Pages

Thursday, November 13, 2014

my article for newspaper: vioo vya mapambo

Boresha muonekano wa ndani ya nyumba kwa kuweka vioo vya mapambo.

Vioo vina kitu kwakweli ambacho ni maalum ndani yake. Vinakusaidia kukujulisha unaonekanaje na pia kukuwezesha kujiweka jinsi ambayo unataka uonekane. Zaidi ya haya maandalizi binafsi na kujiridhisha na muonekano wako kabla hujatoka, vioo vinasaidia pia kwenye kupamba ndani na hivyo kufanya muonekano wa nyumba kuwa maridadi na nadhifu zaidi kwa kila mgeni anayekutembelea.

Kama kuna pambo la ndani ambalo wenye nyumba hatakiwi kulikosa, basi ni kioo. Havitumiki tu kujiangalia unapoingia, bali vina mahadhi yake kwenye kuongeza staili ya chumba au muonekano wa kupagawisha kwa kumfanya mgeni kuduwaa. Sababu nyingine kuu hapa ni kuwa vioo vinaweza kuwa  na bajeti rafiki. Ni kweli kuwa kuna vioo ambavyo ni lazima viwepo nyumbani kwa matumizi kuwa watu wanahitaji ili kuhakikisha kuwa wanaonekana jinsi wanavyotaka kuonekana, lakini leo kwenye makala hii tunaongelea vioo kama mapambo ambavyo unaweka kwenye ukuta wa nyumba yako ili kuongeza staili na ukubwa.

Utagundua kuwa leo, sokoni kuna aina nyingi na tofauti za miundo na aina za vioo. Watengenezeaji wa vioo vya mapambo wanakuja juu kwa kuongeza ubunifu hasa wa fremu wanazofungia vioo hivi. Unaweza kuvipata vioo hivi vikiwa kwenye fremu ya kila malighafi unayohitaji kwa mandhari unaotaka kutengeneza.
Fremu nayo ni kigezo muhimu cha kioo kuwa kifaa cha mapambo. Unaweza kuagiza kioo kwa umbo unalotaka kwa mfano unaweza kuwa na kioo kwenye ukuta wa sebule ambacho kinatoa sura kwenye taswira nne kwa jinsi ambayo ukijitazama unaona uso nne zinazofanana.. Haijalishi staili unayotaka au bajeti uliyonayo, kuna uhakika wa kupata kioo ambacho ni sahihi kwa mradi wako.

Sababu ya kuweka vioo hivi ndani ya nyumba ni ukweli rahisi kuwa unataka kutumia ile hali ya kujiona ndani ya kioo kwa faida ya kimapambo. Baadhi wananunua vioo na kuvitundika kama sanaa nyingine za ukutani, kwa maana ya kuwa wanakitundika katikati ya picha na fremu nyingine, au wanakiweka kwenye ukuta ambao hauna kitu kingine ambacho kingefaa hapo. Hata hivyo unaweza kutumia vioo vya mapambo kuakisi mwanga na vifaa. Kwa mfano unaweza kuwa na ujia (corridor) ambao una mlango upande mmoja lakini mwingine hauna. Pambo lako hapo linaweza kuwa mmea wa kijani (uwe hai au mfu) pale kwenye ukuta usiokuwa na mlango pamoja na kioo. Kioo kitauakisi ujia kwa kuukuza uonekane mpana na mrefu. Kupamba kwa vioo kunafanya eneo dogo lionekane kubwa na mbinu hii inatumika na wataalam wengi wa ubunifu wa ndani nyumba.

Kupamba kwa vioo kunaongeza mwanga wa chumba. Chumba kilichopakwa rangi ya giza kinaweza kuonekana kidogo, kuongeza vioo kwenye kuta zake kutaboresha mwanga. Njia sahihi zaidi ya kuongeza mwanga wa jua bila kuongeza taa ni kufunga vioo vitazamane na madirisha. Vioo vinadaka mwanga wa jua toka dirishani na kuusambaza chumba kizima. Hii inaweza kuwa njia mojawapo pia ya kubana matumizi badala ya kuwasha taa mchana.

Kupamba kwa vioo vya mapambo hakuhitaji mtaalam. Mtu akiwa na vifaa vya toolbox anaweza kufunga vioo ukutani  na kutengeneza chumba chenye muonekano mzuri kwa gharama nafuu.
Chagua vioo vyenye maumbo ya kuvutia, pembe nne ni nzuri ila vioo vyenye maumbo yasiyozoeleka vinafanya umaridadi zaidi. Tafiti aina na maumbo mbalimbali ya vioo kabla hujamua ni vipi unataka.

Ili kukifanya chumba kisicho na uwiano kionekane kuwa nao, funga vioo vya mapambo ukutani. Vioo hivi viwekwe kuakisi vitu fulani kwenye chumba ili kufanya ionekane kama vitu hivi viko katika kila upande wa chumba, kwahivyo pale unapoingia uone kama chumba kina uwiano na ni kikubwa.

Baadhi ya wenye nyumba wanatamani waboreshe muonekano wa ndani wa nyumba zao. Marekebisho yana gharama kubwa, hata hivyo wewe mwenye nyumba usizime tamanio lako. Unaweza kunyanyua uso wa ndani ya nyumba yako kwa kutumia vioo vya mapambo badala ya marekebisho makubwa.. Mradi huu mdogo wa kunyanyua uso kwa kutumia vioo unaweza kukupa matokeo usiyotarajia. Kupamba kwa vioo ni moja kati ya njia nyepesi na rahisi za kuboresha muonekano wa ndani ya nyumba.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com



No comments:

Post a Comment