Pages

Thursday, May 22, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kuhifadhi vyombo makabatini

Jinsi ya kupanga vyombo kwenye makabati ya jikoni

Je vyombo vyako vinataka kuporomoka wakati ukifungua makabati ya jikoni? Kama ndivyo basi ni wakati wa kupanga na kuhifadhi upya na makala hii ni sahihi kwako.  Njia bora zaidi ya kupangilia vyombo na vifaa kwenye makabati yako ya jikoni ni kufikiria ni kwa vipi unavitumia vyombo vyenyewe. Ni vyombo na vifaa vipi unajikuta ukivitumia kila siku, na ni vipi vinakaa tu kabatini. Tosa vile ambavyo unaweza kuendesha shughuli zako za hapo jikoni bila kuwa navyo na elekeza nguvu kwenye kufanya makabati yako yaonekane yanafanya kazi, masafi na yana mvuto. Mara utakapopanga ndani ya makabati yako basi utajisikia furaha tena kuingia jikoni.

Ili kuweza kufanikisha zoezi la kuhifadhi vyombo kwa unadhifu kwenye makabati yako ya jikoni kwanza kabisa ondoa kila kitu kwenye makabati. Ni rahisi kuanza mradi wowote wa kupanga upya kwa kuanza na eneo safi, na kwa makabati ya jikoni ni hivyo hivyo. Songa mbele na toa kila kitu kwenye makabati kuanzia sahani, glasi, vikombe, sufuria, vikaangio na kila kitu kingine chochote ulichohifadhi kwenye makabati yako hayo. Panga kila kitu juu ya kaunta zako za jiko au hata kama una meza ya jikoni ili kuweza kutathmini ni nini unacho na ni kipi unahitaji. Kuondoa vile usivyohitaji kutasaidia kuondoa mrundikano hivyo kukuwezesha kuhifadhi vyema vile unavyohitaji. Na kama utajigungua kuwa kuna chombo ama kifaa unakihitaji lakini huna basi hakikisha unakinunua kwanza kabla ya kuweka mpangilio wako. Kama ukisubiri itakuwa ngumu kupata eneo la kukihifadhi baadaye.

Fikiria kugawa vyombo vya zamani na vile usivyohitaji kwa wanaohitaji zaidi, au hata kupeleka kwenye mnada wa vyombo vilivyotumika endapo viko katika hali nzuri. Kufahamu kuwa vifaa vyako vya zamani vinaenda kwenye jiko lingine itakupa amani zaidi ya kuvitupa tu bila mpangilio.

Futa makabati yako ambayo hayana chombo chochote kuanzia juu hadi chini. Tumia sabuni nzuri za kusafishia pamoja na kitambaa cha kufutia na safisha kila mahali hadi kwenye milango yote ile ya mbao na hata kama ya kioo ipo. “Kama utataka kutumia kemikali za kusafishia,tumiavinega iliyochanganywa na maji kidogo,” anasema Bi Mwajuma Issa ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kufanya usafi majumbani.  Kemikali hii ya asili ya kusafishia imefanikiwa sana kwenye makabati ya jikoni ila kama makabati yako yametengenezwa kwa mbao ambayo haijapakwa rangi basi hakikisha unatumia sabuni za kusafishia ambazo hazitaharibu mbao. Kwa namna hii unaweka makabati yako tayari kwa ajili ya mpangilio mpya wa vyomba na vifaa vingine vya hapo jikoni. Kusafisha makabati yako kwa mtindo huu kutaangamiza makazi ya wadudu na kufanya nyombo, vifaa na vyakula utakavyohifadhi humo kuwa freshi.

Nunua vihifadhio vya kukusaidia katika mpangilio wa jikoni kama vile vitrey vinavyotumika kuweka baadhi ya vyakula vikavu kama vitunguu na viungo , kitufe cha visu kwa ajili ya kuhifadhia visu vingi kwa wakati mmoja na pia kurahisiha matumizi na vitu vingine vidogodogo kama vya kuwekea vijiko kadhaa na uma ambazo zinatumika kila siku. Kwa kawaida vihifadhio hivi husimamishwa kwenye kaunta za jiko. Pia makontena kwa ajili ya kuhifadhia vyakula kama mchele, unga na sukari vitakusaidia kuweka mpangilio jikoni

Baada ya kabati kukauka unyevu wote sasa ni wakati wa kutandika karatasi za kwenye makabati ya vyombo kabla ya kupanga vyombo vyako. Sasa una makabati yako yakiwa masafi na yameshatandikwa, ni wakati wa kufikiri ni kwa namna gani unataka kuweka mpangilio wa vyombo unavyotaka kuhifadhi ndani. Tathmini hivyo vyombo na vifaa unavyotaka kuhifadhi. Weka kila chombo kwenye kundi lake kutokana na aina ya chombo. Wakati wa kupanga makabati ya jikoni inaleta mantiki kupanga vyombo vinavyoendana pamoja.

Hifadhi vyombo vya thamani na kuvunjika kwenye kabati za juu ya kaunta ambapo ni ngumu kwa watoto kufungua na kuvunja.
·         Hifadhi pamoja vyombo vya kuvunjika kama vile glasi za kunywea maji, glasi za juisi na glasi nyingine zozote za matumizi ya kila siku.
·         Hifadhi pamoja glasi za mvinyo na shampeni.
·         Hifadhi pamoja sahani zako za kuvunjika na mabakuli. Ila hapa ieleweke vizuri kuwa sio sawa kuweka sahani na mabakuli kwenye mstari mmoja kama njia ya kuhifadhi nafasi kwani inaweza kusababisha kuvunjikiana.
·         Tofautisha sahani na bakuli za matumizi ya kila siku na zile za matumizi ya msimu.
·         Kama makabati yako ya jikoni yana milango ya kioo fikiria ni vyombo vipi ungependa vionekane kwa nje kwani makabati haya ni kwa matumizi na umaridadi.

Hifadhi sufuria na vikaangio kwenye kabati za chini karibia na jiko. Kila mmoja ana jiko la tofauti, lakini kwa mara nyingi makabati ya chini (chini ya kaunta) ndio sahihi kwa sufuria na vikaangio. Vyombo hivi huwa ni vizito na mara nyingi kuokoa nafasi sufuria moja inaingizwa ndani ya nyingine kuendana na ukubwa kwa hivyo inaleta mantiki kuvihifadhi eneo ambalo haitakuwa na haja ya kuvitoa tokea juu. Zile sufuria na vikaangio unavotumia mara kwa mara viweke karibia na mlango ili kuchukua kirahisi na zile ambazo unatumia kwa nadra zihifadhi mwishoni  mwa makabati. Pia unaweza kuona ni rahisi kuhifadhi sufuria na vikaangio vya kutumika mara kwa mara kwenye raki yake inayoning’inizwa ukutani mbele ya makabati yako. Hii inasaidia kuning’iniza kila moja peke yake badala ya kubebana.

Panga vijiko, uma na visu vya ziada kwenye droo flati,ukiwa umegawanyisha kila kimoja kwenye mahali pake. Vile vinavyotumika mara kwa mara hifadhi kwenye kihifadhio cha vijiko na uma kilichowekwa juu ya kaunta na kitufe cha visu. Pia weka droo moja la flati kwa ajili ya kuhifadhi vitambaa na vitaulo vya kufutia vyombo.

Tafuta eneo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa kama blenda na tosta ambapo vile ambavyo unatumia kila siku waweza hifadhi juu ya kaunta. Kama blenda ni ya juisi ambayo inatumika mara chache kwa juma basi hifadhi kwenye kabati

Hifadhi sabuni na vifaa vya kusafishia ndani ya kabati lililo chini ya sinki.

Sasa umemaliza kuhifadhi vyombo kwenye kabati zako za jikoni, zicheki mara kwa mara kuhakikisha kuwa bado vyombo na vifaa vyako vipo kwenye mpangilio uliochagua. Unaweza kuwa unaweka vidonge vya kuua wadudu kama mende mara moja kila baada ya miezi sita.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment