Pages

Thursday, May 7, 2015

Kamati TLP yamvua Mrema uanachama.....Msajili msaidizi asema kamati haitambuliki kisheria

KAMATI ya Ukweli na Maridhiano ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), imetangaza kumvua uanachama Mwenyekiti wa chama hicho, Agustino Mrema.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam na MTANZANIA Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Joram Kinanda alisema kuwa kamati hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia kwa kina malalamiko yaliyokuwa yakimuhusu Mrema, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa mbali na Mrema wengine waliovuliwa uanachama ni Hamisi Mkadamu, Antoni Mapunda, Nancy Mrikaria, Dominata Rwechungura, Maxmilian Lymo, Richad Lyimo, Hamisi Mkumba na Stanley Temba.

Kinanda alisema kuwa wanachama hao wamevuliwa uanachama kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, toleo la 2005 Ibara ya 9.9 (c) na 2009 ibara 9.5(c).
Kinanda alisema kuwa maazimio hayo yamepelekwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa taratibu za kisheria pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa upande wake Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, alipotafutwa ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema kamati hiyo haitambuliki kisheria.


“Kamati hiyo haitambuliki kisheria, na hata Mrema mwenyewe amekuwa akipinga TLP kuwa na kamati ya aina hiyo na hata viongozi wake hawatambuliki, ” alisema

No comments:

Post a Comment