Pages

Friday, May 30, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kufanana na mazingira yako

Jinsi ya kufanana na mazingira ya nyumbani kwako

Kila mtu anachagua ni vipi anataka mazingira ya nyumbani kwake yawe. Ingawa tunaweza tusijali kuhusu uchaguzi huo lakini mazingira yetu ni dili kubwa kutuhusu. Una nafasi ya kutengeneza mazingira ambayo yatarahisisha maisha yako ama yatayafanya  yazidi kuwa magumu.

Kuna kanuni ya kwanza ya msingi kuwa katika kila kitu kilichopo kwenye eneo linalokuzunguka kina nguvu fulani iwe kitu hicho kina uhai ama hakina. Ni kama watu wa kale walivyoamini kuwa kila kitu kina uhai. Kanuni ya pili ni kuwa kila kitu kwenye mazingira yetu kinahusiana na kitu kingine. Inawezekana kwa mtizamo wa kiroho au wa kisayansi. Na kanuni ya tatu ni kuwa kila kitu kinabadilika kila wakati.

Sasa basi kama kila kitu kwenye mazingira yako kina uhai na kimeunganishwa na wewe basi mabadiliko yakitokea kwenye eneo lako nawe unaguswa. Mazingira yako yanakugusa nawe unayaakisi. Hii ni kama usemi kuwa kila kitu kwenye mazingira yako kinaongea na wewe. Je vitu vya mazingira yako vinasema yale ambayo unapenda kusikia, je vinakusaidia kupata kile unachotaka kupata katika maisha.

Fikiria jinsi unavyoingia nyumbani kwako na kukumbuka usemi kuwa unachokutana nacho mwanzo kinakugusa zaidi . Kama unaingilia varanda iliyojaa makorokoro kila mara unapoingia nyumbani kuna uwezekano mkubwa wa kuchoka hapo hapo nje hata kabla hujafika ndani. Vilevile kama unatembea kuelekea karibia na kizuizi unaanza kujifikiria kuwa inahitaji nguvu kupita pale. Pia kama unafungua mlango wa ofisi asubuhi na kukutana na meza iliyojaa nyaraka, unaweza kujisikia kama siku yako tayari imejaa na hakuna nafasi ya kuanza kitu kipya kwa siku hiyo.

Tembelea kila chumba nyumbani kwako. Je kuna kitu kinakuambia kuwa maisha ni mazuri na yamejaa fursa? Au una picha usiyoipenda, fenicha ambayo haijakaa sawa au rangi ya ukuta ambayo inakupa ukakasi kuitazama? Kila mara unapooana vitu kama hivi, unapotembelea chumba hiki unapata ujumbe hasi. Hata kama akili yako itazoea kuona hivyo lakini dhamira itakuwa inakereka.

Mkusanyiko wa picha unaweza kuwa chanzo cha ujumbe hasi. Hakikisha ni za kumbukumbu na hisia nzuri za watu hao kwako. Zinaweza kuwa ni picha nzuri sana kwa kuonekana kwa macho lakini kama mojawapo inakukumbusha tukio au wakati wa huzuni basi iondoe.  Weka zile zinazokufanya uwe na tabasamu. Watu mara nyingi wana picha kwenye kuta zao kwa sababu tu hawana kitu kingine cha kuweka hapo na sio kwamba ni kwa kuwa wanakipenda kilichopo. Sanaa ukutani inaweza kuwa nzuri sana ila kama ukiitazama haikubariki haina faida kwako. Badala yake inakupa ujumbe hasi na kukunyonya nguvu kila unapoiona. Ni vyema kuiondoa na kuacha nafasi kwa kitu ambacho kinakupa mtizamo chanya katika maisha.

Kuchukua hatua hii mbele zaidi, fikiria ni nini unakipenda kwenye maisha. Mfano mzuri ni mtu anayetaka kuwa na uhusiano. Mara nyingi picha atakazoweka nyumbani kwake na hasa chumba cha kulala ni za akiwa singo. Chumba hicho kitakuwa na taa moja tu ya kivuli na hata kimeza cha kando kimoja. Vyote hivi vinatoa ujumbe kuwa mhusika hana mtu. Badala ya vitu vilivyopo kwenye seti kwa mfano picha yenye watu wawili, na taa mbili za vivuli vinaleta alama za mahusiano.

Mazingira ya mahali unapoishi yanahusika katika kila eneo la maisha yako. Kama unahitaji akili tulivu hakikisha kuwa mazingira yako hayakupi kinyume na matakwa yako kwa kuwa na vitu ambavyo haviko mahali pake. Pia kama unataka kuwa mbunifu zaidi angalia kama je kuna nafasi zaidi ya kuweza kuwa hivyo? Kama unahitaji miundo mbinu safi je njia ya kuendea mlangoni kwako ni wazi, safi na inakaribisha?

Unavyotembea kwenye mazingira ya nyumbani kwako angalia kila kitu kwa jicho la ziada. Ondoa kila kitu ambacho huwezi ukasimama na kushuhudia kuwa unakipenda na ni kitu ungependa kuwa nacho. Unaweza usiwe na kiti kingine cha kuweka kwenye hiyo sehemu ulipotoa kile usichokipenda, lakini kama kinakuletea tukio la huzuni bado,  potelea mbali kitoe tu. Kinaziba kile unachokipenda na pia hicho usichokipenda kinakuletea hisia mbaya. Kwa kuamini utapata kingine unatengeneza uwezekano. Kuwa makini na hivyo vitu vinavyoongea na wewe furaha na kuvipa nafasi ya heshima nyumbani kwako.

Katika nyakati hizi za mihangaiko mingi, ni muhimu kuwa mazingira yako hayakuongezei vikwazo kwenye dunia yako. Hii inahusu hata taarifa za habari kwenye matukio ya mauaji, ajali na mengi ya kutisha. Fuatilia ni nini kiko kwenye vyumba vya watoto. Kama mazingira ya vyumba vyao yanaongea amani, watakua wakiwa wanajifunza amani.

Kwa kuwa makini na kila kitu kwenye mazingira yako unatengeneza makazi ambayo yanafanana na wewe kwa kukupa ujumbe chanya na zenye kukutia nguvu. Kuwa kitu kimoja na makazi yako unakuwa na mtizamo chanya zaidi katika maisha. Mtazamo chaya unagusa kila kitu kwenye maisha yako. Yasikilize mazingitra yako.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Tuesday, May 27, 2014

Thursday, May 22, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kuhifadhi vyombo makabatini

Jinsi ya kupanga vyombo kwenye makabati ya jikoni

Je vyombo vyako vinataka kuporomoka wakati ukifungua makabati ya jikoni? Kama ndivyo basi ni wakati wa kupanga na kuhifadhi upya na makala hii ni sahihi kwako.  Njia bora zaidi ya kupangilia vyombo na vifaa kwenye makabati yako ya jikoni ni kufikiria ni kwa vipi unavitumia vyombo vyenyewe. Ni vyombo na vifaa vipi unajikuta ukivitumia kila siku, na ni vipi vinakaa tu kabatini. Tosa vile ambavyo unaweza kuendesha shughuli zako za hapo jikoni bila kuwa navyo na elekeza nguvu kwenye kufanya makabati yako yaonekane yanafanya kazi, masafi na yana mvuto. Mara utakapopanga ndani ya makabati yako basi utajisikia furaha tena kuingia jikoni.

Ili kuweza kufanikisha zoezi la kuhifadhi vyombo kwa unadhifu kwenye makabati yako ya jikoni kwanza kabisa ondoa kila kitu kwenye makabati. Ni rahisi kuanza mradi wowote wa kupanga upya kwa kuanza na eneo safi, na kwa makabati ya jikoni ni hivyo hivyo. Songa mbele na toa kila kitu kwenye makabati kuanzia sahani, glasi, vikombe, sufuria, vikaangio na kila kitu kingine chochote ulichohifadhi kwenye makabati yako hayo. Panga kila kitu juu ya kaunta zako za jiko au hata kama una meza ya jikoni ili kuweza kutathmini ni nini unacho na ni kipi unahitaji. Kuondoa vile usivyohitaji kutasaidia kuondoa mrundikano hivyo kukuwezesha kuhifadhi vyema vile unavyohitaji. Na kama utajigungua kuwa kuna chombo ama kifaa unakihitaji lakini huna basi hakikisha unakinunua kwanza kabla ya kuweka mpangilio wako. Kama ukisubiri itakuwa ngumu kupata eneo la kukihifadhi baadaye.

Fikiria kugawa vyombo vya zamani na vile usivyohitaji kwa wanaohitaji zaidi, au hata kupeleka kwenye mnada wa vyombo vilivyotumika endapo viko katika hali nzuri. Kufahamu kuwa vifaa vyako vya zamani vinaenda kwenye jiko lingine itakupa amani zaidi ya kuvitupa tu bila mpangilio.

Futa makabati yako ambayo hayana chombo chochote kuanzia juu hadi chini. Tumia sabuni nzuri za kusafishia pamoja na kitambaa cha kufutia na safisha kila mahali hadi kwenye milango yote ile ya mbao na hata kama ya kioo ipo. “Kama utataka kutumia kemikali za kusafishia,tumiavinega iliyochanganywa na maji kidogo,” anasema Bi Mwajuma Issa ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kufanya usafi majumbani.  Kemikali hii ya asili ya kusafishia imefanikiwa sana kwenye makabati ya jikoni ila kama makabati yako yametengenezwa kwa mbao ambayo haijapakwa rangi basi hakikisha unatumia sabuni za kusafishia ambazo hazitaharibu mbao. Kwa namna hii unaweka makabati yako tayari kwa ajili ya mpangilio mpya wa vyomba na vifaa vingine vya hapo jikoni. Kusafisha makabati yako kwa mtindo huu kutaangamiza makazi ya wadudu na kufanya nyombo, vifaa na vyakula utakavyohifadhi humo kuwa freshi.

Nunua vihifadhio vya kukusaidia katika mpangilio wa jikoni kama vile vitrey vinavyotumika kuweka baadhi ya vyakula vikavu kama vitunguu na viungo , kitufe cha visu kwa ajili ya kuhifadhia visu vingi kwa wakati mmoja na pia kurahisiha matumizi na vitu vingine vidogodogo kama vya kuwekea vijiko kadhaa na uma ambazo zinatumika kila siku. Kwa kawaida vihifadhio hivi husimamishwa kwenye kaunta za jiko. Pia makontena kwa ajili ya kuhifadhia vyakula kama mchele, unga na sukari vitakusaidia kuweka mpangilio jikoni

Baada ya kabati kukauka unyevu wote sasa ni wakati wa kutandika karatasi za kwenye makabati ya vyombo kabla ya kupanga vyombo vyako. Sasa una makabati yako yakiwa masafi na yameshatandikwa, ni wakati wa kufikiri ni kwa namna gani unataka kuweka mpangilio wa vyombo unavyotaka kuhifadhi ndani. Tathmini hivyo vyombo na vifaa unavyotaka kuhifadhi. Weka kila chombo kwenye kundi lake kutokana na aina ya chombo. Wakati wa kupanga makabati ya jikoni inaleta mantiki kupanga vyombo vinavyoendana pamoja.

Hifadhi vyombo vya thamani na kuvunjika kwenye kabati za juu ya kaunta ambapo ni ngumu kwa watoto kufungua na kuvunja.
·         Hifadhi pamoja vyombo vya kuvunjika kama vile glasi za kunywea maji, glasi za juisi na glasi nyingine zozote za matumizi ya kila siku.
·         Hifadhi pamoja glasi za mvinyo na shampeni.
·         Hifadhi pamoja sahani zako za kuvunjika na mabakuli. Ila hapa ieleweke vizuri kuwa sio sawa kuweka sahani na mabakuli kwenye mstari mmoja kama njia ya kuhifadhi nafasi kwani inaweza kusababisha kuvunjikiana.
·         Tofautisha sahani na bakuli za matumizi ya kila siku na zile za matumizi ya msimu.
·         Kama makabati yako ya jikoni yana milango ya kioo fikiria ni vyombo vipi ungependa vionekane kwa nje kwani makabati haya ni kwa matumizi na umaridadi.

Hifadhi sufuria na vikaangio kwenye kabati za chini karibia na jiko. Kila mmoja ana jiko la tofauti, lakini kwa mara nyingi makabati ya chini (chini ya kaunta) ndio sahihi kwa sufuria na vikaangio. Vyombo hivi huwa ni vizito na mara nyingi kuokoa nafasi sufuria moja inaingizwa ndani ya nyingine kuendana na ukubwa kwa hivyo inaleta mantiki kuvihifadhi eneo ambalo haitakuwa na haja ya kuvitoa tokea juu. Zile sufuria na vikaangio unavotumia mara kwa mara viweke karibia na mlango ili kuchukua kirahisi na zile ambazo unatumia kwa nadra zihifadhi mwishoni  mwa makabati. Pia unaweza kuona ni rahisi kuhifadhi sufuria na vikaangio vya kutumika mara kwa mara kwenye raki yake inayoning’inizwa ukutani mbele ya makabati yako. Hii inasaidia kuning’iniza kila moja peke yake badala ya kubebana.

Panga vijiko, uma na visu vya ziada kwenye droo flati,ukiwa umegawanyisha kila kimoja kwenye mahali pake. Vile vinavyotumika mara kwa mara hifadhi kwenye kihifadhio cha vijiko na uma kilichowekwa juu ya kaunta na kitufe cha visu. Pia weka droo moja la flati kwa ajili ya kuhifadhi vitambaa na vitaulo vya kufutia vyombo.

Tafuta eneo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa kama blenda na tosta ambapo vile ambavyo unatumia kila siku waweza hifadhi juu ya kaunta. Kama blenda ni ya juisi ambayo inatumika mara chache kwa juma basi hifadhi kwenye kabati

Hifadhi sabuni na vifaa vya kusafishia ndani ya kabati lililo chini ya sinki.

Sasa umemaliza kuhifadhi vyombo kwenye kabati zako za jikoni, zicheki mara kwa mara kuhakikisha kuwa bado vyombo na vifaa vyako vipo kwenye mpangilio uliochagua. Unaweza kuwa unaweka vidonge vya kuua wadudu kama mende mara moja kila baada ya miezi sita.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Sunday, May 18, 2014

super sunday...

maisha ni haya haya wajameni...ha ha haaa...tuendako baada ya hapa hakuna uzoefu kwa hivyo enjoy hapa hapa kwa sana kadri uwezavyo.....




Tuesday, May 13, 2014

pilika mitaani nikakutana na showroom iliyonitumbuiza..

showroom ilinivutia nikapiga picha kwenye hii dressing table.
imetengenezwa kwa mdf ila miguu ni mkongo

ki kiti cha dressing table
TV cabinet

Sunday, May 11, 2014

happy mothers day from my son

wala sikuwa aware...kesho shule nikamwambia mtu wangu mdogo do your homework..nikashangaa ananitolea na kikadi cha mothers day...shule hizi...nami nasema happy mothers kwa wamama wote wasomaji wangu... 


Friday, May 9, 2014

Thursday, May 8, 2014

my article for newspaper: mpangilio wa chumba cha kulala cha wakuu wa familia

Huenda wewe na mwenza wako mnaishi maisha yenye kazi nyingi (busy) ambayo mara nyingi yanapingana na kuwa na muda mzuri wa kukaa pamoja. Hakika mnajua hisia zenu zinavyokuwa kwa ajili ya kukosa muda huo muhimu. Ndio maana ni vyema kuwa na chumba cha kulala ambacho mkiwa pamoja kama wanandoa itawezekana kufurahia ule muda mchache mnaokuwa pamoja. Kwa lengo la makala hii chumba cha wakuu wa familia ni kile cha  baba na mama wa familia – ni koloni lao hapo nyumbani kama wengine wanavyoweza kusema. Wazazi mkiwa ndio nguzo ya familia basi mnahitaji chumba cha kipekee. Mnaokaa kwenye chumba hiki ndio mnaolipa bili na kufanya kazi kwa bidii ili mfanikiwe katika hilo. Kwa nini chumba chenu kisiwe maalumu? Wakuu wa familia mnastahili chumba hiki!

Je wewe mkuu wa familia unakipenda chumba chako cha kulala? Chumba hiki kiwe kama mahali patakatifu kwa wanandoa au yeyote anayelala mule. Chumba kiheshimiwe kisiwe ni ofisi ya nyumbani. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni sehemu ya kupumzika hivyo vitu kama kompyuta havina nafasi kwenye chumba hiki. Ni nini cha kwanza unachokiona mara baada ya kufungua mlango wa chumba hiki, na ni nini unachokiona cha kwanza mara baada ya kufungua macho asubuhi. Chumba hiki kiwe ni sehemu huru pasipo na usumbufu kama wa kufua, ndoo za maji, kompyuta au midoli ya watoto. Chumba hiki sio stoo!                          

Midoli imekuwa ni tatizo kwenye chumba cha kulala hasa kwa wazazi wanaokimbia mchakamchaka wa maisha ya kila siku. Midoli inaishia chumba cha wazazi na hata kitandani.  Kuwa wazi  na kuweka mipaka juu ya chumba hiki na hata midoli ya watoto isijazane chumbani kwako na kitandani. Kwa ujumla watoto wawe na sehemu ya kucheza na kuweka midoli yao. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni cha watu wazima ndani ya familia.

Fenicha kuu kwenye chumba hiki ni kitanda. Kimsingi, kitanda kina lengo moja kuu: kufagilia usingizi wenye afya. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia kinahitaji kitanda chenye kukidhi vigezo vya usingizi bora. Kama matangazo tuseme ya magodoro yanavyoonyesha ni kuwa tunatumia theluthi moja ya maisha yetu kulala. Sasa kwa nini godoro, malazi na fremu ya kitanda visiwe maalumu. Kuna njia nyingi ya kupata kitanda bora kwa bajeti yeyote. Kitanda chenye fremu ya chuma tuu kilichosogezwa karibia na ukuta hakikidhi vigezo. Kila kitanda kinahitaji bodi la kichwani (makala zijazo tutaongelea umuhimu wa bodi hili) ambayo yanapatikana kwa saizi na mitindo mbalimbali.

Kwa kuwa msisitizo wa chumba hiki ni kwa wanandoa,  kama kuna sehemu kubwa weka sofa au viti viwili vya kukalia badala ya kimoja. Mara zote fikiria vitu viwili viwili. Kama wewe ni mwanaume au mwanamke uliye singo lakini ndio mkuu wa familia weka picha ya peke yako kusisitiza utambulisho wako kuwa huna mtu. Kama mnaolala humo mko kwenye mahusiano basi mambo ni kwa seti kama vile taa za vivuli mbili, vimeza vya kando viwili na hata kama mishumaa basi miwili.  Kumbuka unatengeneza mandhari ya kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo wa siku nzima. 

Chagua sanaa inayoelezea uhusiano wenu iwe ni picha ya ngalawa, ndege au hata maneno ya kimahaba. Sio sawa kuweka picha za marafiki, mababu na hata wanafamilia wengine kwenye chumba hiki. Tatizo ni kuwa chumba kinaanza kuonekana kinguvu kimezidiwa na vitu. Watu wote hawa wana haja gani chumbani kwako. Pambeni chumba cha kulala kwa picha zenu nyie wanandoa mnaolala humo.
Chumba hiki kamwe kisiwe na mrundikano, weka kero za maisha ya kila siku mbali na mahali hapa patakatifu. Kama kabati lako la nguo limefurika, punguza ubakize zile ambazo haswa unazivaa. Pia fikiria kupunguza kiasi cha fenicha ili kuwe na nafasi chumba kisionekane kusongamana. Sakafu ionekane peupe isijazane vitu.  

Zingatia kile unachokiona kwanza mara baada ya kuingia chumba chako cha kulala. Kanuni inasema kuwa mlango usiwe usawa mmoja na kitanda, kwa maana ya kuwa ukiwa umelala kitandani uuone mkango lakini ukifungua mlango macho yasione kitanda moja kwa moja. Mlango ukiwa namna hii unawapa walalaji kujiamini zaidi kuwa wanamiliki chumba na usingizi unakuwa mwororo.
Vifaa vya umeme leo hii ni changamoto kwenye chumba cha kulala. Kompyuta, luninga na vifaa vingine vya umeme vinatuzunguka na kutunyonya nguvu kwa  kuleta nguvu ya uvutano mithili ya sumaku ambayo baadaye inaleta msongo wa mawazo. Ili kupumzisha mwili na kuuweka katika afya njema basi ni vyema kuwa mbali na vifaa vya umeme katika chumba cha kulala. Kama hamna jinsi kuwa ni lazima vifaa hivi viwepo chumbani basi sio tu vizime na kuacha vijitaa vinawaka bali chomoa kabisa kwenye umeme wakati wa kulala.

Kumbuka kuwa kila kitu kwenye nyumba tunazoishi kinatupa ujumbe. Chumba chako cha kulala wewe mkuu wa familia kinakupa ujumbe gani? Je kinakukumbusha majukumu yote unayohitajika kukamilisha au kinakupa hisia za utulivu na kukukaribisha kupumzika? Je kinakushawishi kuwasha luninga au kinakuleta kwenye faragha? Je kinaongeza msongo wa mawazo kwenye maisha yako? Au kinakupa pumziko la nafsi hata kama uko singo? Kama ndio basi umeweka mpangilio wa chumba cha kulala ambacho ni kama mahali patakatifu.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Wednesday, May 7, 2014

nukuu: kasheshe homa ya dengue...

“Kwa ufupi, mbu sasa ni hatari kuliko ilivyokuwa awali kwa sababu hawa wanaoambukiza homa ya dengue huuma wakati wa mchana, tofauti na wale wanaoambukiza malaria ambao huuma usiku na watu walikwishajua kujikinga kwa chandarua au dawa,


Friday, May 2, 2014