Pages

Wednesday, February 19, 2014

NEWS: Serikali yaingiza sokoni nyumba 130

NYUMBA 130 kati ya 851 zilizojengwa Dar es Salaam eneo la Bunju A katika mradi
maalum wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma, zimefikia hatua ya kukamilishwa.
 
Kutokana na mafanikio hayo, Serikali imeuagiza Wakala wa Barabara (Tanroads)
kujenga barabara katika eneo ambalo mradi huo unatekelezwa, ili kuwapunguzia
watumishi wa Serikali gharama.
Gharama za nyumba hizo zinaanzia Sh milioni 30 kwa nyumba ya vyumba vinne vya kulala hadi Sh milioni 140 kwa nyumba za ghorofa.
Mtendaji Mkuu wa Mradi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Elius Mwakalinga amesema
hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli aliyefanya ziara ya ghafla katika eneo hilo.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwakalinga alisema nyumba hizo ni sehemu ya nyumba
1,400 zitakazojengwa Dar es Salaam katika mwaka wa fedha 2013/2014 ukihusisha
ujenzi wa nyumba 2,500 katika mikoa 12 ya Tanzania Bara.
Alisema Wakala umepanga kuanza kuuza nyumba 155 kwa njia ya mkopo ingawa hadi
sasa watumishi 3,000 wameomba kuuziwa nyumba hizo.
“TBA imeandaa vigezo vitakavyozingatiwa kuuziwa nyumba ambavyo ni muda wa
mtumishi kazini, umuhimu wa kazi anayofanya mtumishi kulinganisha na eneo ilipo
nyumba husika, maombi ya muda mrefu na mahitaji ya haraka,” alisema Mwakalinga.

Alisema vigezo vingine ni pamoja na ulemavu, mjane, mgane au familia yenye mzania mmoja, uwezo wa mtumishi kulipa deni lote kwa wakati, malipo ya awali na mtumishi anayekaribia kustaafu na mafao yake yanatosha kulipia nyumba.
Hata hivyo alisema TBA imeanzisha kikosi cha Brigedia ya Ujenzi, ambacho kimeunda vikosi saba vitakavyojenga nyumba ambapo vikosi sita vitajenga nyumba za chini
hadi za ghorofa moja, na kikosi kimoja kitajenga nyumba za ghorofa hadi nane
lengo likiwa ni kukamilisha ujenzi wa nyumba 10,000 zinazotakiwa nchini.
Akizungumza katika ziara hiyo, Magufuli aliitaka TBA kutopandisha ghama za nyumba hizo na ikiwezekana ziendelee kushuka huku akiomba kuangaliwa kwa kodi ya
kuingiza vifaa hivyo vya ujenzi, ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika na kuuzwa kwa gharama stahiki.
Kuhusu ujenzi wa barabara, aliiagiza Tanroads kutumia fedha za Mfuko wa Barabara katika ujenzi wa barabara katika eneo ambalo mradi huo unatekelezwa lengo likiwa ni kuendelea kuwapunguzia mzigo wa gharama watumishi wa Serikali.
“Wakati Tanzania inapata uhuru kulikuwa na nyumba 6,000 peke yake ambazo zilikuwa hazitoshi na hadi sasa suala la makazi ni gumu kwani watu milioni tatu wana
upungufu wa makazi,” alisema Dk Magufuli.

CHANZO: HABARILEO

No comments:

Post a Comment