Pages

Saturday, March 21, 2015

WAZAZI EPUKENI KUGOMBANA MBELE YA WATOTO.....UGOMVI WENU UNAWAATHIRI WATOTO KISAIKOLOJIA

Umri kuanzia mwaka 0-6 ni kipindi ambacho wazazi wengi hudhani kwamba watoto wao hawawezi kujua/ kuelewa/ kujifunza kitu chochote kutoka kwao, huku wengi wakidhani kwamba ni umri ambao mtoto hawezi kuelewa hili ni jema na hili ni baya.
Hata hivyo, wataalamu wa afya kutoka nchini Marekani wanaonya kwamba kipindi hicho mtoto ana uwezo mkubwa wa kuelewa mambo, hasa yaliyo hasi na humkaa kichwani hata anapokuwa mzee.
“Kinachotokea huwa hawezi kusema kwa wakati huo, lakini ile picha ya tukio na hata maneno huendelea kumkaa kichwani kwa miaka mingi na kamwe huwa hasahau licha ya kwamba ataishi siku nyingi zenye matukio makubwa zaidi ya hayo, ila tukio kuhusu watu aliowapenda mwanzo (wazazi) huwa halifutiki,” alisema Dk Jones McDonald kutoka Chuo Kikuu cha California.
Kauli ya mtafiti na mwanasaikolojia huyu, inalandana na elimu ambayo hutolewa mara kwa mara na taasisi za haki za binadamu kuhusu ukatili majumbani na namna unavyoweza kuwaathiri watoto kisaikolojia na kupoteza kujiamini kwao, hivyo kushindwa kumudu maisha wawapo watu wazima.
Ushuhuda
Msichana mmoja anayejitambulisha kwa jina la Zawadi, anasema kuwa hatasahau wazazi wake walipoingia katika mgogoro ambao ulisababisha uharibifu nyumbani, baada ya kurushiana vitu akiwa na umri wa miaka mitatu.
“Nakumbuka hiyo siku baba aliwahi kurudi baaya hapo mama akarudi na kuingia jikoni kupika alikuwa amekaanga vitunguu katika chungu cheusi akitumia jiko la umeme, ghafla baba akaja na kupiga teke chungu kikavunjika na kuanza kumshambulia mama, sijui ugomvi halisi ilikuwa nini maana niliwasikia ila sikuwaelewa na sikumbuki walikuwa wakizozana kuhusu nini,” anasimulia Zawadi mwenye umri wa miaka 29 sasa.
Binti huyu aliyeolewa sasa na ana watoto wawili anasema huwa anafikiria hatua hiyo ngumu ambayo aliiona kwa wazazi wake ikimtokea katika ndoa yake itakuwaje, “japokuwa sikuona tena ugomvi baina yao, huwa nafikiria ikitokea kwangu itakuwaje, mume wangu hukasirika wakati mwingine ila hajawahi nipiga, wala kunifokea.”
Benson ni mwanaume ambaye alishuhudia ukatili aliowahi kufanyiwa mama yake mzazi na baba yake siku walipoachana akiwa na umri wa miaka minne.
“Ile picha huwa hainitoki kichwani, nakumbuka baba alimpiga mama yangu mpaka akamtoa nje kwa majirani na kumpigia huko akiwa amevalia khanga pekee, tukio lile lilimkasirisha mno mama yangu na tangu hapo aliamua kuondoka akiwa na ujauzito wa mdogo wangu wa kike,” anasema Benson mwenye miaka 40 sasa.
Anasema anakumbuka kikao kilifanyika kijijini kwao Moshi miaka mitatu baadaye wakati huo akiwa na miaka saba, ambacho kilimtaka mama yake arudi kwa mumewe jambo ambalo mama yake hakuliafiki.
“Huwezi amini baada ya kuondoka kwa baba, mama yangu alianza biashara na kufanikiwa kimaisha na aliweza kutusomesha wote bila shida. Leo nina maisha mazuri, elimu, mke na watoto sitaki kabisa kumnyanyasa mke wangu hata akinikosea huwa namwambia kwa utaratibu, maana najua tabu aliyoipata baba na kuyumba kimaisha kwa kuwa hakuwa na mwongozo, kwani alipenda sana uhuru uliopitiliza,” anasema.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment