Pages

Sunday, April 12, 2015

Uzembe wa Daktari wa Upasuaji Wasababisha Mgonjwa Alipwe Milioni 25....Daktari huyo Aliacha Kitambaa Tumboni mwa Mgonjwa....Ikapelekea Mgonjwa Kuondolewa Mfuko wa Kizazi na Utumbo

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, kuwalipa fidia ya Sh25 milioni Mwamini Adam na mumewe Idrisa Jafari kutokana na madhara waliyopata baada ya uzembe uliofanywa na daktari wa Hospitali ya wilaya hiyo alipokuwa akimfanyia upasuaji Mwamini.

Katika uamuzi wa shauri hilo la madai Namba 13/2011 uliotolewa juzi, Mahakama Kuu imeiagiza halmashauri hiyo kumlipa Sh20 milioni Mwamini aliyepata kilema cha maisha kwa kuondolewa mfuko wa uzazi na kukatwa utumbo.

Pia, mahakama imeiagiza halmashauri hiyo kumlipa fidia ya Sh5 milioni Jafari ikiwa ni gharama za uendeshaji wa shauri hilo.

Akisoma hukumu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Amir Mruma alikubaliana na madai ya walalamikaji kuwa madhara waliyopata kutokana na uzembe uliofanywa na Dk Jackob Kamanda ni makubwa.

Jaji Mruma alisema haipingiki kwamba huo ni uzembe uliofanywa na mtumishi, hivyo mwajiri anapaswa kulipa gharama.

Aliagiza kuwa kiwango hicho cha fedha kitalipiwa riba ya asilimia saba kila siku kuanzia tarehe ya uamuzi ulipotolewa hadi siku mlalamikiwa atakapolipa fedha hizo.

Mwamini na mumewe walifikisha malalamiko yao Mahakamani Kuu, wakidai kulipwa fidia ya Sh505 milioni kutokana na makosa ya uzembe uliofanywa na wataalamu wakati wa upasuaji kwa kuacha kitambaa tumboni mwa mgonjwa.

Wakili wa walalamikaji, Jaji Mussa Kwikima aliiambia Mahakama kuwa uzembe huo umemsababishia kilema cha maisha mteja wake.

Awali, akiwaongoza wateja wake kutoa ushahidi, Wakili Kwikima, waliieleza Mahakama kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji, Mwamini alihamishiwa Hospitali ya Rufani Kitete, lakini hali ilizidi kuwa mbaya ikawalazimu kuhamia Hospitali ya Itigi kulikogundulika tatizo baada ya vipimo.

Walidai kuwa madaktari walibaini kuwa kulikuwa na kitu ndani ya tumbo la Mwamini kilichokuwa kinasababisha atokwe na usaha sehemu za siri na tumboni.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Anatory Lukonge wa Hospitali ya Itigi ambaye alimfanyia upasuaji Mwamini katika ushahidi wake, aliieleza mahakama kuwa walipomfanyia upasuaji walikuta utumbo umeshikana na kizazi huku juu yake kukiwa na kitambaa.

Dk Lukonge alisema walikitoa kitambaa hicho lakini kutokana na sehemu ya kizazi kuharibika, iliwalazimu kukiondoa huku akidai kuwa hali hiyo ilisababishwa na uzembe wa daktari aliyemfanyia upasuaji.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment