Pages

Thursday, February 6, 2014

My article for newspaper: Sinki la jikoni

Jinsi ya kupata sinki la jikoni litakalokufaa

Jiko linaweza kuwa moyo wa nyumba lakini sinki ndilo linabeba dhamana kubwa ya kazi ya jikoni. Hii ni kwa sababu ndani ya sinki ni mahali pekee panapotumika kwa shughuli  ya mwanzo na ya mwisho kwa chochote kinachofanyika jikoni. Ni mahali panapotumika zaidi wakati wa kuanza kupika na kumalizia kusafisha baada ya kupika. Sinki ni kiungo muhimu kwa jiko lolote. Linakuwezesha kufanya shughuli kadhaa kama vile kuosha vyombo, kujaza sufuria maji na kuosha mikono yako. Pia ni muhimu kwa muonekano wa jiko na linafanya chumba cha jiko kionekane maridadi.
Ingawa sinki imara linaweza kudumu hadi miaka 15 lakini huwa linachakaa, anasema muuzaji Awadh Hafidh. Rangi yake kwa mfano yale masinki ya rangi ya bati laini lisiloruhusu kutu inaanza kufifia, na kuvujisha maji kwa kuudhi kunaanza kutokea baadhi ya maeneo. Na kama unafikria marekebisho ya jiko ni busara kubadilisha sinki na bomba zake.

Masinki ya jikoni sokoni yapo ya maumbo mbalimbali ila aina kuu mbili za kawaida sana ni masinki yenye karai moja na yale yenye karai mbili. Sinki la karai moja linakupa karai pana zaidi. Hili linafaa zaidi kama utakuwa na vyombo vingi vya kuosha kwa wakati mmoja na masufuria yanayotumika kwenye jiko husika ni makubwa. Sinki lenye karai mbili za pembe nne zilizolingana ukubwa linafaa zaidi kwa kuoshea na kusuuzia vyombo hasa kama unaosha kwa mikono. Kwa hivyo unatakiwa kujua ukubwa wa chumba cha jiko lako na jinsi utakavyolitumia sinki lenyewe. Umbo na ukubwa wa sinki ni muhimu, na wakati unapoangalia ukubwa wa sinki tupia jicho kwenye kina chake pia. Kutegemea na matumizi ya jiko, sinki lenye kina kirefu ni bora zaidi kwa kuoshea vyombo na masufuria.

Watengenezaji wanazalisha sinki za jikoni zilizotengenezwa kwa vifaa na mitindo mbali mbali kutoka bati la kung’aa lisiloshika kutu hadi vifaa kadhaa vya kisasa zaidi, anasema Awadh. Pia sinki la jikoni ni mojawapo kati ya kifaa cha bei rahisi kinachojumuika kwenye ujenzi wa jiko. Ingawa kuna masinki ya jikoni za kifahari ya bei kubwa, kuna utajiri wa masinki mengi ya jikoni ya bei nafuu.

Cha muhimu msomaji ni kujipatia sinki imara ambalo halitatikisa bajeti yako. Kwa kuwa sinki hili linauzwa pekee kama lilivyo bila kujumuisha bomba, basi katika hatua itakayofuata utaweza kujichagulia bomba la sinki la jikoni la rangi na staili unayopenda.
Mara unapochagua umbo na ukubwa wa sinki unalotaka kuendana na mahitaji yako, uamuzi wako unaofuata ni kuamua juu ya vifaa mbalimbali vilivyotumika kutengenezea sinki hilo iwe ni bati lisiloshika kutu au enameli. Aina ya kifaa kilichotengenezea sinki utakachochagua kati ya hizi mbili itategemea zaidi na ladha binafsi na mfuko wako.

Masinki ya bati lisiloshika kutu ndio ya kawaida zaidi kwa ajili ya jikoni. Ni gharama nafuu, yanadumu na rangi yake ya silva inaendana sana na vifaa na vyombo vingine vya jikoni. Wakati unanunua sinki la aina hii chagua lile la bati nene kwani litadumu zaidi. Sinki la bati nene limetulia kwa hivyo kupunguza hata kelele za vyombo na kufanya mchakato wa kuandaa chakula kuwa wa kimya kimya.

Usisahau kuzingatia vitu vya ziada ambavyo huenda ukahitaji viwepo kwenye sinki lako la jikoni kwa mfano pampu ya sabuni. Baadhi ya masinki yatakuwa na alama hizo wakati mengine hayana.
Nakutakia uchaguzi mzuri wa sinki lako la jikoni.


Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange.  Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment