Pages

Sunday, February 9, 2014

News Zihusuzo Makazi/Nyumba: Wasanii watakiwa kuchangamkia nyumba

MWENYEKITI wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Profesa Penina Mlama ametoa mwito kwa wasanii kuchangamkia kuchangia ujenzi wa nyumba unaoratibiwa na Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) ili kujiandalia makazi.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za wasanii katika kijiji cha Mwanzega, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Profesa Mlama alisema makazi ni sehemu ya maisha ya binadamu hivyo wasidharau mradi huo ni faida kubwa kwao.
Alisema nyumba ambazo ameziona ni nzuri, imara na zinauzwa bei ya chini ambayo huwezi kuzipata sehemu nyingine yoyote nchini na kuongeza kuwa kujenga kwa lengo la kuishi pamoja, kunatoa fursa ya wasanii kubuni njia nyingine ya kuanzisha miradi mbalimbali.
Profesa Mlama alitaka Shiwata isikate tamaa, bali iendelee kuwashawishi wasanii wajiunge na kuchangia ujenzi wa nyumba ili baadaye wasitafute visingizio kuwa hawakupewa fursa hiyo.
Naye Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisifu Shiwata kubuni njia ya kuwasaidia wasanii kupata makazi na kuahidi kuwa baraza hilo litatoa ushirikiano na kutoa ushauri kila unapohitajika.
Mwenyekiti wa Shiwata, Cassim Taalib alisema mpango wa ujenzi wa nyumba za wasanii utaendelea kote nchini na kuwataka wasanii waungane kufanya kazi zao kwa pamoja.
Alisema mpaka sasa nyumba 38 zimekabidhiwa kwa wasanii waliochangia ujenzi katika kijiji cha Mwanzega Mkuranga na nyingine 21 zinatarajiwa kukabidhiwa mwezi ujao.
Shiwata mbali ya kusimamia ujenzi wa nyumba hizo, inasimamia matamasha ya wasanii wachanga, kuendesha makongamano ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya na kutoa elimu na maadili kwa wasanii.
Chanzo cha habari hii ni kutoka magazetini


No comments:

Post a Comment