Pages

Wednesday, February 25, 2015

Kimenuka Iringa

*Raia wachoma magari ya polisi, wapora silaha
*Wawafungulia mahabusu, wateketeza nyaraka
*Mmoja afariki, mabomu ya machozi yatumika


Jambo leo linaripoti kuwa MAPAMBANO makali yameibuka katika Kata ya Ilula mkoani hapa, kati ya raia na polisi, hali iliyosababisha Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kulazimika kutumia mabomu ya machozi kutuliza vurugu hizo zilizoibuka kutokana na kifo chenye utata cha mwanamke mmoja.

Tukio hilo limetokea jana saa 5 asubuhi, ambapo vurugu hizo zilidumu hadi saa 10 jioni, huku Kituo cha Polisi kikivunjwa, bunduki kuporwa na nyingine kuchomwa moto na magari matatu na pikipiki moja ya polisi.

Wakielezea tukio hilo, wakazi wa Mji wa Ilula mkoani hapa, walidai kuwa chanzo ni askari watatu watatu, akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ilula kwenda kufanya msako wa wananchi wanaokunywa pombe muda wa kazi.

Kutokana na msako huo, mwanamke huyo aliyepoteza maisha aliyetambulika kwa jina la Mwanne Mtandi aliamua kukimbia kukwepa kukamatwa na Polisi hao, kabla ya kukutwa nyuma ya jengo la klabu hicho cha pombe za kienyeji kilichopo Mtaa wa Ilala mjini Ilula, akiwa amekufa.

“Polisi hawa kila siku wamekuwa wakifika hapa klabuni na kukamata watu, siku ya kwanza walimkamata marehemu na kumtoza faini ya sh. 20,000 na siku ya pili walimkamata yeye na mumewe na kuwatoza faini sh 40,000, leo walikuwa wakija kumkamata tena na hapo ndipo mwanamke huyo aliamua kutimua mbio, kabla ya kukutwa amekufa” alisema shuhuda wa tukio hilo, Shida Ngwata.

Huku, Mkazi mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema polisi hao walilazimika kutumia mabomu na risasi za moto kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza, huku moja kati ya bomu likiokotwa ambalo lilikuwa halijalipuliwa.

Alisema askari watatu ndiyo ambao walikuwa wakisakamwa na raia hao ambao pia wamevunja vioo vya basi la Upendo kutokana na mkuu wa kituo cha Ilula kukimbilia ndani ya basi hilo wakati akifukuzwa na raia hao.

Diwani wa Kata ya Nyalumbu, Ally Kikunga alisema kuwa, alipigiwa simu na wananchi wake kujulishwa kuhusu vurugu hizo na baada ya kufika eneo la tukio, alikuta mwanamke huyo akiwa mahututi, ila hakuweza kupata msaada kutoka kwa wananchi wengine kumkimbiza hospitali .

Diwani huyo alilishauri jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu zaidi, kwani alisema eneo hilo la klabu ni eneo ambalo wananchi wanapata mahitaji mbalimbali na kwamba, mwanamke huyo alikuwa akifanya usafi katika chumba chake cha biashara ya pombe.

Hata hivyo, alisema raia hao wameharibu mali mbalimbali na nyaraka zote na kuwafungulia mahabusu wote waliokuwemo ndani, huku lori moja lililokamatwa kituoni hapo likilindwa kuharibiwa kuwa halina kosa.

Vurugu hizo zilisababisha wasafiri wanaotumia barabara ya Kuu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kukwama kwa zaidi ya saa sita.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, ilifika eneo la tukio na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akiahidi kutoa taarifa kamili ya mali zilizoharibiwa na chanzo halisi cha tukio hilo, baada ya kukaa kikao na viongozi wa jeshi la polisi na wale wa mji wa Ilula

Ingawa mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari mawili ya polisi na pikipiki yakiwa yamechomwa moto, gari moja la askari pia lilichomwa moto na magari mawili, moja la askari na daladala moja na basi la Upendo kuharibiwa vibaya


Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, hakupatikana kwani alikuwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, baada ya kikao hicho, watatolewa taarfa kamili kuhusu vurugu hizo.

No comments:

Post a Comment