Pages

Monday, February 16, 2015

Ohooooo, kama ulikuwa hujui, kuvaa kimini ni kosa la jinai.

WATUMISHI wa serikali wilayani Masasi mkoani Mtwara, wanaovaa nguo fupi yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania, maarufu ‘vimini’, wameonywa kuacha mara moja tabia hiyo.
Imeelezwa kuwa nguo hizo licha ya kudhalilisha kazi zao, pia ni aibu kwa mtumishi wa umma kuvaa mavazi hayo. Tayari Jeshi la Polisi wilaya ya Masasi, limeagizwa kufanya operesheni maalumu kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wote wanaovaa nguo fupi, kwani kuvaa nguo fupi ni kosa la jinai, ambalo mhusika anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na watumishi wote wa wilaya ya Masasi, madiwani na viongozi wa kimila wa kabila la Wamakua (Mamwenye).

Alisema tabia za baadhi ya vijana za kuvaa nguo fupi, haikubaliki kwa jamii ya kitanzania. Alisema ni aibu na fedheha kwa mtumishi wa umma, kuvaa nguo fupi kwa kuwa kitendo hicho kinakiuka maadili ya utumishi wa umma.

Alisema kuna watumishi wengi tu wanavaa nguo fupi kazini, hivyo amewaagiza maofisa rasilimali watu kushughulika na watu hao. Dendego alisema anasikitishwa na vijana wa kiume, ambao wengi wao kwa sasa wamekuwa wakivaa nguo zinazoonesha sehemu ya nguo zao za ndani kwa kushusha chini suruali zao (mlegezo).

Alisema uvaaji huo haukubaliki na inabidi uachwe na vijana wote nchini. Alisema vijana wengi wamekuwa wakiiga vitu vinavyofanywa na wenzao wa mataifa ya Magharibi.

Aliwaonya kuwa si kila kitu kinachofanywa na vijana hao ni cha maana na kinatakiwa kuigwa, badala yake waige masuala muhimu na ya msingi katika maendeleo yao.

“Nyinyi vijana mliopo hapa ndani naomba mnifikishie ujumbe wangu kwa wenzenu kuwa kuanzia leo yeyote atakayevaa nguo fupi kwa wasichana na mlegezo kwa wavulana, atakamatwa na Jeshi la Polisi na hatimaye kufikishwa mahakamani na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Dendego.

Dendego alisema vijana wavae mavazi ya heshima wakiwa kazini na kwamba kuvaa kwao mavazi yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania, ni kujishushia heshima na hadhi yao kwa wazazi wao na jamii.

Aliwaomba watumishi walio kazini kwa muda mrefu, watoe maelekezo kwa vijana hao waachane na tabia zinazokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.


Alisema kwa sasa kuna vijana wengi tu wanavaa nguo fupi na zile zinazobana, hivyo kusababisha maumbile ya miili yao kuonekana. Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment