Pages

Friday, May 22, 2015

MTOTO MIAKA 15 AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMNYONGA MWENZAKE MIAKA 9....ZIPO TAARIFA PIA HUENDA ALIANGUKA GHAFLA SEBULENI

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kolla Hill, Judith Chomile (15) kwa tuhuma za mauaji.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kumnyonga ndugu yake, Edrin Mafwele (9) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Benard Bendel iliyopo Manispaa ya Morogoro.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati watoto hao walipokuwa nyumbani kwao.
Baba wa marehemu Edrin Mafwere aliyefahamika kwa jina la Barnabas Mafwele, mkazi wa eneo la Kola, alisema jana kuwa mtoto wake alinyongewa chumbani.

“Kabla ya kifo hiki, Mei 10 mwaka huu, majira ya usiku, mwanangu Edrin alipiga kelele na kusema kuna mtu alikuwa ameficha uso wake kwa kitambaa akitaka kumkaba shingo.

“Wakati anapiga kelele sisi tulikuwa sebuleni na tulipomuuliza mtu huyo yukoje alisema anafanana na dada yake Judis ambaye ni mtoto wa ndugu yangu.

“Baada ya muda kidogo tulimuona Judith akiingia ndani na tulipomuuliza alikuwa wapi alisema alikuwa amekwenda dukani.

“Baada ya tukio hilo niliwahoji watoto hao na baadaye nikawaacha na leo mtoto wangu amefariki dunia kwa kunyongwa.

“Ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa nani alimnyonga mtoto huyo, hapa nyumbani tumepata khanga iliyotapakaa damu, tumepata kitanzi kilichotengenezwa kwa nguo na vitu vyote hivyo ni vya hapa hapa nyumbani kwangu,” alisema Mafwele.

Wakati mzazi huyo akisema hayo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, Benald Paul, alisema taarifa alizozipata zinaonyesha mtoto huyo alifariki dunia baada ya kuanguka ghafla alipokuwa sebuleni.

“Taarifa zetu zinasema mtoto huyo alianguka ghafla akiwa sebuleni na alipopelekwa katika hospitali ya mkoa iligundulika kuwa alikuwa amekwisha kufariki dunia.

“Hata mtuhumiwa Judith tulipomhoji, alituambia marehemu alianguka na kutokwa damu puani pamoja na mkojo baada ya kupoteza fahamu.

“Hata hivyo, bado tunaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa ajili ya kupata uhakika zaidi wa tukio hilo,” alisema Kamanda Paul.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment