Pages

Saturday, April 18, 2015

HATIMAYE YULE MZAZI FEKI WA MTOTO WA CHEKECHEA AMEHUKUMIWA KWENDA JELA MIEZI 6 KWA KUIDANGANYA MAHAKAMA

Hatimaye mwalimu wa chekechea, Mollen Calleb, aliyesimama mahakamani kwa kujifanya mzazi wa mtoto wa miaka miwili aliyejeruhiwa kwa kupigwa na mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuidanganya mahakama.
Katika tukio hilo, mwalimu huyo aliidanganya mahakama na kusababisha kesi hiyo ya kujeruhi kufutwa bila mlalamikaji kuwapo mahakamani.

Machi 27, mwaka huu, katika Mahakama ya Mwanzo Ilemela, jijini Mwanza, ilifuta kesi ya kujeruhiwa mwanafunzi, inayomkabili mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day Care, Siwema Bujota, anayedaiwa kumpiga mtoto huyo na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili.

Bujota aliyekuwa na dhamana ya kulea watoto shuleni hapo, alimjeruhi mwanafunzi wa miaka miwili (jina limehifadhiwa), kwa kumchapa  viboko maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa madai kuwa alijisaidia haja kubwa shuleni.

Baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, mwalimu wa shule hiyo, Calleb alikwenda mahakamani na kujitambulisha kwamba  yeye ndiye mlalamikaji wa kesi hiyo na kuiomba mahakama kuifuta kwa madai kuwa hakuwa na nia ya kuendelea na mashitaka na kwamba watamalizana nje ya mahakama.Kutokana na maelezo hayo, hakimu aliyetambulika kwa jina moja la Misana wa mahakama hiyo,  alifuta kesi hiyo bila kujua kama huyo aliyesimama mahakamani si mlalamikaji halali.

Mlalamkaji katika kesi hiyo alikuwa Sabrina Hamis, ambaye kabla ya kesi kuanza kusikilizwa alikwenda hospitali kwa matibabu ya mtoto huyo, ambaye hali yake ilibadilika ghafla.

Kufuatia tukio hilo, Hamis alikwenda  kutoa taarifa  kituo cha Polisi cha Kilumba, kulalamikia kesi yake kufutwa kinyemela.
Jeshi la polisi mkoani Mwanza  lilianza kuwasaka watuhumiwa wote wawili akiwemo mshtakiwa na mwalimu aliyejifanya mlalamikaji.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda, Kamishina Msaidizi wa Polisi jijini Mwanza (ACP), Japhet Lusingu, alisema kuwa Aprili 13, mwaka huu,  watuhumiwa hao walikamatwa.

Alisema Aprili 14, mwaka huu  walifikishwa mahakamani na kupata taarifa kwamba mwalimu huyo amefungwa miezi sita kwa kuidanganya mahakama.


NIPASHE ilizungumza na mlalamikaji ambaye alisema mwalimu huyo amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kuidanganya mahakama. Aidha, alisema mtuhumiwa alipelekwa rumande hadi Aprili 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment