Pages

Monday, May 11, 2015

JAJI ANUSURIKA VURUGU ZA BODABODA

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Kasukulo Sambo juzi alinusurika katika mapambano yaliyoibuka eneo la Soko Kuu mjini hapa mkoani kati ya askari polisi na madereva wa pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama Bajaj, baada ya madereva hao kugoma na kufunga barabara kwa kulala kifudifudi.
Kitendo hicho kilisababisha kusimama kwa huduma ya usafiri katika barabara kuu inayounganisha mji ya Sumbawanga na Tunduma kwa saa kadhaa na kusababisha askari polisi kufyatua risasi hewani na kurusha mabovu ya machozi ili kuwatawanya.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika eneo hilo la tukio wakiwa na silaha nzito wakitumia usafiri wa gari lao lenye namba PT 1854 tayari kukabiliana na mgomo huo .

Licha ya madereva hao kulala kifudifudi barabarani, pia waliweka mbao zilizopigiliwa misumari kuzuia gari lolote lisipitie eneo hilo la tukio na kuchoma matari ya magari.

Miongoni mwa watumiaji wa barabara waliokumbwa na adha hiyo ni Jaji Sambo ambaye gari lake lilizuiwa na kunusurika kushambuliwa na madereva hao waliokuwa wamejawa na ghadhabu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Jaji Sambo alithibitisha kutokewa na mkasa huo na kwamba maofisa askari wa usalama barabarani waliingilia kati na hatimaye akaruhusiwa kupita eneo hilo na gari lake .

“Nilipofika eneo hilo nilikuwa madereva wa bajaji wakiwa wamegoma wakitaka kuonana na Mkuu wa Mkoa kwa kufunga barabara kuu …..walinizuia nisipite hadi askari polisi wa usalama barabara alipoingilia kati pia mlinzi wangu alilazimika kushuka gari akiwa tayari na bastola kwa kujihami…. “Hatimaye niliweza kupita hapo salama saliminik lakini mkasa huo umesababisha adha kubwa kwa watumiaji wengine wa barabara,“ alieleza Jaji Sambo.

Shughuli za kawaida katika soko kuu la mjini Sumbawanga zilisimama kwa muda wa saa moja baada ya jeshi la polisi mjini hapo kuvutana juu ya mgomo wa ghafla ulioitishwa na madereva wa pikipiki za magurudumu matatu maarufu kwa jina la bajaji.

Kaimu Kamanda Polisi mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Leons Rwegasira amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza kuwa bado jeshi hilo linatumia busara kulishughulikia tatizo hilo kabla ya kuanza kamata kamata.

Aliongeza kuwa hakuna majeruhi aliyeripotiwa wala uharibifu wowote uliotokana na vurugu hizo ambapo aliwasihi vijana kuacha kujichulia sheria mkononi na kuanza kurusha mawe kwenye gari la polisi.

Vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa moja zimetokea leo saa sita mchana ambapo madereva hao wa bajaj wanaotoa huduma za usafiri katika Manispaa ya Sumbawanga na vitongoji vyake vilisababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa mjini humo.

Mwenyekiti wa madereva hao, Fred Jackson alisema wameamua kugoma kutokana na utaratibu wanaoutumia askari wa usalama barabarani mjini Sumbawanga ambapo kila siku wamekuwa wakipanga kiwango cha makusanyo ya fedha kutoka kwao na hivyo kulazimisha makosa yasiyokuwapo.

Alisema wameshajipanga kugoma mpaka uongozi wa serikali utakapoyashughulikia malalamiko yao ikiwa ni pamoja na kuwabaini askari wa usalama barabarani wanaofanya ukamataji kwa lengo la kujipatia kipato na siyo kusimamia sheria.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment