Pages

Thursday, March 5, 2015

Maajabu! Wanakijiji wauawa eti wamezuia mvua isinyeshe, wamo mke na mume

Watu wanane wameuawa akiwamo mke na mume wake kutokana na imani za kishirikina katika mikoa ya Mara na Dodoma.
Watu hao wameuawa wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe na kusababisha vijiji vyao kukabiliwa na tatizo la ukame.

Katika tukio la kwanza, watu watano waliuawa katika kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti mkoa wa Mara usiku wa kuamkia jana.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ernest Kimola, akizungumza na NIPASHE jana kwa simu, alisema watu hao ambao hata hivyo hakuwataja majina waliuawa na wanakijiji wenzao wakiwatuhumu kuzuia mvua isinyeshe, hivyo kusababisha ukame kijijini hapo.
 
Kimola alisema juzi wakazi wa kijiji hicho waliitisha mkutano na kuanza kutafakari sababu za kijiji chao kukumbwa na ukame uliosababisha mito na mashamba ya mimea yaliyolimwa msimu huu kuanza kukauka na kuelezana kuwa hali hiyo imetokana na ushirikina unaofanywa na baadhi ya wenzao.
 
Alisema kufuatia hali hiyo walianza kuwataja kwa majina watuhumiwa hao na hivyo siku iliyofuata asubuhi walianza kuvamiwa nyumba zao na kuwashambulia kwa kipigo na kuwaua.
 
“Wananchi waliwachomoa katika nyumba zao watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi hadi kuwaua,” alisema.
 
Kimola alisema Jeshi la Polisi limeendesha msako mkali na  kuwakamata watu sita kwa tuhuma za mauaji hayo huku likiwasaka wengine.
 
Katika tukio lililotokea mkoani Dodoma, watu watatu waliuawa kwa kuchomwa moto nao wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema tukio hilo lilitokea Machi 1 mwaka huu katika kijiji cha Msinyeti wilayani Kongwa.
 
 Alimtaja aliyeuawa kuwa, Saidia Chakutwanga (80) anayedaiwa kuwa ni mganga wa jadi maarufu kama sangoma kwa kupigwa kwa kitu kizito kichwani na kutobolewa macho.
 
Alisema mauaji hayo yalitokea kwenye Kitongoji cha Golani baada ya wakazi wa eneo hilo kumtuhumu Chakutwanga kuzuia mvua isinyeshe.
 
 Misime alisema katika tukio la pili mume na mke, wameuawa katika kijiji cha Ihanda wilayani Kongwa wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe.
 
Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Peter Kaluli (85) na mke wake,  Kaila Kaluli (80).
 
Alisema uchunguzi uliofanywa na polisi umebaini watu hao waliuawa kutokana na imani za kishirikina wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe kijijini hapo.
 
Alisema siku ya tukio Kaluli na mkewe wakiwa wamelala kwenye nyumba yao ya tembe walivamiwa na kundi la watu ambao walibomoa ukuta wa kisha kuichoma moto nyumba hiyo na kusababisha vifo vyao.  Aliongeza kuwa katika tukio hilo, nguruwe mmoja aliuawa huku ng’ombe mmoja akikatwa katwa miguu. 
 
Misime alisema watu wanne, akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji na Wazee wa Kimila wawili wa Kijiji cha Ihanda (majina yanahifadhiwa),  wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
 

Alisema viongozi hao wanashikiliwa na polisi kwa sababu kabla ya mauaji hayo kulifanyika kikao ambacho kiliibua masuala hayo ya tatizo la mvua. Chanzo Nipashe

No comments:

Post a Comment