Pages

Thursday, December 11, 2014

my article for newspaper: kuhifadhi taulo na ugeni

Jinsi unavyoweza kuhifadhi taulo za bafuni kwa ajili ya wageni watakaokutembelea msimu huu wa sikukuu.

Moja ya faida za kipindi cha sikukuu  ni fursa ya kufungua nyumba yako kwa wageni ambao hamjakaa pamoja mwaka mzima.  Kama utakuwa na wageni nyumbani msimu huu wa sikukuu, makala hii inakuhusu. Mahoteli yanafanya wageni wao wajisikie spesho kwa ajili wanafahamu jinsi ya kuwafanya wajisikie  nyumbani kwa kuwapatia mahitaji muhimu. Wewe pia unaweza wafanya wageni wako wajisikie kama wameshukia kwenye hoteli ya kitalii wanapokuwa nyumbani kwako, kwa ajili tu ya buduriko wanalopata wanapokuwa kwenye chumba au vyumba vyao vya wageni hapo kwako.

Ni  bafu chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taulo za wenyeji na wageni kwa wakati mmoja, na huenda unafikiria ni jinsi gani utahifadhi taulo za wageni wako watakapokutembelea. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni dogo namna gani njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi taulo za wageni wako.

Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi taulo za bafuni. Fimbo hizi hazichukui nafasi kubwa na wala hazina marembo kwahivyo ni suluhisho tosha kuhifadhi taulo kavu na hata zile zenye unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu na kuzifanya kukauka kirahisi, hivyo kuzuia kuota kwa ukungu.

Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza kufungwa pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.

Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni fimbo iliyosimikwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi zimewekwa imara kwakuwa kama tujuavyo taulo zikiwa mbichi zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika na watoto kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila wapoona panafaa, na pia wazee kujishikilia wakiwa bafuni. Kwahivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za taulo ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya uimara.

Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu (rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za kuhifadhi taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa zinatundikwa ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili za taulo.

Ngazi za taulo ni chuma kingine kinachoonekana kama ngazi ndogo ambacho hutumika kuwekea taulo,  ni njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una nafasi kwenye ukuta wa chumba cha kulala cha wageni wako ambapo unaweza kuweka ngazi hii? Ni kiasi cha kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa kutandaza taulo za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo ni kuwa wakati kwenye fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya taulo unaweza kuweka hadi taulo 6.

Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya uusumbue ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu ya kusimama inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba cha kulala cha wageni wako kina nafasi kidogo ya ziada basi simamisha susu ya koti kwa ajili ya kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa wakati mmoja. Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo wageni wako wawe wanazigeuza mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za wageni tofauti tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna anayependa kushirikiana taulo.

Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Kama unataka wageni wako wajisikie kama wako kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo zao safi zilizobiringishwa vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano wa kuvutia kwahivyo kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa vizuri ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko ile ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe ni mtu wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.

Kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo kiasi kwamba huna mahali pa kuhifadhi taulo za wageni wako msimu huu wa sikukuu hatimaye leo umefahamu njia kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo wakati huo huo ukiwa unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ilikurahisisha maisha bafuni sikuzote na hata msimu wa wageni.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye anajishughulisha na usafi wa magari, mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda christines.daughter@yahoo.com au 0755 200023

No comments:

Post a Comment