Pages

Sunday, March 15, 2015

LUIZA MBUTU: NILIPATA WAKATI MGUMU FAMILIA YANGU KUELEWA NINACHOKIFANYA

Ukimuona huwezi kuamini anachosema lakini ukweli ni kwamba ana miaka 19 katika muziki wa dansi, anamudu kusimama jukwaani kucheza na kuimba kwa zaidi ya saa nane bila kuchoka huku akifanya hivyo siku tano kwa wiki kuanzia Jumatano hadi Jumapili.

Hapa namzungumzia mwimbaji aliyetimiza miaka 16, akiwa katika bendi ya Twanga Pepeta bila kuhama, naye siyo mwingine ni Luiza Nyoni Mbutu, mke halali wa mwanamuziki Faijala Mbutu.

Mwananchi ilifanya mahojiano na mwanamama huyo ambapo mbali na mambo ya muziki alizungumzia zaidi maisha ya kawaida anapokua mama Brian na mke wa Mbutu.

Luiza anasema kazi yake haimzuii kufanya majukumu yake kama mke na mama; “ukitaka kulibaini hilo unikute nyumbani, nahudumia wageni, familia na nyumba kwa ujumla huwezi kuamini kama ndiyo yule anayewasha moto jukwaani.

Kwa mujibu wa Luiza, anachukia sana baadhi ya wasanii wanaotumia muda mwingi wakila bata na kusahau majukumu yao katika jamii.

Anasema kula bata ni uamuzi ya mtu lakini kwake yeye kama mama mwenye mtoto mmoja anahitaji kuwa na muda wa kupumzika na familia yake badala ya kurandaranda kila kona kwenye kumbi za Starehe.

Anaongeza kuwa kila inapofika siku ya Jumatatu na Jumanne kukaa na familia yake hatoki nyumbani labda iwe kuna kikao muhimu kazini. “Ninatumia siku hiyo kumwandalia vitu muhimu mume na mtoto wangu na hiyo ndiyo siku pekee ambayo tutapata nafasi ya kula pamoja chakula cha jioni kwani ninakuwa nyumbani,”aliongeza kuwa kwake yeye bata ni pale anapokuwa kazini kuwahudumia mashabiki wake.

Kuhusu changamoto anazokutana nazo kutoka kwa ndugu wa mume wake kutokana na kazi yake Luiza anasema hilo linampa wakati mgumu kutokana na utamaduni wa Watanzania kutoamini wanawake wanaofanya muziki.

“Siyo ya familia ya Mbutu pekee hata yangu pia ni changamoto, ukiwa mwanamuziki kila mtu anakutafsiri anavyotaka. Na hiyo ilikuwa changamoto kubwa kwangu ingawa haikunikatisha tamaa nilipambana na nilihakikisha siachi ibada.

“Hata nitoke kazini usiku wa manane lazima Jumapili saa tatu asubuhi niwe kanisani, nifanye ibada ndiyo mambo mengine yafuatie, nimemuomba Mungu mara nyingi awafanyie wepesi wanafamilia kunielewa kuwa mimi nipo kazini na sifanyi vitu tofauti kama wengi wanavyodhani.”

Hata hivyo, Luiza anasema kuwa anashukuru mume wake Mbutu kwa kumuelewa na kuikubali kazi yake huku akiwa balozi wa kutangaza sifa za uaminifu na umuhimu wa yeye kuwa na mwanamke huyo jambo lilomsaidia sana familia zote mbili kumuelewa.

Anasema unenguaji na muziki ni moja ya njia za kutafuta ajira kama kwa sekta nyingine hivyo Watanzania wanapaswa kuheshimu fani hiyo kama ilivyo kwa nyingine.

“Ninachokichukia ni dharau, kejeli, kutokuthamini. Sipendi watoa hukumu wanavyowahukumu watu kwa makosa wasiyokuwa nayo huku wao wakishindwa kufanya kazi yao ya kuchunguza na kuubaini ukweli.”alisisitiza.

Luiza anajigamba kuwa yeye ni balozi wa nidhamu na kamwe hata tumia kazi yake kujidharirisha kama wafanyavyo kwa baadhi ya wasanii wengine nchini.

“Sijawahi kuacha tumbo wala kitovu wazi kwa miaka yote niliyokuwa mwimbaji na mnenguaji, nimefanya hivyo nikiwa na mume na hata nilipokuwa sijaolewa, hivyo unaweza kumuona mnenguaji, mwimbaji tofauti na hili linawezekana na bado watu wakakubali kazi yako.”

Kuhusu wasanii wanao saliti wapenzi wao, Luiza alisema anajiheshimu na kumuheshimu mume wake lakini pia anampenda mtoto wake hivyo hana haja ya kujihusisha na mambo yanayomvunjia heshima.

Luiza ni nani?

“Watu wengi wakisikia Nyoni wanadhani kabila langu ni Mngoni siotoki Songea, Mimi Mmwera wa Lindi;

Nje ya muziki nina shughuli zangu ambazo si vema kuziweka wazi hadi muda wa kufanya hivyo utakapofika, lakini ni halali na zinaniingizia kiasi fulani cha fedha.”alisisitiza

Hata hivyo, Luiza anasema kuwa endapo asingekuwa mwanamuziki ungekuwa mwelimishaji katika jamii, kwa sababu alipokutana na changamoto za kuwa mwanamuziki ndani ya ndoa , alitumia kipawa hicho na jamii na ikamuelewa.


No comments:

Post a Comment