Pages

Thursday, February 19, 2015

MAKALA: Jinsi ya kupamba meza kwa kutumia utepe

Utepe wa kitambaa cha meza (table runner) ni kitambaa chembamba kinachotandazwa  katikati ya meza. Ni njia rahisi na ya haraka ya kubadilisha muonekano wa meza yoyote ile. Vitambaa hivi vinapatikana kwa ukubwa, rangi na malighafi za aina mbalimbali. Wakati unaweza kufuata kanuni katika kutumia utepe wa mezani lakini pia unaweza kuwa mbunifu mwenyewe na kuutupia kwa jinsi unayoona inakupendeza.
Kwa uzoefu kitambaa hiki kinatakiwa kining’inie kila upande wa meza. Kikiwa hivi kinapendeza zaidi kuliko kile kinachoishia mwisho wa meza au hata kifupi kuliko meza. Urefu wa kuninginia unatakiwa kuwa sawa  kila upande kama tu ambavyo kitambaa cha meza kinaning’inia. Kuna ambao wanatumia kitambaa cha meza na wakati huhuo kukiwa na utepe (hasa kwenye shughuli kama harusi wapambaji huwa wanapenda kuweka vyote pamoja). Kama ndivyo basi urefu wa kuning’inia wa vitambaa hivi viwili unapaswa uwe sawa.

Upana wa utepe unatakiwa uwe theluthi ya upana wa meza. Kwa maana hiyo unavyotupiwa pale kati ya meza unabakiwa na pande mbili za meza zenye upana karibia sawa na wa utepe. Na hii ni kama unatupia kwa kuendana na urefu wa meza. Endapo itakuwa unatupia kwa upana, utahitaji tepe zaidi ya moja na upana unaweza kupungua.

Tepe nyingi zimeshashonwa tayari na zinakuja kwa upana wa inchi 10, 12, 13, 14 na 15 na kwa urefu wa inchi 54 hadi 108. Kwahivyo kabla ya kununua unapaswa kufahamu ukubwa wa meza unayotaka kuuwekea.

Kumbuka kuwa hakuna kanuni hasa za kutumia utepe wa mezani, usiogope kama upana au urefu hautakuwa jinsi inavyosemwa hapa, kinachotakiwa ni wewe ujue unachotaka, ukipende na ujue jinsi ya kuupamba. Haya mambo ya vipimo yanahusu zaidi kwa upambaji wa matukio rasmi kama harusi na warsha.

Na hata kama vipimo hivi havitaendana na meza yako, maadam umeshajua mbinu ni kiasi cha kutengenezesha kwa fundi (au hata ukashona mweneywe) kwa kitambaa unachopenda kiwe ni batiki, kitenge na kadhalika.

Tepe za mezani zinaweza kutumika kwa njia mbalimbali na kwa meza yoyote japo kiasili zilitumika kwenye meza za chumba cha chakula, hata hivyo unaweza kuwa mbunifu na kuzitumia kwenye meza yoyote iwe ni ile meza ndefu, ya kahawa, ya pembeni mwa sofa, ya kwenye varanda au ya bustanini. Zinawezekana kwa meza ya umbo lolote liwe pembe nne, duara na yai.

Njia iliyozoeleka zaidi ya kutumia utepe wa mezani ni kwa kuuweka katikati ya meza ukiwa unakimbia kwa urefu. Hii inasadia kuweka pambo la kati na hata mabakuli ya vyakula kwenye mstari wakati wa kula. Huu utepe pia kinasaidia kufanya meza isikwaruzwe na vyombo au mapambo mengine, na kukinga polishi yake isiharibiwe na joto la vyakula.

Unaweza pia ukatumia tepe fupi na nyembaba zilizowekwa kwa upana wa meza. Hizi za hivi zaidi ya kutumika kama mapambo ya meza pia zinaweza kutumika kama mkeka wa meza wakati wa kula kuwekea sahani.

Vimikeka vidogo (mats) vya meza vya kuwekea sahani vinaweza kutumika pamoja na utepe kwa rangi zinazofanana. Na kwa maana hivyo hutakuwa na haja tena ya kutandika kitambaa cha meza.

Kama vinatumika pamoja utepe wa mezani usifanane na kitamba cha meza, unatakiwa kuwa na rangi tofauti ili uonekane usimame peke yake.

Unaweza pia kutumia utepe wa mezani kwenye fenicha nyingine. Tumia tepe kulinda fenicha zilizotengenezwa kwa glasi,utumie wakati unapotaka kuweka kitu juu ya meza ambacho unadhani kitakwaruza meza.

Ni vyema kuangalia ulaini wa kitambaa cha utepe kama utaendana na ulaini wa meza yako. Kwa mfano, kama meza yako ina kioo au imepakwa polishi ina maana inateleza, haifai kuweka utepe wa hariri (silk), satini ama polista.  Tepe za namna hii zitafaa kwa zile meza zisizokuwa na finishing ya kuteleza.

Utepe za mezani uoane na mapambo yako mengine ya hapo chumbani.
Tepe za mezani zinaweza kupatikana popote wanapouza vitambaa vya meza.

Tepe za mezani ni njia bora zaidi ya kupamba meza kwa kuiongezea rangi na muonekano. Zinapendeza pale zinapotumiwa na mapambo mengine mezani kama vile vesi ya maua au bakuli la matunda.


Makala hii imeandaliwa na Vivi ambaye ana mapenzi na muonekano wa nyumba. Kwa maoni ama maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment