Pages

Thursday, May 14, 2015

MTU MMOJA APIGWA RISASI NA JAMBAZI SINZA DAR ES SALAAM

MTU mmoja ambaye jina lake halikufahamika amepigwa risasi mbili na kuporwa fedha na mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi katika eneo la Kijiweni Karibu na Baa ya Delux, Sinza, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea jana ambako MTANZANIA lilifika na kuelezwa na mashuhuda wa tukio hilo waliodai lilikuwa la kushtukiza na lilitokea saa 6.00 mchana.

Akisimulia tukio hilo dereva aliyekuwa akiendesha gari lililoshambuliwa namba T 236 DDT aliyefahamika kwa jina moja la Abasi, alisema fedha ambazo majambazi hao walichukua walikuwa wamezitoa benki eneo la Mlimani City.

Dereva huyo hakutaja kiasi chake lakini mashuhuda wa tukio hilo walisema kiasi kilichoibwa na majambazi hao ni zaidi ya Sh milioni 10.

“Baada ya kuingia na kuegesha gari hapa jirani na hopitali hii ya watoto, alikuja mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi akiwa ameshuka kwenye pikipiki ya Boxer na alipofika alisogelea gari letu na kufunua koti lake alilokuwa amebeba bunduki ya SMG,” alisema.

Alisema mtu huyo alimuelekezea silaha mtu aliyekuwa nyuma ya gari na kumuamuru kutoa fedha, amri ambayo haikutekelezwa kwa kumueleza mtu huyo anayedhaniwa kuwa ni jambazi kuwa hakukuwa na fedha ndani ya gari.

“Baada ya kuona anabisha alimpiga risasi ya kwanza, akageuza SMG kwangu nikakimbia, akafyatua lakini hakunipata ndipo nikasikia risasi nyingine ikipigwa,” alisema.

“Baada ya muda kulikuwa kimya na niliporudi tena nikakuta majambazi wakiwa wameshaondoka na mkoba wa fedha ‘briefcase’ na kutokomea nao hali iliyofanya wananchi kusogea na kumsaaidia mzee ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi,” alisema Abasi.

MTANZANIA ilipomuuliza dereva huyo kiasi cha fedha kilichoibiwa alisema majambazi hao waliondoka na kiasi kidogo cha fedha na siyo zote Sh milioni 10.


Baada ya tukio hilo polisi walifika katika eneo la tukio na kuzoa kipande cha mwili wa majeruhi huyo kilichokuwa kimedondoka sakafuni pamoja na maganda matano ya risasi.

No comments:

Post a Comment