Pages

Wednesday, April 15, 2015

OFISA MTENDAJI MKUU WA RITA, PHILIP SALIBOKO AMESIMAMISHWA KAZI KWASABABU YA KESI INAYOMKABILI YA KUPOKEA MGAWO WA ESCROW

OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, amesimamishwa kazi.
Hatua hiyo inatokana na kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayohusu kupokea mgawo wa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kwa mujibu wa taarifa iliopatikana jana na kuthibitishwa na Saliboko mwenyewe, kusimamishwa kwake ni kutokana na sheria za utumishi wa umma.
Sheria ya utumishi wa umma inamtaka mtumishi yeyote anapokabiliwa na kesi kusimamishwa akisubiri hatima ya suala lake.  

Taarifa hiyo ilieleza kwamba  nafasi ya Saliboko inachukuliwa na Emmy Hudson ambaye anakuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Saliboko kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Wakati kesi hiyo ikifikishwa, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Denis Lekayo, alidai Saliboko anatuhumiwa kupokea rushwa ya sh. milioni 40.4, kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila.
 
Kwa mujibu wa Lekayo, fedha hizo ni sehemu ya zilizokuwa fedha za katika Akaunti Escrow na kwamba Saliboko alipokea fedha hizo kupitia akaunti yake iliyokuwa katika Benki ya Mkombozi.
 
Saliboko aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alitakiwa awe na fedha taslimu sh. milioni 22.

UHURU ONLINE

No comments:

Post a Comment