Pages

Monday, April 20, 2015

KUTOKANA NA MACHAFUKO YANAYOENDELEA AFRIKA KUSINI, UBALOZI WANAJIANDAA KUWAONDOA WATANZANIA WALIOKO HUKO....MAOFISA WAMEPELEKWA KUANGALIA HALI ILIVYO..

UBALOZI wa Tanzania nchini Afrika Kusini umesema umeanza utambuzi wa Watanzania waishio katika maeneo ya hatari nchini humo kabla ya kuanza hatua za kuwaondoa na kuwarejesha nyumbani.
Hatua hiyo inatokana na kushamiri kwa mashambulizi yanayofanywa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya raia wa kigeni ambapo hadi kufikia jana watu sita wameuawa.

Taarifa zilizopo hata hivyo zinasema kwamba hakuna raia wa Tanzania ambaye ameuawa au kujeruhiwa katika vurumai hizo ambazo zimeanza Durban, Kwa- Zulu Natal.

Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, amesema kwamba Ubalozi Afrika Kusini umepeleka maofisa wake katika mji wa Durban kuangalia hali ilivyo. 

Kasiga amesema kwamba serikali imeshatoa 
mwongozo wa namna ya kuwaondoa raia wake nchini Afrika Kusini.
“Utaratibu wa kuwaondoa Watanzania upo tayari, lakini itambulike kwamba si kila Mtanzania anayeishi Afrika Kusini ataondolewa bali wale walio katika maeneo hatarishi.

“Tutawaondoa Watanzania ambao wanaishi katika mazingira yaliyotishio au wale ambao mali zao zimeharibiwa,” alisema Kasiga akizungumza na gazeti dada Daily News kwa njia ya simu jana.

Alisema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye yuko nje kwa safari ya kikazi atatoa taarifa mara tu atakapowasili nchini.

“Kwa sasa waziri yupo nchini Jordan lakini atakuwa na nafasi ya kuzungumzia suala hili mara tu atakaporejea siku chache zijazo,” alisema Kasiga.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment