Pages

Thursday, March 12, 2015

JINSI YA KUKWEPA MRUNDIKANO KATIKA MAISHA YA CHUMBA KIMOJA


Muonekano wa mrundikano katika chumba kimoja

Hakuna ubaya wa kuishi kwenye chumba kimoja kama uko mwenyewe na ndio unaanza maisha ya kujitegemea. Cha muhimu ni kufahamu jinsi ya kupanga vitu vyako. Kuweza kuwa na mpangilio wa vitu mahali unapoishi au pengine popote mara nyingi inakuhitaji uwe na sehemu nyingi za kuhifadhia ambazo ni mashelfu, madroo na makabati.

Kitu kitakachofanya chumba kimoja kukosa mpangilio ni mrundikano. Mrundikano unafanya mahali paonekane pachafu, ondoa mrundikano kwenye chumba chako ambapo kitaonekana kuwa na nafasi na kisafi. Wewe mwenyewe utajisikia msafi na kujiona mwenye kupanga vitu vizuri. Sasa utaniuliza kuwa, chumba ni kidogo sasa nitapata wapi pa kuhifadhia pa ziada? Endelea kusoma utaelewa.

Nunua au tengeneza kitanda, meza na sofa vyenye maeneo ya kuhifadhia kwa chini. Vitu hivi vinawezesha kuweka mpangilio pale vinapokuwa na maeneo ya kuhifadhia, yaani kitanda au sofa ambalo mvunguni kuna droo za kuhifadhia. Vyote hivi ni jinsi ya kuongeza eneo la kuhifadhia kwenye chumba kimoja. Kimeza ambacho kina eneo la kuhifadhia kwa chini ni bora zaidi ya kile kitupu. Mantiki ni kuwa, nunua fenicha ambazo zitakidhi hitaji zaidi ya moja kwenye chumba chako.

Droo za kuhifadhia mvunguni mwa kitanda unaweza kuhifadhi vitu kama shuka, mito, taulo na blanketi za ziada. Droo za chini ya sofa, utafuta viatu vyako vizuri baada ya kutoka kazini na kuvihifadhi humo, na hata vile usivyovaa kila siku lakini bado unavihitaji.

Labda wewe ni mwanafunzi ama unafanya kazi na una mambo mengi yanayokuhitaji kujikumbusha, tundika umbao wa sponji kwa ajili ya kutobolea kwa pini vikaratasi vya  ratiba, vipindi  au mikutano yako ya wiki hiyo. Hi itakusaidia kuondoa mrundikano wa karatasi kusambaa kila mahali kwenye meza hapo chumbani. Zile ratiba za wiki inayofuata zihifadhi kwenye droo hadi zitakapokaribia ndipo nazo unazitobolea kwenye ubao wako. Wakati huohuo ukifaili ama kutupa zile karatasi usizohitaji tena.

Kwenye chumba chako hicho kimoja weka kabati la nguo ambalo lina milango. Kwa ndani kwenye milango pigilia kulabu ambazo utatumia kutundika mikoba, mabegi na hata shanga na mikufu yako.

Ukubwa wa vitu unahusika kwenye chumba kimoja. Fenicha kwa mfano, sofa zitakavyokuwa kubwa ama viti vingi na nafasi nayo itaonekana finyu. Badala yake weka sofa la viti vitatu au viwili ambavyo kwakweli wewe na mgeni wako vinakutosha huhitaji zaidi. Pia michoro mikubwa eneo dogo inafanya sehemu ionekane ndogo. Kwa mfano, kuwa na pazia na shuka zenye michoro mikubwa kwenye maisha ya chumba kimoja zitakifanya chumba chako kionekane kimerundikana. Aidha weka vitambaa vya rangi moja au vya maua madogodogo ambapo pia unatengeneza hisia za utulivu chumbani.

Ukiwa unaishi kwenye chumba kimoja uwe na vitu unavyohitaji kwa wakati husika tu. Huna haja ya kuwa na nguo, viatu na vyombo ambavyo huvitumii kwa wakati huo. Mrundikano wa vitu unavyotumia na usivyotumia utakuvuruga kiasi kwamba unashindwa kuona hata kile unachohitaji kutumia. Wengi wetu tunapenda kuhifadhi vitu tusivyotumia tena, labda ni kwa kuogopa kuwa huko mbeleni tutavihitaji tena au pengine ni hulka tuu. Ni busara kuondoa vizee ili kuacha nafasi kwa vipya. Kwaheri cha zamani na karibu kipya.

Kila utakaponunua kitu kipya na kuingiza kwenye chumba chako kiage kile cha zamnai. Kwa mfano kama umenunua ufagio mpya tupa ule wa zamani badala ya kuhifadhi yote miwili. Kama unadhani wa zamani haujaisha sana kwanini umenunua mpya sasa?

Kwa teknolojia inavyosonga mbele huja haja ya kuwa na picha nyingi za karatasi, badala yake unaweza kufremu chache na nyingine kuziacha kidigitali. Picha za kidigitali zinaweza kutizamwa zaidi kimtandao kwa kushirikisha ndugu, marafiki na wengine wengi ambao wasingeweza kuja kwako wazione kwenye albam ya picha za katatasi.

Kila wakati chumba chako kimoja kiwe kwenye mpoangilio. Kutumia dakika 15 asubuhi kuweka vitu vizuri na kutandika kitanda kitafanya maisha yako ya chumba kimoja yaonekane nadhifu kupita maelezo.


Makala hii imeandaliwa na Vivi ambaye ana mapenzi na muonekano wa nyumba. Kwa maoni ama maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment