Pages

Tuesday, April 21, 2015

Kutokana na vurugu zinazoendelea Afrika Kusini, Watanzania 23 wamenusurika kuuawa kwa kujificha supermarket

SERIKALI imesema Watanzania 23 wamenusurika kuuawa katika ghasia zinazoendelea nchini Afrika Kusini baada ya kujificha kwenye duka kubwa (Supermarket).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hadi jana hakuna taarifa za Mtanzania aliyepoteza maisha.

Alisema katika vurugu hizo, watu wanane ambao walifariki dunia wanatoka nchi za Malawi, Msumbiji, Ethiopia, Zimbambe, Swaziland na Somalia.

Alisema baada ya Serikali kupata taarifa hizo, waliwasiliana na Serikali ya Afrika Kusini pamoja na ubalozi wa Tanzania nchini humo ili kupata taarifa kamili kuhusu suala hilo.

“Tuliwasiliana na ubalozi wetu kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini, wametuhakikishia hakuna Mtanzania hata mmoja aliyefariki dunia katika vurugu hizo,” alisema Membe.

Hata hivyo, alisema kuna taarifa ya vifo vya Watanzania watatu waliofariki dunia katika matukio tofauti na majina yao yamekuwa yakisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Aliwataja kuwa ni Ali Hashim Mohamed aliyefariki kwa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ambaye mwili wake umewasili nchini juzi na Athuman China Mapepo aliyefariki baada ya kuchomwa visu kwenye vurugu zilizotokea ndani ya gereza, akitumikia kifungo baada ya kushtakiwa kwa kosa la jinai.

Mwingine ni Rashid Jumanne ambaye aliuawa baada ya kushiriki tukio la wizi kwenye nyumba ya mtu.
Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, zaidi ya wananchi 3,000 kutoka mataifa mbalimbali walikimbilia kwenye kambi ya ‘Supermarket’ ili kunusuru maisha yao.

“Tayari tumewatuma maofisa ubalozi nchini Afrika Kusini kuzungumza na Watanzania waliopo kwenye kambi hiyo ili waweze kupata taarifa kamili juu ya mgogoro huo.

“Baada ya mazungumzo hayo, kati yao 21 wamekubali kurudi nyumbani, lakini wawili wamekataa,” alisema.

Alisema Tanzania inaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kulaani na kupinga vurugu hizo na kuitaka Serikali ya Afrika Kusini kuongeza juhudi za kuchukua hatua.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment