Pages

Thursday, September 18, 2014

my article for newspaper: vifaa vya msingi jiko dogo la kisasa


Huenda pengine ndio unaanza maisha ya kujitegemea au ya ndoa, unahitaji kuwa na vifaa vya msingi jikoni vya kuanzia kwa miezi michache ya mwanzo—hata miaka michache. Au labda ni mzazi unayetaka kumsaidia huyo kijana wako, binti au rafiki namna ya kuanza maisha. Pia kama ni bibi harusi mtarajiwa makala hii inakuhusu. Nimefanya kazi kubwa ya kutafiti katika maduka ya vifaa vya jikoni na kukuandalia orodha ya vifaa vya msingi kabisa vinavyotakiwa kuwepo jikoni kwa ajili ya kukuwezesha kuandaa chakula katika maisha yako hayo mapya.

Nia hapa ni kuonyesha orodha ya vifaa vya kawaida kabisa vya msingi vya jiko dogo la kisasa.
Ni rahisi kuangukia kwenye ushawishi wa muonekano lakini kitu kimoja cha kujua kwa kweli ni kuwa hauna haja ya kuvunja benki ili kuwa na vifaa vya jikoni vya kiwango.  Orodha hii ya vifaa vya msingi jikoni inaweza kubadilika kutokana na hitaji la mhusika. Pia vyombo vya mezani kama vile sahani vijiko na glasi vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi na kwa sababu hiyo sijaviorodhesha hapa. Kwa hivyo vifaa vya msingi vya jiko dogo la kisasa ni kama vifuatavyo:

Visu

Kisu kikali cha mpishi ni moja kati ya vifaa muhimu zaidi jikoni, na kama utanunua kilicho sahihi kitatumika kwa miaka mingi. Nunua visu vya jikoni ambavyo havishiki kutu.

Ubao wa kukatia

Ubao sahihi wa kukatia utafanya visu vyako vidumu, na rahisi kusafishika. Kuna aina nyingi za mbao hizi kama vile plastiki, miti na hata glasi.

Kifungulia chupa na makopo (opener)

Nunua ambayo unaweza kufungulia chupa na makopo ya aina tofauti tofauti. Nzuri ni ile iliyo rahisi kwa matumizi.

Kisaga vyakula (Blender)

Kama kawaida nunua ambayo ni rahisi kutumia na yenye kazi nyingi tofauti ambapo utaweza kusaga vyakula vyako na kutengeneza juisi.

Vikaangio na masufuria

Iwe uko singo au ni wanandoa wapya kwa kuanzia unahitaji vikaangio japo viwili na sufuria nne hadi sita. Sokoni vikaangio na sufuria zipo zilizotengenezwa kwa material nyingi mno. Nunua ambazo hazing’ang’aniani na chakula (nonstick).
Stovu
Watengenezaji wengi wameunganisha stovu na tanuri ukinunua mbayo unaweza kutumia nishati zaidi ya moja itakuwa ni busara zaidi.

Jokofu
Kwa maeneo mengi ya nchi yetu walau inahitajika kuwa na jokofu kwa ajili ya kuhifadhia chakula kisiharibike. Kwa kuanzia si mbaya ukawa nalo dogo kwenye jiko lako hili la kuanzia maisha.

Kipasha chakula (Microwave)
Hiki kinafanya kazi kubwa ya kupashia na hata kupikia baadhi vya vyakula. Habari njema ni kuwa zipo za bei rahisi kabisa. Ni rahisi kutumia na wengi wanapendelea kuziweka juu ya kaunta ya jiko. Huna haja tena ya kupashia chakula kwenye sufuria.

Kikausha mikate (Toaster)

Hiki nacho kwa wengi wanaopendelea kula mikate iliyokaushwa huwa wanakiweka juu ya kauta.
Mabakuli/Vikontena
Wanasema mapishi ni sanaa, sio? Kuwa na mabakuli na vikontena ndani ya jiko lako la kuanzia maisha vitakusaidia katika maandalizi ya mapishi na hata vikontena vitakusaidia kupashia na pia kuhifadhia vyakula kwenye jokofu.

Kindoo cha uchafu
Unapoandaa chakula na kuosha vyombo lazima utahitaji hiki kindoo kwa ajili ya kuwekea uchafu. Ni muhimu kiwe kile cha mfuniko wa kujifunga chenyewe.
Jiko lenye vifaa vya msingi vinavyopaswa kuwepo jikoni ni rafiki kwa mpishi. Unapokuwa na vifaa sahihi na unajua jinsi ya kuvitumia, unaweza kuelekeza akili yako kwenye chakula unachoandaa. Kama nilivyosema awali vifaa hivi vinaweza kuongezeka kutegemea na mhusika na mazingira unaweza kuwa na vifaa hivi vya msingi jikoni kwa kuanzia na baadaye ukaongeza kidogo kidogo kwa kadri ya mahitaji yako. Mpishi mzuri anatumia vifaa tofauti tofauti na mwishoni anapata vile hasa anavyohitaji.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment