Pages

Monday, May 25, 2015

Mgombea uraisi CCM kujulikana July 12...Wagombea watachukua na kurudisha fomu bila shamrashamra

MGOMBEA Urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) atajulikana Julai 12 mwaka huu baada ya kukamilisha mchakato mzima wa kuomba kuwania nafasi hiyo, kutafuta wadhamini na kujadiliwa katika chama hicho.
Hayo yalielezwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza yanayoendelea katika siku ya pili ya kikao hicho Dodoma.

Alisema mchakato wa kupata wagombea wa CCM katika vyombo vya dola yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani kwa uchukuaji wa fomu utafanyika kuanzia Juni 3 hadi Julai 15 mwaka huu.

Gharama za fomu hizo hazijapanda zimebaki vile vile kama zilivyokuwa mwaka 2010 na katika kanuni, yaani shilingi milioni 1 kwa urais, shilingi laki moja kwa ubunge na elfu hamsini kwa diwani.

Akifafanua zaidi alisema kwamba, wagombea Urais wataanzania kuchukua fomu,bila mbwembwe kuanzia Juni 3 na kutakiwa kurejesha fomu hiyo mwisho saa 10 ya Julai 2 mwaka huu katika mazingira hayo hayo ya kutokuwepo na shamrashamra.

Aidha alisema kuanzia tarehe hiyo ya uchukuaji fomu hadi marejesho yake, wagombea watakuwa wanatafuta wadhamini 450 kutoka mikoa 15 nchini huku mikoa mitatu ikiwa ni kutoka Zanzibar na angalau mkoa mmoja uwe wa Unguja au kisiwa cha Pemba.

Ongezeko hilo la mikoa na wadhamini linatokana na haja ya kutafuta sampuli inayooana na idadi ya watu na mikoa kwa sasa. Tanzania ina mikoa 31.

Uchaguzi uliopita wagombea walitakiwa kutafuta wadhamini 250 katika mikoa 10, minane ikiwa ni kutoka Bara. Alisema wagombea urais hao wanapokwenda kutafuta wadhamini, wajumbe wote wa mkutano mkuu wa taifa hawataruhusiwa kuwa wadhamini, huku mwanachama atakayekuwa mdhamini akizuiwa kufanya udhamini wa zaidi ya mtu mmoja.

Kwa anayewania Urais wa Zanzibar tarehe za kuchukua na kurejesha ni zile zile za Jamhuri, huku akitakiwa kupata wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu, mmoja ukiwa ama Unguja au Pemba.

Alisema vikao vya kuchuja wagombea Urais Zanzibar vitafanyika kuanzia Julai 4 hadi 10 ambapo Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM itamtaja Mgombea Urais wa Zanzibar.

Aidha wajumbe wote wa NEC hawaruhusiwi kumdhamini mgombea Urais wa Zanzibar. Akizungumzia fomu za wagombea Ubunge, alisema kwamba wanachama watachukua fomu hizo Julai 15 na kuzirejesha Julai 19 na mikutano ya kampeni itafanyika kuanzia Julai 20-31 ili kuomba kura.

Kura ya maoni ya kuwapata wanaowania nafasi ya Ubunge kupitia CCM itafanyika Agosti 1, mwaka huu. Kwa wanaowania Viti Maalumu ratiba ni ile ile, lakini safari hii mchujo wa mwisho utafanywa na Baraza kuu la UWT ambao kimsingi ndio wanaomiliki viti hivyo maalumu, ingawa mchujo wa awali utafanyika katika jumuiya husika.

Viti maalumu safari hii vitawaniwa pia na jumuiya ya wazazi ambao wamepewa viti viwili.Jumuiya nyingine ni jumuiya ya vijana, UWT yenyewe,jumuiya ya wasomi, wafanyakazi na wenye ulemavu.

Ratiba ya kuwania udiwani nayo ni Julai 15 hadi 19 na kura za maoni zitafanyika Agosti Mosi. Katibu huyo wa NEC hata hivyo aliwatahadharisha wanaowania nafasi hizo za dola kupitia CCM, kuangalia kwa makini kanuni za uchaguzi za chama hicho, kuzisoma na kuzielewa kwa kuwa kama watafanya kosa litawagharimu ,huku akisisitiza ‘kosa moja goli moja’.

Akizungumzia namna ya kufanikisha kura ya maoni alisema chama chake kitafunga daftari la wanachama Julai 15 na wapiga kura wa chama hicho watalazimika kuwa na zaidi ya kadi ya chama kwa utambulisho ikiwamo kadi ya kupiga kura ili kushiriki kura ya maoni.

Alisema nia ya kuweka vitambulisho viwili ni kuzuia wapiga kura bandia ambao safari iliyopita walionekana kuwa chanzo cha matatizo. Aidha, wanafanya hivyo ili kuzuia wasioitakia mema CCM kula njama ya kuiangusha kupitia matumizi ya kadi bandia.

Aidha alisema ipo mikakati ambayo tayari inafanyiwa kazi kuhakikisha mchakato mzima hadi kura wa maoni unafanikiwa kuwapa Watanzania kile wanachokihitaji.

Pia alisema wagombea wote watakuwa pamoja katika mikutano ya kuomba kura. Akijibu swali maana ya maelekezo ya sasa kama ni hakikisho Katiba mpya haitakuwepo, Nape alisema CCM inafanya utaratibu wake kwa kuzingatia Katiba iliyopo sasa na kama katiba mpya itakuja watakutana kufanya mabadiliko yanayohitajika.

Mpaka gazeti hili linaenda mtamboni jana Kikao cha halmshauri Kuu ya CCM kilikuwa kinaendelea.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment