Pages

Tuesday, May 19, 2015

ASKARI JKT ADAIWA KUMUUA RAIA TANGA...ALIMPIGA NGUMI KICHWANI KATIKA KUAMUALIA UGOMVI

ASKARI wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyefahamika kwa jina la Ramadhani Hamisi (24), anadaiwa kumuua mkazi wa Mikanjuni, mkoani Tanga, Salim  Omary (21).

Tukio hilo linadaiwa kutokea Mei 17,
mwaka huu, wakati marehemu na mtuhumiwa wakiwa kituo cha kujiandikisha kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya uraia ambavyo vinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mtuhumiwa Hamisi anadaiwa kumpiga ngumi Salim Omary aliyekuwa akiamulia ugomvi uliotokea kati ya askari huyo na mama mmoja ambaye jina lake halikufahamika.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Zubery Mwombeki, alisema lilitokea saa 9:30 alasiri katika Shule ya Msingi Mikanjuni, Kata ya Mabawa, ambako kulikuwa na kituo hicho.

Alisema baada ya mama huyo kulalamika kuwa amekaa muda mrefu kituoni hapo bila kupata huduma ndipo ukatokea mzozo kati yake na askari huyo ambapo Salim iliingilia ili kuwaamua lakini akajikuta akipigwa ngumi ya kichwani na mbavuni.

"Marehemu alikimbizwa katika Kituo cha Afya Mikanjuni kwa ajili ya matibabu lakini jitihada za madaktari na wauguzi kuokoa maisha yake zilishindikana ambapo maumivu makali aliyopata ndiyo yaliyosababisha kifo chake," alisema.

Aliongeza kuwa, askari huyo anashikiliwa na jeshi hilo na atafikishwa mahakamani muda wowote.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa jiji hilo ambaye ni Diwani wa kata hiyo, Mzamin Shemdoe, alidai kupata taarifa za tukio hilo baada ya kupigiwa simu na wananchi wake.

"Nimepigiwa simu kuambiwa kuna askari wa JKT amempiga raia ngumi ya mbavu na kichwa baada ya kutokea mgogoro, tukio hili limenisikitisha sana," alisema.

MAJIRA

No comments:

Post a Comment