Pages

Sunday, April 26, 2015

Serikali imeanza kutekeleza agizo lake la kufuta asasi zinazoenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake...Asasi 24 kufutwa ndani ya siku 7 kuanzia jana....Zimo Tanzania Christian Outreach na Tanzania Muslim Social Community

Serikali imeanza kutimiza ahadi yake ya kuyafuta mashirika na asasi zisizo za kiserikali, NGO, yakiwamo ya kidini na kwa kuanzia imetangaza kusudio la kuzifuta asasi 24 katika kipindi cha siku saba kuanzia jana.

Miongoni mwa asasi hizo ni
taasisi mbili za dini ambazo ni Tanzania Muslim Social Community na Tanzania Christian Outreach Ministries ambazo zimepewa siku saba kujitetea.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Issack Nantanga aliliambia MWANANCHI kuwa asasi zote zitakazothibitika kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, zitafutwa.

Nantanga pia alisema panga hilo litazipitia pia asasi ambazo zimekuwa haziwasilishi kwa msajili ada ya kila mwaka na taarifa za fedha zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa.

“Haya mashirika 24 ndio tumeanza nayo na ukaguzi unaendelea. Tumetoa muda wa siku saba kuanzia leo (jana) kujitetea kwanini yasifutwe na wakishindwa kufanya hivyo, yatafutwa rasmi,” alisema.

Aliyataja mashirika mengine kuwa ni Kagwa Development Society, Morning Star Production Training Centre, Chama cha Kujitegemea na Kujiendeleza na The Organisation of Tanzania Community.

Mashirika mengine ni Mbezi Juu and Salasala Woman Agricultural and Environmen Association, Waridi Training Society, Vituka Machimbo Development Association na Gerezani Nguvukazi.

Mengine ni Nyakasangwe Small Scale Farmers Association, Vitendo Trust Fund, Bahari Beach Silvers and Woman Association, Owners Social Club na Magovent Development Association.

Kwa mujibu wa Nantanga, mashirika mengine yaliyomo katika orodha hiyo ni Hananasifu Quarters Women Association, Mburahati Barafu Development Community na The Movers Club.

Pia yamo Umoja wa Maendeleo ya Jamii Mlima Mindu, Tabata Tujiimarishe Club, Umoja wa Wauza Miche Ubungo, Kunguru/Kinzudi Development Association na Women & Environment Association.

“Ukitazama katika tovuti ya wizara utakuta tuna orodha ya mashirika 10,624 yaliyosajiliwa tangu 1953. Tutapitia moja baada ya jingine na yatakayobainika kukiuka sheria yatafutwa,” alisisitiza.

Wakati Serikali ikianza mchakato huo, imebainika kuwa baadhi ya klabu za waandishi wa habari za mikoa, nazo ziko hatarini kuangukiwa na rungu hilo kwa kutolipa ada. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya klabu hizo za waandishi wa habari hazina taarifa za fedha zilizokaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa na wala taarifa hizo haziwasilishwi kwa msajili.
Hatua hiyo ya Serikali kuanza kuyafuta mashirika hayo imekuja takribani wiki mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kutangaza mpango wa kuyafuta mashirika yanayokiuka sheria.

Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa siku chache baada ya taasisi za dini nchini kutoa matamko mbalimbali kluhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya, likiwamo Jukwaa la Wakristo ambalo liliwataka waumini kuikataa Katiba Inayopendekezwa kwa kuipigia kura ya hapana.

Jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT).

Jukwa hilo linadai kuwa Serikali imewaahidi Waislamu kuingiza Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba ili waipigie kura ya ndio Katiba Inayopendekezwa, jambo ambalo limesema linaweza kusababisha mgawanyiko.

Tamko hilo lilijibiwa na taasisi za Kiislamu zilizosema kuwa suala la Mahakama ya Kadhi ni haki yao na kuwataka viongozi hao wa Kikristo kuwaacha waumini wake wajiamulie wenyewe mambo ya Katiba.

Katika tamko lake, Chikawe alizionya taasisi hizo za kidini dhidi ya kujihusisha na shughuli zilizo kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake, akitaja kitendo cha kuwataka waumini wapige kura ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa.

Pia zilitishia kutoikubali Katiba Inayopendekezwa iwapo Serikali haitatekeleza ahadi yake ya kuingiza suala hilo kwenye Katiba.

Chikawe alisema kuanzia Aprili 20, Serikali ingezifuta taasisi zote zilizosajiliwa chini ya wizara yake ambazo haziwasilishi taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za kisheria.

Chikawe alisema Serikali inatoa onyo kwa taasisi za dini ambazo zimetoa matamko ya aina hiyo kwamba wasirudie tena vinginevyo Serikali itakuwa haina njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuyafuta.

Alisema waumini wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao, lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao bila ya kushawishiwa na mtu yeyote kama sheria zinavyotaka.

“Mfano ni pale viongozi wa dini wanapochangisha fedha za kuandamana au kukutana na wanasiasa na kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema Chikawe.

“Hii si kazi ya taasisi za dini na ni kinyume na sheria,”
Hata hivyo uamuzi huo wa Serikali ulipokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa Dini, wakisema uamuzi huo una lengo la kuwafunga midomo wasikemee maovu.


Viongozi wa dini walienda mbali na kudai wamesema taasisi zao zinawakilisha watu hivyo zina haki ya kikatiba na kisheria kupinga jambo lolote zitakaloona linakwenda kinyume na maslahi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment