Pages

Thursday, January 15, 2015

my article for newspaper: mwavuli wa kwenye bustani

Fahamu haya kabla ya kununua mwavuli wa kwenye bustani


Kwa kawaida ya binadamu anafurahia zaidi akiwa amepumzika nje ya jengo, ndio maana utaona kuwa sehemu nyingi za burudani iwe ni kwenye migahawa wengi wanapendelea kukaa nje kuliko ndani. Ukishafungia watu ndani tu, wanahama kuelekea pengine ambapo watakaa nje. Sasa basi ni nani asiyependa kuwa na wakati mzuri akiwa katika mazingira ya nje ya nyumba yake? Imekuwa ni burudani kwa binadamu toka enzi kwa hivyo kuwa tu na meza na viti kwenye bustani bila mwavuli hailipi.

Samani za kwenye bustani zimetengenezwa na wataalam, na wao wanajua zaidi, kwa hivyo nimewauliza ushauri  na wakanieleza ni aina gani za samani zinazotakiwa kwa matumizi ya wazi kwenye bustani na katika makala hii tutatizama zaidi mwavuli wa kwenye bustani.

Mwavuli wa kwenye bustani zaidi ya kutumika pia ni pambo eneo la nje ya nyumba Mwavuli huu ni sahihi kwa kuwapa wenyeji na wageni kivuli siku za jua kali. Na zaidi ni kuwa unaboresha afya, Aisha anaanza kueleza.

Kwanza kabisa ni lazima kuwa makini sana na malighafi iliyotengenezea mwavuli. Mwavuli wa kwenye bustani unatakiwa kuwa imara sana kwani unatumika nje ya nyumba. Unatakiwa uwe imara vya kutosha kuhimili jua la kiangazi, mvua kubwa na upepe mkali.

Miavuli hii ni mikubwa tofauti na ile ya kubeba mkononi na inapatikana kwa maumbo, rangi na vitambaa mbalimbali.

Kuamua ni aina gani ya mwavuli wa bustani utakufaa inakupasa uijue kwa undani ndipo unapoweza kufanya uchaguzi. Eneo la kitambaa la mwavuli huu ni lile linalowakinga jua na mvua wale walio chini yake. Mwavuli unafaa uwe wa kufunga na kufungua mithili ya ule wa mkononi na fremu zake zipo za aluminiam, mbao na chuma. Mlingoti wa mwavuli unene wake ni kati ya inchi moja hadi tatu.  Vipande vya fremu vinavyoupa mwavuli umbo lake na kubeba kivuli ukiwa umefunguliwa vinapaswa kuwa imara. Mbavu za mwavuli (zile zinazoshikilia kitambaa) pia zinatakiwa ziweze kuhimili pepo za wastani hadi za kasi. Kitako cha mwavuli kiwe na uzito wa kutosha kubeba sehemu yote ya mwavuli iliyobakia. Ukifahamu sehemu hizi za mwavuli wa bustani itakusaidia kupata mawazo ya kuweza kununua mwavuli sahihi na wenye vigezo na malighafi utakazo, anasema Aisha.

Nunua mwavuli ambao unatosha eneo unalotaka kufunika na kukupa kivuli unachotaka. Miavuli ya kwenye bustani inasimama yenyewe, na pia haijalishi ni mtindo upi, rangi na ukubwa miavuli hii inapatikana kwenye maduka yanayouza samani za bustanini, anasema Aisha.

Miavuli ya bustani inauzwa yenye milingoti ya kati ya futi 6 hadi 13 japo mzunguko wa kivuli hauhusiani na urefu wa mwavuli. Mwavuli wa bustani mdogo sana haupendezi, mkubwa unafaa zaidi japo unategemea na ukubwa wa eneo lako. Pima ukubwa wa samani zako au eneo litakalofunikwa na mwavuli husika kabla ya kununua mwavuli wenyewe.

Kwa unene wa mlingoti, wateja wenye meza zenye tobo la mwavuli katikati wanapaswa kupima kwanza ukubwa wa tundu kabla ya kuamua unene wa mlingoti ili kujiridhisha kuwa sio dogo sana au kubwa zaidi. Miavuli mikubwa inahitaji uimara zaidi, na milingoti yake inakuwa minene.

Hakuna ubishi kuwa kitambaa cha mwavuli ndicho kinachoonekana zaidi. Wenye nyumba wengi wanapenda kuchagua kitambaa hiki kwa kutizama rangi. Wengine hupenda kuoanisha rangi ya kitambaa hiki na rangi nyingine za nje ya nyumba zao. Wakati hili nalo ni muhimu, wanunuzi wanapaswa pia kuchagua kivuli cha mwavuli kuendana na malighafi za kitambaa.

Zaidi ya kuamua rangi au michoro fulani ya kitambaa, chagua mwavuli wa bustani wenye malighafi zitakazohimili matumizi yako, wapo ambao wanauweka mwavuli bustanini kwa kipindi cha matumizi tu na wapo ambao mwavuli upo hapo kila siku hautolewi. Malighafi na rangi ya kitambaa utakayochagua isiwe inapauka au kuota ukungu.

Utakapoweka mwavuli wa bustani nje ya nyumba yako huenda ukabadili mfumo wa maisha wa mwenzi wako akajikuta badala ya kwenda baa mnatengeneza nyama choma na kula hapo hapo nyumbani!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christinesdaughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment