Pages

Saturday, May 2, 2015

Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sofia Mjema akemea ngoma za vigodoro, chipsi na simu kwa wanafunzi

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, amewataka wazazi  kuwa na tahadhari na ngoma za vigodoro, chipsi kuku na simu za mikononi baada ya kuonekana kuwa vyazo vikuu vya wanafunzi wa kike kukatisha masomo na kupata mimba.

Akizungumza katika
maadhimisho ya wiki ya elimu, Mjema alisema anasikitishwa na baadhi ya wazazi wanaokwepa majukumu yao kwa kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika vitendo hivyo na kusababisha elimu kuporomoka.

Hata hivyo, aliwapongeza watendaji na wadau wa elimu kwa jitihada zao za kuisaidia wilaya hiyo hadi mwaka huu kuwa ya kwanza mkoa wa Dar es Salaam kwa kufaulisha wanafunzi zaidi ya asilimia  70 .

Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kata ya Kijichi yaliandaliwa pamoja na Manispaa Temeke, taasisi ya kijamii ya  Ocode na Shirika la Kimataifa la We World ambapo baadhi ya shule na wanafunzi waliofanya vizuri walipewa zawadi.

“Haiwezekani mtoto anatoka masaa matatu bila taarifa halafu mnakuwa kimya, muda huo ni mwingi  kwa binti kuharibu maisha yake, ngoma za vigodoro na safari za ufukweni si salama lazima tuhakikishe tunawajibika kuwakemea,” alisema Mjema.

Alisema mwaka huu waliamua kufanya kazi maalum kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu ambapo matunda yake yameonekana baada ya ufaulu kuongezeka kwa shule za msingi na sekondari.

Alisema ufaulu kwa shule za msingi ulikuwa asilimia 72 mwaka jana kutoka asilimia 60 mwaka 2003 na asilimia 64 kutoka chini ya asilimia 50 kwa sekondari.

“Ufaulu huu umeonyesha jinsi tulivyoamua kuwa pamoja kati ya serikali na wadau kuhakikisha elimu yetu inakua kwa kasi, nawapongeza na nawataka kuongeza kasi zaidi ili tuongoze ngazi ya Taifa,” alisema.

Mratibu wa Ocode, Joseph Jackson, alisema kwa kushirikiana na We World wametumia jumla ya Sh. milioni 655.9 kwa ajili ya kuboresha mazingira na utendaji wa kazi ya walimu kwa shule nne za msingi.

Alizitaja shule zilizonufaika kuwa ni Kijichi, Bwawani, Kibondemaji na Buza.

Alisema shule hizo zimeboreshwa kwa kukarabatiwa madarasa, mitandao ya maji, jiko kwa ajili ya kupikia chakula cha wanafunzi pamoja na ununuzi wa madawati kwa shule hizo.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment