Nyumbani
kwako ni eneo lako la kuwepo ambapo unakutana tena na ndugu na wapendwa wako
baada ya siku ndefu na yenye uchovu mwingi. Je, ili uweze kujisikia amani ukiwa
nyumbani, si vyema kuwa na uhakika wa ulinzi na usalama kwenye lango kuu ili
kuwalinda mlioko ndani kutoka kwa walioko nje na wavamizi? Ni ukweli kuwa kila
mmoja anahitaji faragha kwa hivyo nawe unayesoma makala hii ni vivyohivyo. Kuwa
na lango kuu lenye vigezo vya msingi itakusaidia kupunguza muingiliano na ugeni
usio wa lazima kwenye makazi yako.
Katika
nyumba nyingi za kisasa, utaona lango kuu limekuwa ni kivutio,
na kwa lengo la
makala hii ambayo inazungumzia lango kuu na sio ule mlango mdogo pembeni wa
mtembea kwa miguu, nimefanya mahojiano na bwana Mmasi ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza
na kufunga malango katika makazi ya watu. Na hapa Mmasi anaanza na kueleza
faida za kuwa na lango kuu.
Kuna
faida kuu tano za kuwa na lango kuu la kuingilia nyumbani, anasema Mmasi. Nazo ni
ulinzi, kuboresha muonekano wa nyumba, kuongeza thamani ya nyumba, usalama wa
watoto wako na wanyama walioko kwenye makazi yako faida ya tano ni kuwa na faragha.
Wezi
ni wahalifu wanaoangalia fursa ya kuiba,
kwa mfano kama nyumba yako ina lango kuu la kuingilia na ya jirani haina,
unadhani ni nyumba ipi mwizi ataivizia zaidi? Kama umejibu “sio yangu”, basi
kuna uhakika mkubwa uko sahihi. Kuwa na gate
kunaongeza ulinzi wa nyumba.
Endapo
gate lako litakuwa limebuniwa kwa
sanaa yenye mvuto litakapofungwa hakuna shaka kuwa litaleta mvuto wa makazi
yako na hivyo kuongeza thamani ya mali (nyumba), anasema Mmasi. Huu ni ukweli
mtupu.
Lango
kuu linasaidia kuwaweka wanyama wako ndani, tuseme una mbwa mkali ambaye
anaweza kutoka na kudhuru watu pale unapokuwa umemfungulia kwa ulinzi.
Na
kuhusu faragha unajua ni kwa kiasi gani mpita njia navyoweza kupita popote nje
ya nyumba isiyokuwa na lango kuu, hasa kwa wale wanaoishi mijini. Nyumba
zisizokuwa na gate watu wanapitapita
tu popote.
Sasa
tukiwa tumeshaziona faida kuu tano za kuwa na lango kuu la kuingilia nyumbani hebu
tuangalie miundo ya malango haya kwenye nyumba nyingi za kisasa. Kwa Watanzania
wenye nyumba za kisasa kuna miundo mikuu miwili ya malango ya kuingilia kwenye
nyumba zao. Nayo ni yake ya kufungua
kama milango mingine ya nyumba, yani kwa mfano kama unavyofungua mlango wa
chumba chako cha kulala na muundo wa pili ni yale ya kuteleza kwenye reli.
Mwanzoni
wengi walikuwa na haya malango ya kufungua kama milango mingine ya nyumba,
kadri ubunifu unavyoongezeka wapo wanaoanza kuweka haya ya kuteleza.
Tukianza
na haya malango ya kufungu kama mlango wa chumbani ni kuwa nayo yapo ya aina
mbili. Lile lango lililo moja tu na unafungua upande mmoja na aina ya pili ni
lile lango lililo na pande mbili la kufungua huku na huko. Sasa kuamua ni
mtindo upi kati ya hii miwili inazingatiwa na upana wa njia panapofungwa lango.
Kama njia ina upana wa mita mbili (wapo wanaofanya nhadi mita mbili na nusu) basi
unaweza kuweka lango la upande mmoja. Na kama upana wa njia ni zaidi ya huo
inashauriwa kuweka lango la pande mbili la kufungua huku na huko. Pia nisisitize
kuwa malango ya aina hii yanapaswa kufunguka kwa ndani. Endapo utaamua kufungua
lango lako kwa nje basi uhakikishe una nafasi ya kutosha na hauko karibu na
barabara kwamba wakati wa kufungua haitaleta usumbufu kwa wengine. Na bila kusahau ni kuwa malango haya
yanatakiwa kufungwa eneo ardhi ni tambarare.
Sasa
tukiingia kwenye hii aina ya pili ambayo naweza kusema ni ya kisasa zaidi ni
hii ya lango kuu la kuteleza. Kama jina lake linavyosema kuteleza, ni kwamba
lango hili lina gurudumu ndogo ambazo zinateleza kwenye reli.
Ili
kuweza kusimika lango la kuteleza unapaswa uwe na eneo la kutosha kwenye upande
ambao lango litafungukia. Eneo hili liwe pana sawa na upana wa lango lenyewe.
Na malango ya aina hii hayana upande maalumu wa kufungukia, laweza kufunguka au
kushoto ama kulia kuendana na eneo ulilonalo la ziada liko upande upi. Kama
huna eneo hili kwenye upande mmojawapo wa lango basi fahamu kuwa huwezi
kusimika lango la kufunguka kwa kuteleza kwenye reli.
Lango
kuu la kuteleza linatakiwa liwe yamefungwa mota kwa kuwezesha kufungua na
kufunga. Ila kuna wenye nyumba wengi tu ambao pamoja na kuwa wana malango ya
mtindo huu lakini wanayafungua na kufunga kwa kusukuma kwenye reli kwakuwa bado
hawajaweka mota.
Mmasi
anamalizia na kukuambia wewe msomaji wangu kuwa umeshajua faida na mitindo ya malango
ya kuingilia nyumbani. Ni kazi kawako sasa kuamua ni mtindo upi utakaokufaa.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea
www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment