Pages

Thursday, February 26, 2015

Unavyoweza kuboresha sebule yako haraka na kwa gharama nafuu

Kama unatafuta njia rahisi na haraka ya kuboresha sebule yako basi makala hii inakuhusu. Utapata mawazo hapa ya kubadilisha muonekano wa sebule uwe bora zaidi kwa haraka, bila gharama kubwa na bila wataalam.
Kwa kuboresha muonekano wa ukuta  suluhisho la gharamna nafuu zaidi ni kupaka rangi. Paka rangi nyeupe au yoyote ya mwanga kama unataka dari ionekane ndefu. Endapo hutapenda kupaka rangi basi bandika karatasi za ukutani. Vinginevyo kama rangi ya ukuta inaonekana ni safi  unaweza kuongeza muonekano kwenye  kwa haraka na gharama nafuu kwa kutumia stika za ukutani. Bandika stika kubwa na za rangi za giza kwenye maeneo unayotaka kusisitiza au kwa kutengeneza boda kuzunguka kioo. 

Stika za ukutani ni wazo zuri za kubadilisha muonekano, pia ni gharama nafuu na unaweza kuziondoa pale ambapo huzihitaji tena.

Funga vioo ukutani kuongeza mwanga na nafasi sebuleni, vinageuza eneo dogo na lenye mwanga hafifu kuonekana kubwa na lenye mwanga wa kutosha. Weka kioo ukuta unaotazamana na dirisha ili kibebe mwanga unaongilia dirishani kiusambaze chumbani. Pia kioo kikufungwa kutazamana na vitupio au maua yaonekane yapo mawilimawili.

Sanaa zinabadilisha muonekano wa chumba, tundika picha mpya za familia au fremu za michoro kuboresha muonekano wa ukuta wa sebule yako. Picha na michoro hii unaweza kuviweka kwenye fremu za rangi tofauti tofauti kuoongeza mvuto.

Sasa umemalizana na ukuta. Ukija kwenye sofa ziboreshe pamoja na mito na kusheni zake kwa kushonea kitambaa kipya. Ni gharama nafuu kuliko kununua sofa mpya, na vitambaa na mafundi wapo wengi. Hata zile sofa zenye vitambaa ambavyo havivuliki ili kusafishwa kwa kina vitakuwa vimeondolewa ama kufunikwa ndani ya hiki kipya. Kama una cherehani na unaweza kushona foronya za mito na kusheni inakuwia nafuu sana kwani hata kuzishona sio kazi kubwa.

Weka maua na miti artificial, hii inasaidia sana kuboresha muonekano wa sebule. Pia baadhi ya maua na miti yanafanana kwa karibu sana na ya asili kiasi kwamba kama hujaigusa ni ngumu kutofautisha. Pasipo shaka maua na miti ni njia rahisi mno na ya gharama nafuu ya kuongeza rangi kwenye sebule yako.

Ongeza mvuto kwa kubadilisha vikombe vya taa za ukutani au vivuli vya taa za mezani. Pia kama taa ya ukutani ni balbu pekee basi ivalishe kikombe. Na kwa gharama nafuu kama ulikuwa na hizi taa za vivuli tayari, kwanini usibadili tu kivuli chake? Tembelea kwenye maduka ya vitu vya sanaa wapo wanaouza vivuli vya taa kwa malighafi za asili kama vitenge na mkeka.

Valisha upya madirisha ya sebuleni, baada ya muda pazia huwa zinapauka hasa pale ambapo panapigwa na jua kali kwa kipindi kirefu cha siku. Kusema la ukweli maduka yenye vitambaa vya mapazia au mapazia yaliyoshonwa tayari ni mengi na yapo ya iana nyingi na kwa bei ya kuridhisha ambapo walau kwa chini ya elfu 15 unapata pazia.

Sakafuni kama umetandika mazulia makubwa ficha sehemu zinazoanza kuchakaa kwa vizulia vidogo badala ya kununua lingine kubwa. Kumbuka hapa tunajuzana njia za gharama nafuu, kwa mfano kama umeweka zulia la ukuta kwa ukuta, kuficha maeneo chakavu kwa vizulia vya kutupia ni gharama nafuu kuliko kuondoa lote na kutandika jipya. Pindi utakapokuwa kwenye hali nzuri kipesa ndipo utakaponunua kubwa jipya. Vizulia vya kutupia viwe na rangi kali ili kuleta mvuto wa chumba. Rahisi zaidi - na haraka – kuliko kubadilisha zulia zima!

Mpenzi msomaji, natumai umekubaliana na mimi kuwa hizi ni njia za haraka zaidi na gharama nafuu za kubadilisha muonekano wa sebule yako ili iwe na mvuto zaidi. Je kuna njia ambayo nimesahau? Tuelimishane kupitia kwenye blogu yangu hapo chini.

Makala hii imeandaliwa na Vivi ambaye ana mapenzi na muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com


No comments:

Post a Comment