Pages

Thursday, November 6, 2014

my article for newspaper: fenicha za kwenye bustani na varanda

Zingatia haya kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba


Fenicha za nje ya nyumba pia zinajulikana kama fenicha za kwenye bustani au varanda.  Aina hii ya fenicha huwa imetengenezwa kwa malighafi inayozuia maji kupenya, kwa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya nje. Fenicha za  nje ya nyumba zimekuwa zikitumika toka enzi za himaya ya Roma.

Fenicha za nje ya nyumba  ni muhimu kwa mikutano wakati unapokuwa na kikundi cha watu kwa ajili ya siku maalum kama vile siku ya kuzaliwa na kadhalika. Hakuna kinachofurahisha zaidi kama kuwa na kiusingizi kwenye upepo mwanana wa kwenye varanda au bustani. Kuwa na chakula cha usiku na mwenzi wako wakati nyota ziking’aa angani inakuwa ni mahaba zaidi ya ndani ya nyumba.

Ila kuna jambo linalofanya aina hii ya fenicha kuwa tofauti na zile za ndani; malighafi ya fenicha za nje ya nyumba ni lazima iwe imara kwa sababu fenicha zitapambana na mvua kubwa, jua kali, upepo na baridi kali. Je hali ya hewa ya unapoishi ni joto na ukame, au unaishi karibia na pwani? Mvua ni za mara kwa mara? Haya yote ni maswali muhimu ya kupatikana majibu kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba. Hapa ni sababu, hali ya joto na ukame inafanya mbao kupasuka. Upepo mkali unaweza kufanya fenicha za aluminiam zipeperushwe.

Ndio maana ni muhimu sana kuhakikisha kuwa fenicha unazotumia kwenye mazingira ya nje ya nyumba ni sahihi kwa matumizi hayo.

Kwa malighafi, fenicha nyingi za kutumia nje ya nyumba zimetengenezwa kwa plastiki, mbao aluminiam na chuma cha pua. Amua ni malighafi ya aina gani unataka kwa ajili ya fenicha zako za nje. Vitu vitatu ambavyo vitakusaidia kuamua ni hali ya hewa, utunzaji na muonekano. Baadhi ya malighafi kama vile aluminiam hazihitaji utunzaji wa kina. Chuma cha pua kinaweza kudumu kwa muda mrefu sana na kinamudu joto na unyevu. Hapa ni muhimu kufahamu kuwa fenicha za nje za mbao sio imara kama nyingine, kwa hivyo inatakiwa kuziweka dawa mara kwa mara, anasema mseremala Rajab Hamis.Bottom of Form

Fenicha za nje ya nyumba zinakusaidia kuongeza ukubwa wa makazi yako, unapata eneo zaidi la kupumzika hasa wakati ule ambao jua sio kali sana au mvua sio nyingi. Kwa hivyo fenicha hizi zinakamilisha ahadi ya mapumziko, burudani na raha kwa ujumla. Uchaguzi wa fenicha za nje unazingatia hatua zilezile za kununua fenicha za ndani. Japo kunahitajika umakini wa ziada kwa ajili ya tofauti  kati ya fenicha hizi mbili.

Fikiria ni eneo kiasi gani ulilonalo na lina umbo la namna gani. Je ni varanda ndefu na nyembamba au ni fupi pana? Tumia eneo na umbo la varanda au bustani yako kufahamu ukubwa wa fenicha zako za nje. Hakikisha unaacha nafasi ya kutosha kati ya fenicha zako ili uweze kupishana kirahisi. Tumia utaratibu ule ule wa kupanga fenicha za ndani. Kwa eneo dogo meza za ukubwa wa kwenye mgahawa na stuli zitafaa zaidi kwani zitachukua nafasi ndogo.

Ni wapi utakapoweka fenicha zako za nje, je kwenye bustani yako kuna eneo la kukaa ambalo lina paa? Na pia je fenicha zako zitakaa juu ya sakafu laini ya udongo na majani au zitakaa juu ya sakafu ngumu? Hii itakusaidia kuchagua malighafi ambayo itaoana na mazingira yako.

Hakikisha kuwa ukikalia fenicha zako unapumzika vyema. Hata kama viti haviji na mito unaweza kutengenezesha mito yako mwenyewe na uwe unaihifadhi ndani majira ambayo hutumii fenicha za nje. Jaribu fenicha za nje kabla ya kununua na hata kuzilaza kwa jinsi ambayo ungetaka viwe kama vitanda vya mchana.

Yote hayo yakiwa yameshasemwa bajeti yako ndio itaamua ni nini unachoweza kununua. Siwezi nikasisitiza ni kwa namna gani ni muhimu kununua fenicha imara zaidi unazoweza kumudu. Kama uchumi unagomba, bado kuna namna unayoweza kupata fenicha za nje zilizo imara kwa hela uliyonayo. Unaweza kupata fenicha za nje nzuri na imara kwa bei nafuu kabisa kwa kununua zile zilizotumika. Fenicha zinazouzwa kwenye minada ya wafanyakazi wa kimataifa wanaomaliza muda wao na hivyo kurejea kwao, ukizifanyia maboresho kidogo na kuzisafisha zinaonekana kama mpya, na huwa hizi zinakuwa na ubora unaokubalika. Unaweza pia kufikiria kubadilisha mito na makusheni kwa ajili ya kuhuisha fenicha za nje za zamani.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment