na vitu mbalimbali anbavyo vinahusika kwenye zulia hilo. Chagua rangi za giza kama kuna watoto wadogo ili kuficha yale madoa yasiyoepukika. Kama una wanyama wa ndani fikiria vitu kama tope wanaloweza kuingiza. Hata kama huhusiki na hivyo vyote basi fikiria hata sherehe na wale wageni ambao kwa vyovyote vile hawatainama kuvua viatu vyao!
Chagua rangi ya zulia itakayoendana na haiba na mazingira ya nyumbani kwako. Kwa mfano, kuna familia ambazo kuna sebule rasmi kwa ajili ya wageni tu na kuna nyingine ya  familia. Hii rasmi huenda kwa kawaida huwa na muonekano wa rangi za kifahari na rangi za mazulia yake huwa ni moja kwa mfano zulia la sakafu yote ya sebule rasmi yaweza kuwa ya rangi ya maziwa. Sasa kabla ya kuamua rangi ya zulia jiulize je unapenda kutembea kwenye chumba ambacho zulia lake lote ni la rangi moja tena ya mwanga?
Rangi za zulia utakazochagua zinahusiana vip na rangi za kuta na mapambo mengine hapo chumbani? Kila chumba kinahitaji sehemu moja ambayo ni kitovu. Zulia lako linaweza kuwa ndio kitovu, hautaki zulia lishindane na mapambo yako mengine kwa ajili chumba kinaweza kuonekana vurugu vurugu.
Shirikisha wanafamilia na chukua kura! Kwa ajili wote mnaenda kutumia mazulia haya, inaweza kuwa vyema kujua ni rangi zipi familia yako inaona zitafaa zaidi chumba fulani. Lete sampo nyumbani mshauriane pamoja. Huenda ukagundua rangi ambayo haukuwa umeiwaza mwanzo.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange.  Vivi ni mjasiriamali  upande wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment