Pages

Wednesday, February 25, 2015

Hatari za kuweka picha za mtoto mtandaoni

Nimekutana na article hii ambapo mwandishi anatahadharisha  tabia ya kuweka picha za watoto mtandaoni, ni kweli kuwa wengi tunafanya hivyo. Je, wewe unaona ni poa tu kuweka picha ama sio sawa.

Nianze kwa kukuuliza wewe mzazi; unapoweka picha ya mtoto wako kila hatua tangu akiwa mchanga hadi anaanza kutembea na kuanza shule, alikuomba au ulipata ruhusa yake?

Ingekuwa wewe umepigwa picha bila idhini yako halafu ukaikuta kwenye mtandao utafurahi?
Najua unampenda mtoto wako na ana haki zake za msingi pamoja na kuheshimiwa faragha yake popote alipo. Haiwezekani chochote anachofanya ukiweke kwenye mtandao.

Naomba kueleza madhara yanayoweza kutokea kwa kuweka picha za mtoto wako au wa mwenzako kwenye mitandao hasa mitandao ya kijamii kama facebook , instagram na mingineyo.

Kwanza fahamu kuwa kampuni karibu zote za mitandao ya kijamii zimesajiliwa Marekani, chache zimesajiliwa Ulaya na Asia, lakini karibu zote zinatumia sheria na sera za mataifa hayo.

Katika mataifa hayo wanasisitiza mtoto asijiunge kwenye mitandao ya kijamii hadi atakapofikisha miaka 13, wengine miaka 15 au 16 .

Kampuni zote za mawasiliano zina utaratibu wa kuhifadhi kila kitu kinachotokea kwenye shughuli zao za kila siku kwenye chombo maalumu cha kuhifadhi taarifa za mtandao (server). Kwa hiyo ukiweka picha za mtoto zinahifadhiwa huko hata kama utazifuta.

Hapo awali, nilisema mtoto anahitaji faragha yake, unaporusha picha za mtoto wako kwenye hii mitandao au mawasiliano yoyote, unaingilia faragha yake na huko mbele anaweza kukushtaki wewe au wengine walioingilia faragha yake.

Mtoto anatakiwa kufunzwa kuanzia mdogo kabisa kuhusu faragha yake, nini cha kusema au kutoa na nini asiseme au asitoe. Hii ni pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, simu na huduma nyingine za mawasiliano .

Umeshawahi kuona wanasiasa wanaweka picha za watoto wao au ndugu zao wa karibu kwenye mitandao hasa ya kijamii ? unajua ni kwa nini ?
Kwa sababu kila anachofanya yeye kinamwathiri mtoto wake au watu wake wa karibu kwa ubaya au uzuri. Ni rahisi kuweka rehani faragha za watoto na ndugu zake.

Kama ni mtoto wa kike anaweza kuanza kufuatiliwa na ‘mabazazi’ kwa sababu ya picha tu. Watatafuta anapoishi, shule anayosoma na usishangae siku moja akabakwa.

Siku hizi kuna biashara ya kutangaza ngono mitandaoni ukiweka picha ya mtoto hujui kina nani wanaangalia na kwa matumizi gani. Wapo wanaoweza kuitumia picha hiyo kutangaza kuwa mwenye picha anafanya biashara ya ngono, utajisikiaje kama mzazi?


Hata hivyo, picha ya mtoto wako inaweza kutumika kutangaza biashara fulani bila wewe kujua. Haya yameshatokea.

No comments:

Post a Comment