Pages

Wednesday, June 10, 2015

CCM Yamsajili Darasa la Saba Kugombea Uraisi

Mkulima kutoka Kigoma, Elidephonce Bilohe akiondoka baada ya kushindwa kuchukua fomu kutokana na kutokamilisha malipo ya ada ya fomu hizo. Hata hivyo, alikamisha baadaye na atachukua fomu leo Picha na Edwin Mjwahuzi 
Makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwamo wa darasa la saba, jana walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na chama hicho wagombee urais.

Waliojitokeza ni Dk Mwele Malecela, Dk Hamis Kigwangalla na Elidephonce Bilole mwenye elimu ya darasa la saba ambao walifika Makao Makuu ya CCM kati ya saa nne asubuhi na saa saba kwa staili tofauti kwa ajili ya kuchukua fomu hizo.

Hata hivyo, Bilole (43) aliyetembea kwa miguu huku akiwa amebeba chupa mbili za maji, mfuko wa plastiki na begi dogo jeusi, hakuweza kuchukua fomu kutokana na kufika katika ofisi hizo akiwa hana Sh1 milioni za malipo.

Baadaye alifanikiwa kulipa ada hiyo na sasa amepangiwa kuchukua fomu yake leo saa 10.00 jioni.
“Nilikuwa Benki ya CRDB, nikaitwa ofisi za chama nikaona nije ili nisikilize wito, kabla ya kuchukua fedha kwanza,” alisema Bilole aliyefika peke yake kwenye ofisi hizo.

Bilole alisema anajua Mungu atamwezesha kukabiliana na watu wengine walioomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.

Alipoulizwa sababu ya kufika pekee yake katika ofisi hizo, alisema hajawahi kuwa na makundi ambayo yameonekana kwa makada wengine... “Nadhani naweza ndiyo maana nimejitokeza kuwania nafasi hii. 

Nitawavusha kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi,” alisema na kuongeza kuwa alijiunga na chama hicho mwaka 2003 huku akiahidi kuhakikisha anainua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Bilole ni nani?
Bilole alizaliwa Januari 21, 1971 katika Kijiji cha Mtala wilayani Kasulu mkoani Kigoma na anajishughulisha na kilimo.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment