Pages

Thursday, July 24, 2014

my article for newspaper: mpangilio wa chumba cha kulala

Chumba chako cha kulala ni sehemu ambayo unalala, kwahivyo ni muhimu pawe katika mazingira ya kupumzikia. Wakati huohuo unataka pawe eneo la kufanyia shughuli mbalimbali zinazotakikana kufanyikia hapo kwa mfano kujiandaa kwa ajili ya kutoka asubuhi. Jinsi ambavyo fenicha zimepangwa italeta matokeo chanya au hasi kwa mazingira ya chumba chako cha kulala. Kitanda ni fenicha nambari moja kwa chumba chochote cha kulala na kwa asili ndio kitovu cha jicho linakotazama.

Vyumba vya kulala vinavyotumika na watu wa kundi fulani vina mahitaji ya kipekee kwa kundi hilo. Iwe unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia, cha mgeni au cha watoto makala hii itakupa dondoo za jinsi unavyoweza kupangilia.

Iwapo unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia (kumbuka kuwa chumba hiki sio lazima kiwe ni kikubwa zaidi kama wengi wanavyodhani) kinachotakiwa tu ni kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika mule. Na kama chumba chako ni kidogo zaidi ya ambavyo ungependa, fikiria mbinu za kukifanya kiwe kikubwa kama vile kuondoa mrundikano na kuweka fenicha, pazia na malazi yenye rangi za mwanga kwani zinafanya chumba kionekane kikubwa.

Tukiachana na ukubwa wa chumba cha kulala cha wakuu wa familia, dondoo hizi zitakusaidia kukifanya kiwe sehemu bora zaidi ya mapumziko. Weka vimeza vya pembeni mwa kitanda vyenye ukubwa wa kuendana na eneo lako. Kama unatazama luninga ukiwa kitandani utagundua kuwa vimeza hivi vitakusaidia. Tafuta eneo japo kwa kiti kimoja au viwili vya kukalia. Viti vinasaidia sana siku ya ugonjwa, kupumzika mchana au wakati wa kusoma. Fikiria kuweka zulia sakafu yote ya chumba hiki ili kuondoa kelele za fenicha na nyayo kwenye chumba. Kama una nafasi si mbaya kuweka deski kwa ajili ya kukaa na kuandika chochote.

Kwa upande wa watoto wanaoingia kwenye rika la ujana huwa wanajua ni nini wanachotaka kwenye chumba chao cha kulala, na hawachelewi kukuambia wewe mzazi au mlezi wanahitaji sehemu ya kuhifadhia vitabu na muziki ama eneo lao lingine la kuhifadhia vitu vyao vingine vyovyote unavyoweza kudhani.Wana mawazo yao kuhusu mpangilio na rangi, kwa hiyo waulize!

Pilika nyingi zaidi ya kuperuzi mitandao na burudani zinafanyika kwenye chumba cha kulala cha watoto wa rika hili la kuingia kwenye ujana. Viti vya ziada na vimeza vitawezesha eneo la wageni wao. Weka fenicha zitakazotumika na rahisi kutunza.

Vyumba vya kulala vya watoto wadogo viwekwe fenicha kwa kufikiria miaka yao ijayo. Ila mwanzoni, hakikisha unaweka eneo la kuwabadilishia karibia na kitanda. Kwenye chumba hiki hakikisha usalama unapewa kipaumbele. Usiweke kitanda karibia na dirisha kama dirisha hilo linafunguliwa mara kwa mara. Mara nyingi kuweka kitanda katikati kama chumba kina nafasi kubwa huwa ndio mpangilio mzuri zaidi.  Ila kama nyumba yako ina viyoyozi na madirisha hayahitajiki kufunguliwa basi unaweza kuweka kitanda chini ya dirisha.

Hakikisha mtoto hawezi kuanguka toka kitandani. Hakikisha droo za chumba hiki ni laini kufunga, kwa mfano endapo mtoto atakuwa amefungua kwa bahati mbaya basi reli zitateleza zenyewe na droo kufunga. Zikiwa ni droo ngumu kufunga mtoto anaweza akanyanuka droo ikiwa wazi na kona yake ikamtoboa kichwani. Vitasa vya milango na mikono ya makabati visiwe na ncha kali kwenye chumba hiki. Ikiwezekana funika swichi za umeme na nyaya zisisambae sakafuni.

Kuwa na chumba cha mgeni kunamfanya mgeni wako kuwa huru zaidi ugenini na hata wewe mwenyeji wake. Unaweza kupanga chumba cha kulala cha mgeni kwa kitanda sahihi na vifaa vinavyohitajika na kukisahau. Hakikisha kuwa mgeni wako ana sehemu ya kutosha ya kuhifadhia, seti mbili za shuka, mito na komfota au kava la duveti.

Kwa kufanya haya utakuwa umeweka mpangilio wa kufaa kwa kila chumba cha kulala kwa watu wa kada mbalimbali walioko ndani ya familia yako.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment