Pages

Saturday, February 21, 2015

Binti anapopelekwa mahabusu pengine ajifunze kumbe inasababisha balaa zaidi

POLISI aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumbaka mahabusu katika kituo kidogo cha Ilembula wilayani Wanging'ombe mkoani hapa, Juma Nyambega, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Njombe kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Majira linaripoti kuwa:
Askari huyo mweye namba F 6565 alihukumiwa adhabu hiyo na mahakama ya Wilaya ya Njombe mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Augustine Rwezile.

Akisoma hukumu hiyo, Rwezile alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mlalamikaji pamoja na vielelezo vya daktari aliyempima binti huyo mwenye umri wa miaka 19 na kubaini kuwepo kwa michubuko sehemu zake za siri.

Askari huyo alipandiswa mahakamani hapo kwa kosa la kumbaka binti huyo, aliyekuwa amewekwa mahabusu. Ilidaiwa kuwa alitolewa kwenye chumba cha mahabusu na kumbaka.

"Mahakama baada ya kusikiliza maelezo ya daktari aliyempima binti huyo na maelezo ya upande wa mlalamikali imebaini kuwa mshtakiwa alifanya kosa hilo na mahakama inamuhukumu kwenda jela miaka 30,"alisema hakimu huyo.

Alisema mshtakiwa kama atakuwa hajaridhika na hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama yake anaruhusiwa kukata rufaa. Awali akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali Magdalena Kisowa aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 10, mwaka jana saa 2 usiku akiwa kituo cha polisi.

Siku ya tukio hilo askari huyo alikwenda kwenye chumba cha mahabusu ambacho alikuwepo mlalamikaji na kumwambia kwamba anampeleka chumba kingine ambacho kilikuwa na mwanga na kisha kumbaka.

Aidha wakili Kisowa aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za ubakaji kwani kitendo hicho ni cha unyanyasaji na udhalilishaji kwa mwanamke.


No comments:

Post a Comment